HOTUBA YA MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA MWENYEKITI WA CCM KWENYE UFUNGUZI WA MKUTANO MKUU WA NANE WA CHAMA CHA MAPINDUZI, UKUMBI WA KIZOTA – DODOMA, TAREHE 11 NOVEMBA, 2012
Utangulizi
Mheshimiwa Dkt. Amani Abeid Karume, Makamu Mwenyekiti
wa CCM na Rais Mstaafu wa Zanzibar;
Ndugu Pius Msekwa, Makamu Mwenykiti wa CCM wa Bara;
Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Ndugu Benjamin William Mkapa;
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Waziri Mkuu;
Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ;
Viongozi Wakuu Wastaafu;
Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu Wilson Mukama;
Ndugu Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM;
Wageni wetu waalikwa kutoka vyama rafiki,
Ndugu zetu wa Vyama vya Siasa Nchini;
Waheshimiwa Mabalozi,
Viongozi wa Dini,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana;
Kama ilivyo ada, naomba tuanze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kukutana hapa Dodoma, siku ya leo, kwenye Mkutano Mkuu wa Nane wa Chama cha Mapinduzi.
Ndugu Wajumbe;
Karibuni Dodoma. Karibuni Mkutanoni. Nawapeni pole kwa safari. Tunamshukuru Mungu kwa kutuwezesha kufika salama na tuombe turejee makwetu salama. Kwa niaba yenu, niruhusuni niwashukuru wenyeji wetu, yaani wana-CCM na wananchi wote wa Dodoma, wakiongozwa na Alhaji Adam Kimbisa, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Dodoma na Mkuu wa Mkoa Dkt. Rehema Nchimbi, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa. Tunawashukuru kwa kutupokea vizuri na kwa ukarimu wao unaotufanya tujisikie tuko nyumbani katika huu mji ambao ndiyo Makao Makuu ya nchi yetu na Chama chetu.
Ndugu Wajumbe;
Napenda kuchukua nafasi hii kutoa pongezi nyingi kwa Halmashauri Kuu ya Taifa kwa matayarisho mazuri ya Mkutano huu wa Nane wa Taifa wa CCM. Natoa pongezi maalum kwa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa chini ya uongozi mahiri wa Katibu Mkuu Ndugu Wilson Mukama na Kamati zote za Maandalizi ya Mkutano kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya ya kuwezesha Mkutano huu kufanyika. Kwenu nyote nasema hongereni na asanteni sana.
Ndugu Wajumbe;
Karibuni tena Kizota. Nasikitika kwamba matumaini yangu ya kufanya Mkutano Mkuu katika ukumbi wetu wenyewe hayakutimia. Hii ni kwa sababu kazi ya matayarisho imechukua muda mrefu kuliko nilivyotazamia. Tumechelewa kupata kiwanja kilichokidhi mahitaji yetu na matazamio yetu. Kwanza tulipata kiwanja nyuma ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM). Lakini tukaona ni mbali mno na walipo wananchi. Tukaja kupata kiwanja kingine juu ya Kilimani Club ambacho hakikuwa kikubwa cha kutosha. Mapema mwaka huu ndipo tulipopata kiwanja eneo la Makulu ambacho kinakidhi sifa za kuwa kikubwa cha kutosha na kuwa karibu na katikati ya mji wa Dodoma. Tumekiafiki na matayarisho ya kuanza ujenzi yamekamilika. Leo asubuhi tumeweka jiwe la msingi kuzindua ujenzi wa Ukumbi wa Mkutano (Dodoma Convention Centre). Baadae utafuta ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya CCM na jengo la Hoteli ya Kisasa.
Wageni Karibuni
Ndugu Wajumbe;
Kama mjuavyo Chama cha Mapinduzi kina marafiki wengi Afrika na kwingineko duniani. Tumekuwa na mazoea ya kualikana katika mikutano mikuu yetu. Safari hii tumefanya hivyo tena. Kwa niaba yenu niruhusuni niwashukuru sana wageni wetu wote wa kutoka vyama rafiki Afrika na duniani kwa kukubali mwaliko wetu na kuja kujumuika nasi siku ya leo. Kuwepo kwao ni kielelezo tosha cha udugu na urafiki uliopo baina ya vyama vyetu na nchi zetu ambao hatuna budi kuudumisha, kuuendeleza na kuukuza. Hali kadhalika, nawashukuru Mabalozi wa Nchi za Nje na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa walioweza kuja kushiriki nasi katika sherehe za ufunguzi wa Mkutano wetu.
Ndugu Wajumbe;
Tunawakaribisha kwa furaha na upendo mkubwa viongozi na wawakilishi wa vyama vya siasa vya hapa nchini kwa kukubali mwaliko wetu na kuja kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM siku ya leo. Tunawashukuru kwa moyo wao wa uungwana kwani tofauti za vyama si uadui. Wamethibitisha jinsi demokrasia ya vyama vingi inavyozidi kustawi na kukomaa hapa nchini.
Nawashukuru sana pia, viongozi wetu wa dini na wananchi mbalimbali waliojumuika nasi. Kuwepo kwao ni jambo la faraja kubwa. Dua za viongozi wa dini zitasaidia kuponya na kuupa baraka mkutano wetu uende salama, uwe wa mafanikio na kuwafanya wale wote wasiokiombea mema Chama chetu watahayari na kufadhaika.
Karibuni Diaspora
Ndugu Wajumbe;
Napenda kuwatambua na kuwakaribisha viongozi na wananchama wa Chama chetu waliopo nje, Marekani, Italia, India na Uingereza. Ndugu zetu hawa kwa upenzi wao kwa Chama wamesafiri masafa marefu kuja kushiriki nasi. Hawa wanastahili pongezi maalum kwa jinsi wanavyopeperusha bendera ya CCM na kueneza sera zake. Naomba tuwape makofi ya nguvu.
Agenda ya Mkutano
Ndugu Wajumbe;
Agenda ya Mkutano Mkuu wa Taifa wa Nane wa Chama cha Mapinduzi ina mambo makuu manne. Kwanza kufanya marekebisho ya Katiba ya Chama cha Mapinduzi. Mengi ya marekebisho hayo yanatokana na uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Taifa katika kikao chake cha trehe 11 – 12 Aprili 2011 wa kufanya mageuzi ndani ya Chama. Miongoni mwa matunda ya mageuzi hayo ni kuundwa kwa Baraza la Ushauri na Wajumbe wa NEC kuchaguliwa Wilayani badala ya Mikoani.
Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, Halmashauri Kuu ya Taifa ina mamlaka ya kufanya marekebisho ya Katiba na marekebisho hayo kutumika. Hata hivyo, marekebisho hayo hayana budi kuletwa katika Mkutano Mkuu wa Taifa ili yaingizwe rasmi kwenye Katiba.
Ndugu Wajumbe;
Jambo la pili litakuwa ni kwa Serikali zetu mbili kutoa taarifa za maendeleo ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya 2010 – 2015 tangu baada ya uchaguzi mkuu hadi sasa. Vile vile, tutapokea Taarifa ya Halmashauri Kuu ya Chama kuhusu kazi za Chama kwa miaka mitano iliyopita. Jambo la nne na la mwisho ni kufanya uchaguzi wa Mwenyekiti, Makamu wake wawili na Wajumbe wa NEC wa Kundi la Zanzibar na Tanzania Bara.
Ndugu Wajumbe;
Tofauti na mikutano iliyopita, Halmashauri Kuu ya Taifa inapendekeza kuwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wajigawe katika makundi matano kujadili taarifa ya kazi za Chama na zile za utekelezaji wa Ilani. Kisha kila kikundi kitatoa taarifa ya maoni na mapendekezo yake. NEC ilifikiria iwe hivyo ili kutoa muda wa kutosha kwa wajumbe kujadili taarifa hizo muhimu katika utaratibu wa zamani wa mtu mmoja kila mkoa kuitwa kusoma, wajumbe hawapati fursa ya kutosha ya kuzijadili taarifa zinazotolewa.
Kuimarisha Chama Kazi Endelevu
Ndugu Wajumbe;
Katika hotuba yangu ya kushukuru baada ya kuchaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi kwenye Mkutano Mkuu wa Taifa Maalum wa tarehe 25 Juni, 2006, pamoja na kuzungumzia mambo mengine, nilisisitiza umuhimu wa kuimarisha Chama chetu. Nilitoa maoni yangu kwa upana kiasi kuhusu mambo ya kuzingatia. Leo tena, katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu huu narudia kusisitiza jambo hili. Nafanya hivyo kwa sababu hilo ndiyo jukumu la kudumu na jukumu la kwanza na la msingi kwa kila kiongozi na kila mwanachamawa CCM. Isitoshe, kwa hali ilivyo sasa, kuimarisha Chama cha Mapinduzi lazima iwe agenda kuu ya kila mmoja wetu. Ni ukweli ulio wazi kuwa ustawi na uhai wa Chama unategemea viongozi na wanachama kufanya kazi ya ziada kuimarisha Chama chao.
Ndugu Wajumbe;
Bahati nzuri, chini ya uongozi wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu Lt. Yusuf Rajab Makamba tarehe 19 Desemba, 2006 ulianzishwa Mradi wa Kuimarisha Chama. Mradi huo ndiyo uliokuwa dira na mwongozo wetu wa kufanya kazi za Chama tangu wakati huo mpaka leo. Wajibu wa kila kiongozi na kila mwanachama na kila kikao cha kila ngazi vimeainishwa vizuri. Pia, uliwekwa utaratibu mzuri wa kufuatilia utekelezaji wake. Bila ya shaka mtakumbuka kuwa utaratibu maalum uliwekwa wa kutoa tuzo kwa Mikoa iliyofanya vizuri katika utekelezaji wa vipengele mbalimbali vya uimarishaji wa Chama kwa mujibu wa Mradi huo.
Ndugu Wajumbe;
Kazi ya kuimarisha Chama chetu ni jukumu endelevu kwa kila mwanachama wa CCM, kila kiongozi wa CCM na kila mtumishi wa CCM. Kwa sababu hiyo, Mradi wa Kuimarisha Chama ni mchakato usiokuwa na ukomo. Ni kazi ya kudumu na wala siyo tukio lililoanzishwa na Katibu Mkuu Lt. Yusufu Rajabu Makamba na kukoma siku alipostaafu.
Tuongeze Wanachama
Kazi ya kuingiza wanachama wapya ni ya kudumu katika uhai wa Chama cha Mapinduzi. Hii siyo kazi ya msimu wa uchaguzi wa ndani ya Chama au wakati wa kura za maoni na hivyo kugeuzwa kuwa ni kwa ajili ya kuwapigia debe watu wanaotafuta vyeo. Lazima wakati wote tuwe tunaingiza wanachama wapya lakini pia lazima tuzingatie utaratibu ulioelekezwa na Katiba ya CCM. Hatuna budi kuhakikisha kuwa tuna wanachama walio waumini wa kweli na wapenzi wa dhati wa CCM, itikadi yake na sera zake na zile za Serikali zake.
Ndugu Wajumbe;
Wanachama ndiyo nguvu kuu ya uhai na ushindi wa CCM. Lazima Chama chetu kiwe na Jeshi kubwa la wanachama walio tayari kukijenga, kukisemea na kukipigania. Kuwa na Wanachama wengi ambao ni waumini wa kweli wa Chama chetu ina maana ya kuwa na kura nyingi za msingi za kuanzia katika uchaguzi wa dola. Pia wanachama ni nyenzo muhimu ya CCM kupata kuungwa mkono na wananchi hasa pale ambapo wanachama wataifanya ipasavyo kazi ya Chama ndani ya umma. Kila mwanachama akifanya kwa mafanikio kazi ya kushawishi wananchi kupigia kura wagombea wagombea wa CCM tutapata kura nyingi za uhakika.
