JK Apokea Taarifa ya Ujenzi wa Kampasi za Tiba ya Afya

Rais Jakaya Mrisho Kikwete na ujumbe wa Wizara ya Afya na Mfuko wa Afya ya Jamii (National Health Insurance Fund) NHIF Bw. Emmanuel Humba Novemba 23, Ikulu jijini Dar es salaam

Rais Jakaya Mrisho Kikwete Novemba 23, 2012 amepokea taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa Kampasi mbili za tiba ya afya vinavyojengwa katika Chuo Kikuu cha Dodoma na Mloganzila huko Kisarawe, ambavyo pia vitatumika kama hospitali hapa nchini.
Rais Kikwete amepokea maendeleo ya ujenzi wa Kampasi ya Afya ya Chuo Kikuu cha Dodoma kutoka kwa Mkurugenzi wa Mfuko wa Afya ya Jamii (National Health Insurance Fund) NHIF Bw. Emmanuel Humba .
Ujenzi wa kampasi hii umeshaanza na kufikia hatua ya juu na hospitali inatarajiwa kuanza shughuli zake rasmi mwaka 2015.
Kulingana na Bw. Humba, maandalizi ya kufanikisha uanzishaji wa Chuo/ Hospitali hiyo vimeshaanza ambapo baadhi ya wataalamu wakiwemo Madaktari na watumishi wengine wako nchini na nje ya nchi kwa ajili ya masomo na mafunzo mbalimbali.
Chuo hicho kinatarajia kuwa na vifaa vya kisasa vya tiba vinavyokidhi mahitaji ya Afya na Elimu ya Udaktari wa kiwango cha Kimataifa.
Rais pia amepokea taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa Kampasi ya Mloganzila ambapo katika ujenzi na uanzishwaji wa Kampasi hizi zote, Rais Kikwete amesimamia kuanzia hatua za awali.
Kampasi ya Mloganzila ambayo ni sehemu ya Hospitali kuu ya Muhimbili inajengwa kwenye eneo la ekari 3800 na itakua sehemu ya kutolea mafunzo kwa wanafunzi wa udaktari na huduma za Afya, lakini pia itakua sehemu ya kutolea matibabu ya maradhi yote makuu na ya kawaida nchini.
Ujenzi wa Hospitali hii unatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Januari, 2013 na unatarajiwa kukamilika miaka miwili baada ya ujenzi.
Katika hafla hiyo Makamu Mkuu wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili Prof. Ephata Kaaya ametumia nafasi hiyo kumkabidhi Rais Kikwete Cheti cha Udaktari wa Public Health (Honoris Causa), kufuatia Shahada aliyotunukiwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi, Muhimbili Disemba, 2010 kwa Kutambua mchango wa Rais Kikwete katika kuendeleza Sekta ya Afya nchini.
Akitoa taarifa hiyo ya maendeleo kwa Rais Kikwete, Prof. Kaaya amesema tayari wataalamu na wafanyakazi wanaotarajiwa kufanya kazi katika kampasi ya Mloganzila wameshaanza mafunzo. Mara hospitali hiyo kubwa na ya kisasa itakapokamilika itakua na uwezo wa vitanda vya kulaza wagonjwa mia sita (600).
Rais Kikwete amewapongeza wataalamu wote kwa juhudi zao na kuwa ahidi kuwa lengo lake ni kuhakikisha nchi inaondokana na adha ya kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
Rais amesema moja ya lengo kubwa la serikali yake, ni kutoa kipaumbele katika sekta ya Afya ili kuhaklikisha watanzania wanapata huduma bora, kupanua mafunzo ya Afya na kuongeza wataalamu watakaoweza kutibu magonjwa yote makubwa hapa hapa nchini.
Rais amewaahidi watendaji wa Kampasi zote mbili kuwa atahakikisha ujenzi wa huduma hizi muhimu kwa Umma haukwami kwa sababu ya ukosefu wa pesa kwani ni jambo ambalo amedhamiria.