Makala: Uwongo na Ufisadi ni Kansa

Zitto Kabwe (Mb)

Na Zitto Kabwe

KATIKA kitabu chake kiitwacho Africa – Altered States, Ordinary Miracles mwandishi Richard Dowden anaelezea viongozi wa kiafrika kwa mfano wa Mwanafunzi aliyemfundisha nchini Uganda Willy Kiyingi. Willy alikuwa ni kijana mwenye akili nyingi sana shuleni. Alikuwa anashika nafasi ya kwanza kila siku darasani. Siku moja akaiba pesa za mwalimu wake, akaenda dukani kujinunulia suti na viatu. Kisha akapanda taxi kurudi kijijini na kushuka katikati ya soko la kijiji, watu wakamwona na kumshangilia. Siku ya pili akafukuzwa shule kwa kosa la wizi. Hivyo ndivyo Willy allivyokatisha maisha yake: kwa suti, viatu na taxi. Ufahari wa siku moja tu ukamaliza ndoto zote za maisha yake. Hii ni sura ya ufisadi katika mataifa mengi ya Afrika. Tanzania inao kina Willy wengi sana.

Mkutano uliopita wa Bunge ulidhihirisha namna ambavyo tabia za uwongo zinaweza kuhatarisha Taifa. Katika mkutano wa kabla ya mkutano wa Tisa wa Bunge, Mkutano wa Nane wa Bunge la Kumi, kulikuwa na tuhuma kadhaa dhidi ya Wabunge. Baadhi ya tuhuma zimegundulika kuwa ni za uwongo. Tuhuma zingine zimefunikwa tu bila kuzitolea maamuzi ya Kibunge. Lakini Mbunge yeyote makini alijua kuwa tuhuma zile zilitungwa kwa sababu maalumu – kupitisha Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini. Lakini Bajeti ile haikuwa na tishio lolote la kupitishwa. Waziri na Manaibu wake walikuwa wanaungwa mkono na wabunge wengi sana na hivyo hata kama Kamati ya Nishati na Madini ingetaka kuzuia Bajeti, Bunge linegipitisha. Badala yake Wizara ikaingia kwenye kutunga uwongo, kupata ushujaa wa siku chache na kisha kuaibika kwa kuonekana wanasema uwongo.

Wabunge na wananchi nao waliingia mtegoni. Wabunge waliitwa kwenye Ofisi za Wizara na kutajiwa wala rushwa. Wabunge wakawaka moto ndani ya Bunge. Ukisoma kumbukumbu za Bunge za tarehe 27 na 28 Julai utaona namna wabunge walicharuka. Walipoitwa kutoa ushahidi kwa yale waliyoyasema, wakabaki wanatoa macho kama mjusi aliyebanwa na mlango. Spika alipowasomea kuwa walikurupuka tu (walitumwa) wakabaki wanalalamika kuwa ‘kesi ya nyani anahukumu ngedere’ na kusahau kuwa duniani kote Mabunge hujiwekea taratibu za kujidhibiti. Wabunge wengine ni watu jasiri na wenye uzalendo usio na mashaka. Lakini umaarufu wa siku moja ukawaingiza kwenye historia ya kuwa watu wanaotumika.

Jambo ambalo wananchi hawalijui ni kwamba, siku ya uwasilishaji wa hotuba ya Wizara ya Nishati na Madini ndio siku ambayo Wabunge waliongezewa mishahara yao kimya kimya wakati Walimu na Madaktari wanalia. Suala hili halikuingia kabisa kwenye mjadala kwani wananchi waliwaona wabunge wanawasemea. Wakawapigia ngoma za furaha, wanawatetea. Juhudi zote za kupinga nyongeza zisizo halali za malipo ya wabunge zikasinyaa. Utawapinga mashujaa wanaopinga ufisadi?

Sio hivyo tu, wananchi wanaendelea kupumbazwa zaidi kwani badala ya maamuzi ya Spika kuzungumzia masuala ya msingi yaliishia kusema nani mwongo na nani kasamehewa. Suala la msingi linabakia, je Wabunge hawafanyi biashara na Serikali au mashirika yake? Hakuna mgongano wa kimaslahi kwa Wabunge kuendelea na biashara zao wakati wanashikilia nafasi zao za kisiasa? Majibu yote ni ndio.