Tuwe na Viongozi Wazuri
Ndugu Wajumbe;
Kazi ya kuhakikisha kuwa Chama cha Mapinduzi kina viongozi wazuri ni ya kudumu na wala siyo ya msimu wa kuchuja majina ya wagombea. Lazima Chama chetu kiwe na viongozi ambao ni waumini wa dhati wa itikadi yetu na wanaozijua vyema sera za Chama cha Mapinduzi na Serikali zake. Wao ndio wanaotarajiwa kuonesha njia kwa kuelimisha wanachama na wananchi. Viongozi wa CCM lazima wawe hodari wa kufafanua sera na masuala mbalimbali yahusuyo Chama chetu na Serikali zake. Hawataweza kufanya hivyo kama wao wenyewe ni maamuma. Kiongozi mzuri wa Chama cha Mapinduzi ni yule ambaye ni jasiri kukitetea Chama cha Mapinduzi na kama hapana budi yuko tayari kujitolea muhanga. Kuwa na kiongozi ambaye haguswi wala kusikitishwa na hali mbaya ndani ya Chama au hujuma dhidi ya Chama ni sawa na kutokuwa na kiongozi. Bora asiwepo. Na kuwa na kiongozi ambaye yeye mwenyewe anafanya vitendo viovu dhidi ya CCM na Serikali zake ni kuwa na nyoka ndani ya nyumba. Ni jambo hatari lisilokubalika na halistahili kuvumilika. Tukiwajua tuwaseme, tuwashughulikie, wachague wanapotaka kwenda.
Ndugu Wajumbe;
Kiongozi mzuri wa CCM lazima awe muaminifu na muadilifu na lazima wanachama na jamii imuone hivyo. Chama chetu kinashindania kushinda akili na mioyo ya Watanzania na hiyo ndiyo kazi tunayomtarajia kiongozi wetu afanye katika jamii. Hii ndiyo hasa kazi ya Chama ndani ya umma. Lakini, ili kiongozi wetu aweze kuifanya kwa mafanikio taswira yake mbele ya jamii ni kitu muhimu. Awe na taswira nzuri mbele ya wananchi. Kama jamii inamuona kuwa si mtu muadilifu itakuwa taabu sana kwake kufanikisha jukumu la msingi la Chama chetu. Hivyo ndugu zangu, lazima tuhakikishe kuwa viongozi wetu wanakuwa waadilifu ili wasigeuke kuwa balaa na hasara kwa Chama.
Ndugu Wajumbe;
Baada ya kukamilisha mchakato wa uchaguzi ngazi ya taifa, tutatengeneza na kutekeleza programu maalum ya kutoa mafunzo kwa viongozi wa Chama kuanzia ngazi ya Tawi hadi Taifa. Hali kadhalika, tutaendeleza na kukamilisha kazi ya ukarabati na upanuzi wa Chuo cha Ihemi ili kiwe kitovu cha kutoa mafunzo ya siasa kwa makada na viongozi wa Chama na Jumuiya zake kama ilivyokuwa inafanywa katika Chuo cha CCM cha Kivukoni na vyuo vyake vya kanda.
Ndugu Wajumbe;
Bahati nzuri vyama vya ukombozi vya nchi za Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika vimekubaliana kuwa Chuo cha Ihemi kiwe Chuo cha Mafunzo ya siasa kwa makada wa vyama vyao pia. Ni heshima kubwa kwa CCM, lakini pia inakipa Chama chetu wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa Chuo hicho kinawekwa katika viwango vya kimataifa. Tuko tayari na tutajipanga ipasavyo kutimiza wajibu wetu huo wa kihistoria.
Vikao Vifanyike Ipasavyo
Ndugu Wajumbe;
Ni kazi endelevu kwetu sote, wanachama na viongozi, kuhakikisha kuwa vikao vinafanyika kwa wakati na kwamba mikutano inaendeshwa vizuri na ina agenda zenye maslahi ya kujenga Chama na kuendesha nchi. Pia, ni muhimu kuhakikisha kuwa kinachoamuliwa kinatekelezwa ipasavyo. Naamini kwamba mafunzo tutakayotoa kwa viongozi na watendaji wa Chama kuhusu wajibu wao na jinsi ya kuutekeleza yatasaidia sana kuimarisha CCM.
Watendaji Mahiri
Ndugu Wajumbe;
Kwa Chama chetu kuwa na watendaji wazuri ni jambo lisilokuwa na mjadala. Lazima tuwe na watendaji ambao ni makada wazuri na watu mahiri kwa kazi zao. Wawe ni watu ambao wana uelewa mzuri wa sera za Chama na kwamba wanaweza kuzifafanua, kuzieneza na kuzitetea. Pia, wawe ni watu wanaojua vyema kazi yao ya utendaji, kwa mujibu wa shughuli zao wanazozifanya. Ni vyema kwa kazi za kitaalamu tukapata watu wataalamu wa kazi hizo. Ni muhimu sana tukayazingatia haya kwani utendaji mzuri katika Chama ni nguvu muhimu sana ya kukifanya Chama chetu kuwa imara. Chama chetu kiwe na mipango thabiti ya kuwaendeleza watumishi wake na kama hapana budi kuwadhamini wakasome. Tufanye hivyo.
Bila ya shaka mtakumbuka kuwa tarehe 3 Novemba, 2007, pale Kizota, niliahidi kuwa tutaboresha maslahi ya watumishi wa Chama. Tumetimiza ahadi hiyo. Leo nasema kuwa tutajitahidi kuendelea kuboresha maslahi ya watumishi wetu kadri uwezo utakavyoruhusu.
Tujitegemee
Ndugu Wajumbe;
Lazima Chama chetu kiwe na uwezo wake chenyewe wa kujisimamia na kujiendesha. Kiwe na fedha za kutosha na vitendea kazi. Hivi sasa hatuko hivyo. Hatuna budi kuongeza maarifa na juhudi za kukiwezesha Chama cha Mapinduzi kujitegemea kifedha bila ya kujali kama kuna ruzuku au hakuna. Jambo hili sasa liwe ni la kufa na kupona kwetu kuhakikisha linakuwa. Iwe agenda kuu ya Chama katika ngazi zote. Kila mmoja afikirie nini cha kufanya na kifanywe. Jambo la kuzingatia ni kufanya shughuli halali. Fursa zipo tuzitumie. Tusikubali kushindwa kwenye azma kwani hiyo itakuwa maangamizi wa CCM. Lazima tushinde.
Ndugu Wajumbe;
Mtakumbuka pia kwamba niliahidi kuimarisha usafiri ndani ya Chama. Ahadi hiyo tumeitimiza. Kila Mkoa na kila Wilaya imepata gari mpya tena gari nzuri na imara. Gari hizi tukizitunza vizuri zitatuwezesha katika uchaguzi ujao bila ya taabu. Kwa Mikoa na Wilaya mpya mipango ya kuwapatia magari iko mbioni. Kila Jumuiya tuliipatia magari yasiyopungua matatu.
