MWILI wa kiongozi wa zamani wa Palestina, Yasser Arafat, umefukuliwa kutoka kaburi lake liloko ukingo wa Magharibi mjini Rammala ili kuwawezesha kuufanyia uchunguzi kubaini iwapo aliuwawa kwa sumu.
Bwana Arafat alifariki dunia mwaka 2004 nchini Ufaransa baada ya kuugua kwa kipindi kifupi. Maradhi yaliyopelekea kifo chake hayakubainika. Uamuzi wa kuufukua mwili wa Yasser Arafat katika kaburi lake lililoko ukingo wa Magharibi unafuatia makala ya televisheni iliyodai kupata mabaki ya madini ya kitonoradi aina ya Polonium kwenye nguo zake.
Wapalestina wengi wanashuku kwamba huenda Israel ilihusika katika kifo cha kiongozi huyo. Israel imekuwa ikikanusha shutuma hizo.
Uchunguzi wa mauaji dhidi ya Bwana Arafat umeanzishwa nchini ufaransa kufuatia ombi lililowasilishwa na mjane wake.
-BBC