Kuna kundi kubwa la Wabunge ambalo linafanya biashara na taasisi za Serikali. Mbaya zaidi wabunge wengine wanakaa kwenye kamati za Bunge ambazo zinasimamia sekta ambazo wao wanafanya biashara nazo. Kuna wabunge wanafanya biashara ya usafirishaji kwa njia ya barabara na ni wajumbe wa kamati ya Miundombinu. Hawa kamwe hawatataka kuona Reli zetu zinafanya kazi. Kuna wabunge wana miradi ya Umeme na ina mikataba na TANESCO ya kuuza umeme na wanakaa kwenye kamati ya Bunge ya Nishati na Madini. Kuna Wabunge ambao wanafanya biashara na TANESCO ya ugavi nk na wamo ndani ya kamati hiyo inayosimamia TANESCO. Kuna wabunge wanafanya biashara za madawa na wamo kwenye kamati ya Huduma za Jamii ambayo inasimamia Wizara ya Afya. Kuna Wabunge, sio wafanya biashara, lakini ni wajumbe wa Bodi za Mashirika ya Umma na wanakaa kwenye kamati za Bunge zinazosimamia Mashirika hayo!

Haya ndio masuala ya msingi ambayo yalipaswa kujibiwa na Kamati ya Bunge ya Maadili. Haya ndio masuala ambayo Bunge linapaswa kuyawekea utaratibu ili kuzuia ufisadi unaotokana na mgongano wa kimaslahi. Haya ndio masuala ambayo hayapati kabisa mjadala mpana licha ya juhudi mbalimbali za kuleta mjadala huu kwenye Umma. Mwaka 2007, 2008, 2009 na 2011 niliwasilisha Muswada binafsi Bungeni kutunga Sheria mpya maadili kwa kuweka miiko ya uongozi kupitia kifungu nambari 12 cha Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge ya mwaka 1988. Kifungu hiki kinataka Bunge kupitisha Maadili kwa Wabunge (Conflict of interest code). Toka mwaka 2004 ambapo kifungu hiki kiliwekwa kwenye sheria hii, hakuna juhudi zozote za kutekeleza takwa hili la kisheria. Wanapaswa kutekeleza takwa hili ndio wanaofadikika na kutokuwepo kwake, Wabunge.

Unapokuwa fisadi ni lazima uwe mwongo. Ufisadi na Uwongo ni kansa ambazo zinaondoa kabisa uwezo wa viongozi kuendsha nchi zao sawa sawa. Hapa Tanzania kusema uwongo ndio utamaduni wa kisiasa kiasi cha kwamba wanaosema kweli ndio huonekana waongo hata pale ukweli unapodhihiri. Fisadi asiposema uwongo atagundulika ufedhulli wake. Wafuasi wa ufisadi huamua kukaa kimya kwa mtindo ambao Paul Freire anauita ‘culture of silence’ yaani utamaduni wa kukaa kimya. Kila mtu anashiriki ufisadi kwa kukalia kimya ufisadi ambao umefanywa na mtu wake.

Watu wenye tabia za kifisadi hupenda watu wengine wote waonekane mafisadi pia. Hivyo huzusha uwongo na upuuzi wa kila namna ili jamii iseme ‘wote ni walewale tu’ na wanasiasa wa namna hii husaidiwa sana na vyombo vya habari. Njia pekee ya kuondokana na hali hii ni kuweka mifumo mizuri ambayo lazima itaumbua waongo na kushughulikia mafisadi na mafedhuli ambao kwao wizi na ubadhirifu ni sehemu ya maisha. Mfumo mmoja wapo ni Uwazi.

Kwa nini iwe zahama kila tunaposema viongozi wote wa kisiasa waweke mali zao wazi? Kwanini viongozi wa kisiasa waseme hiyo ni kuingilia maisha yao binafsi? Mtu anayetaka kuhifadhi maisha yake binafsi asiingie kwenye siasa. Anayetaka kufanya biashara zake asiingie kwenye siasa maana siasa inapaswa kuwa utumishi.

Mfano wa kijana Willy wa Uganda unaotolewa na bwana Dowden ni mfano unaowakilisha wanasiasa wengi sana na hata raia wa kawaida kabisa wa Afrika. Ufahari wa siku moja dhidi ya maendeleo endelevu. Kujionyesha kwa siku moja dhidi ya kuonekana kwa muda mrefu hata baada ya mauti kama ilivyo kwa Mwalimu Nyerere. Kwa tabia kama hizi za Willy rasilimali za Afrika zimekuwa zikibakwa na wananchi tunatazama. Viongozi wamekuwa wakisema uwongo bila kuadhibiwa kwa uwongo wao.Afrika inaendelea kudidimia katika lindi la umasikini. Nchi inapozidi kuwa tajiri zaidi, uwongo unakuwa mwingi zaidi na ufisadi unarutubisha uwongo huo.

Tusipoukataa uwongo kwenye siasa, tutaendelea kuishi na ufisadi daima dumu.