Jumuiya za Chama
Ni wajibu wa kudumu wa Chama chetu kuhakikisha kuwa Jumuiya zake zinaimarika na kutimiza ipasavyo wajibu wake. Jumuiya ndiyo mkono mrefu wa Chama cha Mapinduzi kuufikia umma mpana wa Watanzania hasa wale ambao si wanachama. Jukumu letu ni kuhakikisha kuwa watu hao wanakuwa wanachama au wapenzi na marafiki wa CCM. Kwa hiyo, kuwepo kwa Jumuiya ni fursa nzuri kwa Chama cha Mapinduzi kuungwa mkono na watu wengi ili wakati wa uchaguzi tuweze kupigiwa kura na kupata ushindi. Jumuiya lazima zihakikishe kuwa zinatimiza ipasavyo wajibu wake ili wasiipotezee CCM fursa hii adhimu.
Ndugu Wajumbe;
Kwa muhtasari, hayo ndiyo baadhi ya mambo ya msingi ya mradi wa kuimarisha Chama. Mtakubaliana nami kuwa haya yote ndiyo kazi na wajibu wa kila mmoja kufanya. Ni kazi endelevu isiyokuwa na ukomo. Tupo kwa ajili hiyo na rai yangu kwenu ni kuhakikisha kuwa kila mwanachama na kila kiongozi anatimiza ipasavyo wajibu wake.
Mageuzi Ndani ya Chama
Ndugu Wajumbe;
Kwa dhamira ya kuendelea kukiimarisha zaidi, Chama cha Mapinduzi, katika mkutano wake wa tarehe 11-12 April, 2011, Halmashauri Kuu ya Taifa iliamua kuanzisha mchakato na kufanya mageuzi ndani ya Chama. Lengo kuu la uamuzi huo ni kukiwezesha Chama chetu kuwa na taswira inayovutia katika mitazamo na hisia za wanachama wake na wananchi.
Kimsingi NEC inataka tukiwezeshe Chama cha Mapinduzi kiendelee kupendwa na kuaminiwa na wananchi wote wa Tanzania. Tunataka wanawake na wanaume, wadogo na wakubwa, maskini na matajiri, wanyonge na wenye nguvu waone kuwa CCM ndiyo kimbilio lao.
Ndugu Wajumbe;
Kwa ajili hiyo mageuzi ya ndani ya Chama yamejengeka juu ya misingi ifuatayo:-
1. Kukiwezesha Chama cha Mapinduzi kuwa na makada na viongozi mahiri, waadilifu na waaminifu kwa Chama chao;
2. Kukiwezesha Chama kuwa na sera zinazojali maslahi ya wengi na kusukuma mbele kwa kasi maendeleo ya taifa letu;
3. Kukiwezesha Chama kuwa na muundo na mfumo wa uendeshaji ulio nyumbulifu na unaokifanya kuwa karibu na wanachama na wananchi;
4. Kukiwezesha Chama kujitegemea kimapato na kiuchumi ili kiweze kuendesha shughuli zake kwa uhakika, uhuru na heshima;
5. Kukiwezesha Chama kuwa na watu hodari wa kazi na Makada wazuri ambao wanalipwa vizuri na kuwezeshwa kutekeleza majukumu yao;
6. Kukiwezesha Chama kuwasiliana na umma kwa urahisi na kupambana na propaganda chafu za vyama vya siasa; na
7. Kukiwezesha Chama cha Mapinduzi kupambana na maovu ndani ya Chama na katika jamii likiwemo tatizo la rushwa na mengineyo.
Ndugu Wajumbe;
Katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa iliamuliwa kuwa kutokana na umuhimu wa hoja na haja ya kufanya mageuzi ndani ya Chama utekelezaji wa mageuzi uanze mara moja. Aidha, pawepo na progamu ya utekelezaji unayoainisha nini kinafanyika lini na mhusika ni nani! Bila ya shaka mtakumbuka kuwa katika kikao kile, tuliunda upya Kamati Kuu na kuteua Sekretarieti mpya. Vile vile iliamuliwa kuwa tufanye marekebisho katika muundo wa Chama na moja ya matokeo yake ni Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa kuchaguliwa kutoka wilayani. Nafasi za NEC za mikoa zikafutwa na zile za taifa zikapunguzwa. Aidha, limeundwa Baraza la Taifa la Ushauri ambalo wajumbe wake ni viongozi wakuu wa Chama wastaafu. Wanapata fursa ya kukaa na kutoa ushauri kwa Chama na viongozi wake.
Ndugu Wajumbe;
Tuliamua, pia, kuunganisha chaguzi za Chama na Jumuiya zifanyike mwaka mmoja. Shabaha ya uamuzi huo ni kutaka kujipa muda wa kutosha wa kujenga Chama na Jumuiya zake na kujiandaa kwa chaguzi za dola. Uamuzi huo umeokoa takriban mwaka mzima ambao tulikuwa tunautumia kwa uchaguzi. Vile vile Halmashauri Kuu ya Taifa iliamua kwamba mgao wa fedha unatokana na mapato Chama zinazopelekwa kwenye Matawi na Mashina uongezwe. Lengo ni kuziwezesha ngazi hizi muhimu za Chama kufanya kazi vizuri zaidi.
Ndugu Wajumbe;
Suala la nidhamu na maadili ya viongozi na wanachama lilisisitizwa sana kwa sababu ya umuhimu wake kwa taswira ya Chama chetu mbele ya jamii na wanachama wake. Pia, kutokana na ukweli kwamba ni kilio cha wanachama na wananchi cha kutaka tuiondowe taswira mbaya dhidi ya Chama iliyopo katika jamii kuwa ni Chama kisichokerwa na rushwa. Hicho ni kilio cha dhati kwa watu wenye nia njema na CCM: Chama chao, wanachokipenda na kukiamini. Chama ambacho bado hakina badala yake wa kuiongoza vyema nchi yetu na watu wake.
