EAC Yadai Utata wa Hali ya Usalama Waweza Athiri Uchaguzi Kenya

Rais wa Kenya Mwai Kibaki

Na Issac Mwangi, EANA-Arusha

MASUALA ya hali tete ya usalama yanaweza kuleta athari katika uchaguzi mkuu ujao nchini Kenya, Timu ya Tathmini ya Awali ya uchaguzi huo toka Jumuaiya ya Afrika Mashariki (EAC) imetahadharisha.

Kufuatia mwaliko wa kufanya tathmini ya awali ya uchaguzi huo, uliotolewa na Tume Huru ya Uchaguzi ya Kenya(IEBC), taarifa ya timu hiyo iliyonaswa na Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) imeleza: “Suala la Baraza la Jamhuri ya Mombasa, mgogoro wa Tana River, Kisumu na Baragoi” linahitaji kudhibitiwa ili kutoathiri ushiriki wa raia katika uchaguzi huo.

“Kamati ya usalama ya uchaguzi (Kamati za Usalama za Kitaifa, mikoa na wilaya) kwa kushirikiana na wakala nyingine za serikali zina nafasi muhimu katika jambo hili ili kuhamasisha uchaguzi kuwa wa amani,” ilieleza taarifa hiyo.

Timu hiyo ya EAC inayoongozwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Uganda, Dk. Bandru Kiggundu, imejumuisha wajumbe 30 kutoka kwenye tume za uchaguzi za taifa kutoka nchi wanachama, Bunge la Afrika Mashariki (EALA) na Sekretarieti ya EAC.

Wawakilishi kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa na Taasisi ya Uchaguzi na Demokrasia Endelevu Barani Afrika walishiriki pia katika utaratibu wa ushirikiano baina ya taasisi hizo na EAC.

Lengo la msingi la kufanya tathmini ya awali kati ya Novemba 15 na 16, mwaka huu ni kuhakiki hali ya utayari wa IEBC, vyama vya siasa, vyama vya kiraia na wadau wengine muhimu katika mwenendo mzima wa maandalizi ya uchaguzi.

Matokeo ya tathmini ya timu hiyo yanalenga kupelekwa kwa timu za EAC za uangalizi wa uchaguzi huo za muda mrefu na muda mfupi.

Pamoja na mambo mengine timu hiyo ya EAC imebaini kuwepo kwa maendeleo katika sheria za uchaguzi lakini imetoa wito wa kuwepo kwa utashi wa kisiasa ili kuwezesha sheria zilizopo kutoa utatuzi wa migogoro inayotokana na uchaguzi.

Huku timu hiyo ikipongeza ‘mabadiliko ya kisheria’ yaliokwishafanyika, timu pia imetoa wito wa kutungwa kwa sheria za masuala ya uchaguzi zilizosalia kama vile sheria ya Fedha za Kampeni, ambayo timu hiyo inasema itatoa uwazi zaidi na usawa katika uchaguzi.