NIMEGUSWA na suala hili juu ya dawa ya Babu wa Loliondo, mkoani Arusha, hivyo nami nimeamua kutoa maoni. Kwa kuwa suala la tiba itolewayo na Babu wa Loliondo ni suala la kiimani, twaweza kulikabili na kulipima kwa kutumia vitabu vya imani. Katika Biblia Mathayo 24:24 Yesu anawaambia wanafunzi kuwa kkadiri mwisho wa dunia unavyokaribia, watajitokeza makristo na manabii wa uongo ambao watafanya miujiza mikubwa na maajabu ili kuwadanganya wengi. Katika ufunuo 16:13-14 Yohana alioneshwa katika maono ya siku za mwisho kule kisiwani Patmo kuwa roho chafu zitokazo katika kinywa cha Joka (yaani Shetani), kinywa cha mnyama na kinywa cha nabii wa uongo zitatokea. Hizi ni roho za Mashetani zifanyazo miujiza na maajabu makubwa. Lakini pia Paulo katika barua yake ya pili kwa Wathesalonike; 2 Wathesalonike 2:9-10, anatabiri kuwa siku za mwisho watakuja watu waliojazwa nguvu na Shetani na kufanya aina zote za miujiza na maajabu ya uongo.
Kwa hivyo unaweza kuona jinsi watu tunavyopaswa kusoma na kupambanua kati ya miujiza ya kweli na miujiza ya uongo. Na hii haiwezi kufanywa kwa kutumia usomi wa kibinadamu tu bali kwa kutumia upambanuzi wa kiroho unaotokana na Mungu mwenyewe. Unajua shida si muujiza, bali ni “Ni nani anayefanya miujiza hiyo” kwa sababu si Mungu tu anayefanya miujiza bali Shetani pia hufanya miujiza. Tofauti kati ya miujiza ya Mungu na miujiza ya Shetani ni kuwa miujiza ya shetani inalenga kuwafanya watu wakamatwe katika mitego ya shetani na ndo maana mara nyingi ukishaipokea miujiza hiyo huwa ni vigumu kujichomoa kwa sababu unakuwa tayari umeshanaswa na ikibidi shetani hukuua ili ufe ukiwa upande wake.
Tofauti na miujiza ya Mungu ambayo inalenga kuwaonesha juu ya upendo na huruma za Mungu kwa mwanadamu aliyeanguka dhambini na hii huwa haina matangazo kama biashara na haitendwi ovyoovyo tu wala kwa masharti kama tunayoshuhudia wengi wakitoa. Hata Yesu mwenyewe alipofanya miujiza alifanya baada ya kuona kuwa kuna hitaji la lazima kufanya hivyo. Soma Mathayo 12:38-39;16:1-4 na Matahayo 15:21-28, Marko 2:1-5. Hapa tunaweza kuona kuwa kiini cha miujiza ya Yesu ilikuwa kuwaonesha watu kuwa dhambi zao zimesamehewa na ndiyo maana mara nyingi utakuta akisema “dhambi zako zimesamehewa” Jukumu lililopo kwetu leo ingekuwa ni kuwafundisha watu waujue ukweli ili wayaache maovu na hapo ndipo uponyaji wa kweli utakapotokea na si kufanya miujiza kama bango la dini. Hakika yake kama hatutakuwa makini, muda si mrefu watu wengi watamwabudu Shetani kwa sababu tu miujiza iliyoenea kote!!!
Kwa mengi zaidi, tembelea blog yangu www.afrikayetu.blogspot.com
Angalizo: Maoni haya ni ya msomaji wa Thehabari hivyo hayana uhusiano wowote na uongozi wala wahariri wa mtandao huu.