Halmashauri Kuu ya Taifa iliamua mambo mawili yafanyike. La kwanza, mfumo mzima wa kushughulikia masuala ya usalama na maadili katika Chama utazamwe upya na uimarishwe. Pili, Chama kichukue hatua na lazima kionekane kinachukua hatua dhidi ya viongozi na wanachama wasiokuwa waadilifu na waaminifu wanaofanya sura ya Chama ichafuke mbele ya jamii. NEC iliagiza wenyewe wajipime na kuamua na wasipofanya hivyo vikao husika katika Chama vichukue hatua.
Ndugu Wajumbe;
Hayo ni baadhi tu ya mambo muhimu yaliyoamuliwa yafanyike katika kufanya Mageuzi Ndani ya Chama. Utekelezaji wake umeanza. Yapo yaliyokamilika na yapo yanayoendelea kutekelezwa. Yapo mambo mengi ambayo ni endelevu kama vile mapambano dhidi ya rushwa. Hatuna budi kuendelea kulikemea na kusimama kidete kupambana na tatizo hili mpaka likomeshwe. Ni kwa maslahi na heshima ya Chama chetu kuendesha mapambano haya bila ya woga mpaka tushinde. Tukishindwa itakuwa hatari kwa uhai wa Chama chetu.
Umoja ni Ushindi
Ndugu Wajumbe;
Mara ya mwisho tulipokutana tarehe 11 Julai, 2010, tulikuwa tunajipanga kwenda kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Mliniteua mimi na Dkt. Mohamed Ghalib Billal kupeperusha bendera ya CCM kwa nafasi ya Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia tulipitisha Ilani ya Uchaguzi ya 2010-2015. Siku moja kabla ya Mkutano Mkuu, Halmashari Kuu ya Taifa ilikuwa imemteua Dkt. Ali Mohamed Shein kupeperusha bendera yetu kwa nafasi ya Rais wa Zanzibar.
Bahati nzuri tumepata ushindi kwa nafasi zote hizo za juu za uongozi wa taifa letu. Pia tulifanikiwa kupata Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wengi zaidi kuliko vyama vya upinzani. Kwa sababu hiyo, tumeunda Serikali zote mbili za nchi yetu na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi unaendelea vizuri.
Ndugu Wajumbe;
Kwa upande wa Zanzibar, tuna Serikali ya Umoja wa Kitaifa na mambo yanakwenda vizuri. Tuzidi kuunga mkono na kuwatakia heri Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Kwanza wa Rais, Mheshimiwa Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd. Tunawapongeza sana kwa mafanikio yaliyopatikana. Zanzibar ina amani na umoja unaozidi kuimarika. Tunatakiwa tuendelee kuiunga mkono Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili ifanikiwe zaidi.
Ndugu Wajumbe;
Uchaguzi uliopita kwa upande wa Tanzania Bara ulikuwa na changamoto nyingi ambazo hatukuzizoea wala kujiandaa nazo. Zinaelezea matokeo tuliyoyapata jambo ambalo linatulazimu kuwa makini zaidi katika uchaguzi ujao. Tusikubali kushtukizwa tena. Lakini, jambo moja lililo dhahiri ni kwamba umoja na mshikamano miongoni mwa wana-CCM ndiyo uliotuwezesha kukabili changamoto hizo na kupata ushindi tulioupata. Bila ya hivyo, mbinu hasi zilizotumika zingetufanya tushindwe.
Napenda ukweli huu uwepo katika vichwa na mioyo ya wana-CCM na sisi viongozi wao tuliochaguliwa hivi majuzi na watakaochaguliwa katika Mkutano huu. Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere alisema: Umoja ni Nguvu, ni kweli kabisa na sisi ni mashahidi. Nami napenda kuongeza kwa kusema kuwa Umoja ni Ushindi.
Ndugu Wajumbe;
Nawaomba wakati wote wa mkutano na baada ya mkutano tukumbuke na kuzingatia Umoja. Tuishikilie kamba ya Umoja isituponyoke. Tuimbe Umoja kimoyo moyo na tubainishe wazi wazi kwa kauli na matendo yetu kuwa: Umoja ni Nguvu Utengano ni Udhaifu! Umoja ni Ushindi! Umoja na Ushindi!. Napenda kuona kuwa tunatoka hapa tukiwa kitu kimoja, tukiwa watu tunaopendana na tulioshikamana. Nataka tuondoke katika Mkutano sote tukivuta kamba upande mmoja badala ya kuvutana. Nataka tuazimie kukabiliana na kauli, matendo au watu wanaopandikiza chuki na kuhatarisha umoja ndani ya Chama chetu na miongoni mwetu. Nataka kaulimbiu ya ujumbe wa Mkutano huu uwe Umoja ni Ushindi! Umoja na Ushindi! Tukiendelea kuwa watu tunaovutana na kuhasimiana hatutaweza kukijenga Chama chetu wala kuwatafutia ushindi wagombea wa Chama chetu. Tutakuwa sawa na ule msemo wa Kiswahili usemao: “vita vya panzi furaha ya kunguru” Tusijigeuze panzi na wala tusikifikishe Chama chetu kiwe hivyo.
Ndugu Wajumbe;
Mtakubaliana nami kuwa harakati za kutafuta uongozi ndani ya Chama au uteuzi wa kugombea katika chaguzi za dola imekuwa ndiyo chanzo kikuu kinacholeta mifarakano na kuvuruga umoja ndani ya Chama chetu. Hili ndugu zangu siyo sawa hata kidogo. Kugombea uongozi ni haki ya msingi ya mwanachama na raia wa Tanzania. Kwa nini mtu achukiwe au aonekane adui kwa kuamua kuitumia haki yake hiyo? Kwa nini afanyiwe vitimbi, vitendo viovu au njama za kuhujumiwa? Nani mwenye haki zaidi ya mwanachama ama raia mwenzake? Ni ubabe na jeuri ya pesa isiyokuwa na msingi. Ni ubinafsi na uchu wa madaraka uliopitiliza mipaka. Watu wa namna hiyo ni hatari sana kwani wanaweza hata kuua au kukivuruga Chama chetu kizuri kama tamaa zao zisipokidhiwa.
Ndugu Wajumbe;
Napenda kutumia nafasi hii kuwasihi wale wote wanaochukiana kwa sababu ya kugombea watakafakari upya misimamo yao. Wafanyayo siyo sahihi, wanaathiri nguvu na uhai wa Chama chetu. Naomba Kamati za Siasa za ngazi zote ziwatambue watu hao na kuwaita kuwapatanisha. Naomba wahusika watoe ushirikiano wao. Hata wale wanaohisi kuwa hawakutendewa haki katika uchaguzi, walidhulimiwa au hata kushindwa kwa sababu ya vitendo vya rushwa, wakumbuke kuwa Chama chetu kina utaratibu wa kushughulikia malalamiko yao. Wautumie utaratibu huo badala ya kufanya vitendo vinavyokigawa na kukivuruga Chama chetu. Kulalamika katika vyombo vya habari, kufanya ghasia au kuchochea migawanyiko hakutaleta ufumbuzi.
Ndugu Wajumbe;
Niruhusuni nitumie nafasi hii kuwasihi wale wote wenye tamaa ya kugombea uteuzi ndani ya Chama wasituulie Chama chetu. Kuwa na tamaa ya kugombea Urais, Ubunge na Udiwani si kosa ni haki ya mwanachama na ni haki ya raia wa nchi hii. Jambo ambalo halikubaliki na gumu kulivumilia ni kufanya vitendo vya kuwagawa wanachama na Chama chetu. Kuwalazimisha au kuwashinikiza kujiunga na kundi fulani siyo sawa. Kumchukia mtu kwa sababu naye anagombea au amekataa kukuunga mkono au kumuunga mkono umpendae ni jambo baya. Unaifanya demokrasia iwe haina maana au kichekesho. Na, lililo baya kupita kiasi ni kutumia fedha kushawishi, kuwarubuni au kuwanunua watu kukuunga mkono au kumuunga mkono mgombea wako au kujiunga na makundi. Hili ni jambo haramu na ni utovu wa maadili usiokubalika ambao lazima tuukatae, tuukemee na tuupige vita kwa nguvu zetu zote. Naomba wote tushirikiane katika mapambano haya kwa heshima ya Chama chetu.
Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi
Ndugu Wajumbe;
Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010 unakwenda vizuri kwa Serikali zetu zote mbili. Taarifa zitakazotolewa na Waziri Mku, Mheshimiwa Mizengo Pinda, kwa upande wa Serikali ya Muungano na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Balozi Seif Ali Idd kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, zitathibitisha ukweli huu. Niruhusuni nichukue muda wenu kidogo nizungumzie baadhi ya mambo yahusuyo shughuli za Serikali.
Nchi Iko Salama
Ndugu Wajumbe;
Napenda kuanza kwa kuwahakikishia kuwa Tanzania iko salama pamoja na kuwepo matukio ya hapa na pale. Mipaka yetu iko salama. Hakuna tishio lo lote la kiusalama la kutufanya tuhamanike. Hata mpaka wetu na Malawi uko salama pamoja na kuwepo kwa maneno maneno yahusuyo nchi zetu mbili kutofautiana wapi ulipo mpaka halali. Hakuna jambo lo lote linalofanywa upande wa wenzetu ambalo linatufanya tuwe na mashaka ya usalama wa nchi yetu kuwa hatarini. Kwa sababu hiyo hatujaiona haja ya kusogeza Majeshi yetu mpakani na anayesema tumefanya hivyo ni muongo. Apuuzwe na kushushuliwa.
Ndugu Wajumbe;
Tumeendelea na juhudi za kuimarisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa kuwajengea uwezo, zana na vifaa vya kisasa vya kivita. Lengo letu ni kukuza nguvu ya kimapigano ya Jeshi letu na kuimarisha utayari wake kivita. Hali kadhalika, tumeendelea kuboresha maslahi ya wanajeshi na mazingira yao ya kufanyia kazi na ya kuishi. Kwa upande wa usalama wa raia, yaani maisha na mali zao, matukio ya uhalifu yanaendelea kupungua. Hali hii inaashiria kuwa Jeshi la Polisi linafanya kazi nzuri. Kama tufanyavyo kwa JWTZ, tutaendeleza juhudi za kuimarisha Jeshi la Polisi kwa watu, zana na vifaa vya kisasa vya kufanyia kazi. Tutaendelea kuboresha maslahi na mazingira ya kufanyia kazi na ya kuishi ya Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama.
Ndugu Wajumbe;
Pamoja na kutokuwepo kwa tishio lililo dhahiri la shambulio la kigaidi, wakati wote vyombo vyetu vya ulinzi na usalama viko katika hali ya tahadhari kuepuka kushtukizwa. Kama mnavyokumbuka mwaka 1998 Ubalozi wa Marekani hapa nchini ulishambuliwa na ndugu zetu 11 walipoteza maisha. Hivyo basi, kuchukua tahadhari ni jambo la busara kufanya. Aidha, tuko katika hali ya tahadhari dhidi ya uharamia wa kuteka meli katika Bahari Kuu ya Hindi. Takriban mwaka mzima umepita bila ya matukio ya kutekwa nyara meli katika bahari yetu . Hata hivyo hatuachi kuchukua tahadhari.
Ndugu Wajumbe;
Matukio ya hivi karibuni ya vurugu zenye mwelekeo wa kidini yanasikitisha na kusononesha. Ni mambo ambayo hayafanani na sifa ya nchi yetu ya kuheshimiana na kuvumiliana pamoja na kuwepo tofauti zetu za dini, kabila rangi au maeneo tutokako. Vitendo hivyo havikubaliki na Serikali haitawavumilia au kuwaonea muhali wale wote wanaohusika na kuchochea vurugu hizo. Tumechukua hatua na tutaendelea kuchukua hatua bila ya ajizi. Ombi langu na wito wangu kwa viongozi na wafuasi wa dini nchini kuhubiri dini zao huku wakitambua na kuzingatia umuhimu wa kuheshimu imani za wengine na kuvumiliana. Tusipofanya hivyo nchi yetu tutaingiza kwenye matatizo yasiyostahili kuwepo.
Ndugu Wajumbe;
Inatia moyo kuona kuwa watu wenye nia njema na nchi yao ni wengi. Kwa sababu hiyo pamoja na jitihada za baadhi ya watu wasiyoitakia mema nchi yetu hawajafanikiwa kuwagawa na kuwafarakanisha Watanzania. Nawaomba Watanzania wenzangu tuwe na moyo huo huo na sisi katika Serikali tutaendelea kumchukulia hatua mtu ye yote anayetaka kutuvurugia amani na utulivu wa nchi yetu na watu wake.
Ndugu Wajumbe;
Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali haitamuonea mtu ye yote asiyehusika. Tutaendelea kuidumisha sifa yetu ya kuendeleza utawala bora, kuheshimu haki za binadamu na kuzingatia utawala wa sheria. Kadhalika tutaendelea kuheshimu mgawano wa madaraka miongoni mwa mihimili mikuu ya dola. Nafurahi kwamba mpaka sasa mambo yanakwenda vizuri.
Muungano Imara
Ndugu Wajumbe;
Muungano wetu ni imara pamoja na kuwepo vitendo vyenye lengo la kuudhoofisha vinavyofanywa na baadhi ya viongozi wa siasa na wa dini hasa kule Zanzibar. Jambo linalosikitisha ni watu hao kutumia njia za vitisho na ghasia ili kuwalazimisha watu kuwaunga mkono. Njia hizo hazikubaliki na wala hazitavumiliwa.
Inastaajabisha mambo hayo kufanyika hivi sasa wakati kuna Tume ya Katiba. Kama mtu ana maoni yo yote kuhusu Muungano ayafikishe tu, yatapokelewa na kupimwa. Vile vile Kamati ya Pamoja ya Serikali zote mbili inayowakutanisha Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar chini ya Uenyekiti wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano imekuwa inafanya kazi nzuri kutatua kero za Muungano. Kama mtu analo jambo analotaka lipatiwe jawabu awasilishe kwa wahusika litashughulikiwa.
Hali ya Uchumi
Ndugu Wajumbe;
Katika Mkutano Mkuu Maalum wa Julai, 2010 hapa Kizota, nilielezea mafanikio tuliyoyapata na changamoto tulizokumbana nazo katika kukuza uchumi wa nchi yetu na kupunguza umasikini. Nilieleza pia nia yetu ya kuendelea kupambana na changamoto zilizokuwa mbele yetu pamoja na ugumu unaotokana na hali ya kuyumba kwa uchumi wa dunia ambamo na sisi pia tumo. Kwa ajili hiyo mwaka 2011 tulizindua Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano(2011/12 – 2015/16).
Mpango huu ni wa kwanza kati ya mitatu katika safari yetu ya kutekeleza Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025. Kwa mujibu wa Dira yetu hiyo, tunatarajia ifikapo mwaka 2025 nchi yetu itaondoka katika kundi la nchi maskini sana duniani na kuwa nchi ya uchumi wa kati. Yaani tunataka pato la wastani la Watanzania litoke kwenye dola za Kimarekani 545 za sasa hadi kufikia dola za Kimarekani 3,000. Lengo hilo ni kubwa linalohitaji mipango thabiti na uwekezaji makini wa Serikali na sekta binafsi. Pia inahitaji kuwepo kwa nidhamu ya dhati ya viongozi na wananchi wa Tanzania.
Ndugu Wajumbe;
Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo umekwishaanza. Lengo la jumla katika Mpango wa kwanza ni Kufungulia fursa kwa ukuaji wa uchumi; wa pili ni Ujenzi wa mazingira ya maendeleo ya viwanda; na wa tatu ni Kuimarisha ubunifu na ushindani kimataifa. Tayari miradi ya kimkakati imekwishaainishwa na inapewa kipaumbele katika bajeti ya Serikali na ubia baina ya sekta binafsi na sekta ya umma. Katika kila hatua suala la kukuza ajira limepewa umuhimu mkubwa kwani lengo letu ni kuwa na ukuaji wa uchumi unaojumuisha maisha ya watu. Vijana ni walengwa wakubwa.
Mwelekeo wa uchumi wetu ni mzuri. Kasi ya ukuaji wa uchumi iliyokuwa asilimia 6.4 mwaka wa jana inatarajiwa kufikia asilimia 7 mwaka huu. Mauzo yetu ya nje yanazidi kukua na kuongezeka. Kwa mfano mwaka 2005 ilikuwa dola za Kimarekani milioni 2,945.5 na sasa ni milioni 7,461.2. Akiba yetu ya fedha ya kigeni nayo ni nzuri. Hivi sasa ni dola za Kimarekani bilioni 4.1 inatuwezesha kuagiza bidhaa kutoka nje kwa miezi 3.8.
Ndugu Wajumbe;
Changamoto kubwa katika uchumi ni mfumuko wa bei. Ni kweli umepungua kutoka asilimia 19.8 Desemba, 2011 hadi asilimia 13.5 Septemba, 2012, hata hivyo kupungua huko ni kidogo mno. Tunaendelea kuchukua hatua za kudhibiti na kupunguza zaidi mfumuko wa bei. Kwa vile moja ya sababu ni kupanda kwa bei za mafuta. Tumeipa dhamana EWURA kusimamia kwa karibu uagizaji na upangaji wa bei ya mafuta.
Kwa kuwa bei za vyakula hasa mchele na sukari navyo huchangia kupanda kwa mfumuko wa bei na kuongeza gharama ya maisha mamlaka husika zimeagizwa kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wanawezeshwa kuagiza bidhaa hizo kwa wingi kutoka kwa nje kwa kuwapatia nafuu ya baadhi ya kodi. Pamoja na hayo jawabu la kudumu lipo katika kuendeleza mageuzi ya kilimo ili nchi yetu ijitosheleze kwa chakula na kupata ziada kubwa ya kuuza nje. Hayo ndiyo malengo na hatua zinazochukuliwa katika ASDP, Kilimo Kwanza na SAGCOT. Ndiyo maana tutaendelea kutoa ruzuku ya pembejeo kwa wakulima, kuimarisha masoko na miundombinu vijijini.
Mapato na Matumizi ya Serikali
Ndugu Wajumbe,
Tunazidi kupata mafanikio ya kutia moyo kwa upande wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Makusanyo ya mapato ya kodi Mwezi Agosti 2012, kwa mfano, yalifikia shilingi bilioni 554.8 ikilinganishwa na makusanyo ya shilingi bilioni 147 mwezi Desemba 2005. Mafanikio haya yametokana na juhudi za dhati za Serikali katika kusimamia mabadiliko ya sera na kuimarisha mifumo na taasisi za ukusanyaji wa mapato ya kodi na mengineyo.
Kwa sababu ya kuongezeka huko kwa mapato, bajeti ya Serikali nayo imeongezeka kutoka shilingi trilioni 4.13 mwaka 2005/06 hadi shilingi trilioni 15.12 mwaka huu. Jambo linaloleta faraja ni kuwa mchango wa Serikali kutokana na bajeti hiyo nao umeongezeka kutoka shilingi trilioni 2.1 mwaka 2005 hadi trilioni 8.8 mwaka huu. Utegemezi wa wahisani nao unaendelea kupungua kutoka asilimia 44 mwaka 2005/6 hadi 21.
Ndugu Wajumbe;
Sambamba na kuongeza mapato, nidhamu, udhibiti wa matumizi ya fedha na mali za umma vinazidi kuimarika. Hii ni kutokana na kuimarika kwa mifumo na kada ya uhasibu katika Serikali Kuu na Serikali za Mitaa. Pia ni matokeo ya kazi nzuri inayoendelea kufanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma. Hati Chafu katika idara za Serikali zinaendelea kupungua katika taarifa ya ukaguzi kila mwaka. Hivi sasa tunaelekeza nguvu zetu katika kuhakiki thamani ya fedha zilizotumika na kazi iliyofanyika au huduma iliyotolewa.
Uwekezaji
Ndugu Wajumbe,
Serikali imechukua hatua kadhaa kuboresha mazingira ya uwekezaji na ya kufanya biashara hapa nchini. Lengo letu ni kuvutia wawekezaji wa ndani na nje kuongeza vitega uchumi nchini na kupanua biashara ndani ya nchi na kati ya nchi yetu na nchi nyingine duniani. Tunafanya hayo kwa kutambua ukweli kwamba uchumi unakua na kuongezeka pale ambapo uwekezaji unaongezeka. Takwimu zinaonyesha kwamba uwekezaji umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka katika sekta ya utalii, viwanda, kilimo, madini, fedha, ujenzi na sasa kwenye utafutaji wa gesi na mafuta. Tumepata mafanikio makubwa katika utafutaji wa gesi na nchi yetu itakuwa moja ya mzalishaji mkubwa wa gesi. Mwaka 2011, kwa mfano, kulikuwa na jumla ya miradi 826 yenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 7,177 itakayozalisha ajira ya watu 79,000. Haya ni mafanikio madogo lakini tunaweza kufanya vizuri zaidi.
Tutaendelea kutumia fursa ya kijiografia ya nchi yetu kuvutia uwekezaji na kuifanya Tanzania kuwa lango kuu la biashara na usafirishaji kwa nchi za Afrika ya Mashariki na Kati. Ili kufanikisha hayo, tutaendelea kuboresha miundombinu ya barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege na teknohama.
Miundombinu
Ndugu wajumbe;
Moja ya vipaumbele vya juu vya Serikali ya CCM ninayoiongoza ni kuboresha miundombinu ya usafiri wa ardhini, majini na angani nchini. Tumethibitisha hayo kwa mgao wa fedha za bajeti ya Serikali ambapo miundombinu ni ya pili baada ya elimu. Mwaka huu ni shilingi trilioni 2.4, ambayo ni asilimia 16 ya bajeti ya Serikali ukilinganisha na elimu yenye trilioni 3.6 ambayo ni sawa na asilimia 24, na afya yenye shilingi trilioni 1.5 sawa na asilimia 10 ya bajeti ya Serikali. Tunafanya hivyo kwa kutambua mchango muhimu wa sekta ya usafiri kwa maendeleo ya nchi yetu na watu wake. Usafiri unapokuwa bora na wa uhakika, gharama za usafirishaji zinapungua, shughuli za uzalishaji viwandani na kilimo zinaimarika. Ni kichocheo kikubwa cha kuibuka kwa fursa mbalimbali za uchumi na kuongeza kasi ya maendeleo na kukuza kipato cha Watanzania waliopo mijini na vijijini.
Ndugu Wajumbe;
Tunafanya uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa barabara kuliko wakati mwingine wo wote katika historia ya nchi yetu. Hivi sasa barabara zenye urefu wa kilometa 11,154 zinajengwa kwa kiwango cha lami katika sehemu mbalimbali nchini. Tulijipa lengo la kuunganisha mikoa yote kwa barabara za lami na barabara zote kuu ziwe za lami.
Nafurahi kusema kuwa utekelezaji wake unakwenda vizuri. Tumeanza kufanikiwa kuifikia ile mikoa ambayo kwa muda mrefu ilikuwa haifikiki kwa urahisi kwa kukosa barabara za lami. Katika hotuba yangu ya tarehe 25 Juni, 2006 niliwaambia Wajumbe wa Mikoa ya Ruvuma, Rukwa, Mtwara, Kigoma na Tabora kuwa kilio chao tumekisikia. Niliahidi kuwa ujenzi wa barabara katika Mikoa hiyo tutaipa kipaumbele. Tumetimiza ahadi hiyo na kazi inaendelea kwa kasi na hata wenyewe ni mashahidi. Karibu tunafikia ndoto yetu ya kwamba hakuna mkoa utakaoachwa nyuma.
Ndugu Wajumbe;
Inafurahisha zaidi kuona kuwa zaidi ya asilimia 60 ya gharama za ujenzi wa barabara tunazojenga nchini ni fedha zetu wenyewe. Aidha, uwezo wa Mfuko wa Barabara (Road Fund) nao umeongezeka sana kutoka shilingi bilioni 58 mwaka 2005 hadi shillingi bilioni 430. Hali hiyo imeongeza uwezo wetu wa kujenga na kukarabati barabara mbalimbali nchini. Kwa ajili hiyo tumeongeza bajeti ya barabara kwenye Halmashauri zote nchini.
Ndugu Wajumbe;
Pamoja na barabara, tunaendelea kuimarisha viwanja vya ndege, bandari na usafiri wa reli. Changamoto mbalimbali zinajitokeza katika utekelezaji wa lengo letu na kubwa zaidi ikiwa ni ile ya gharama za ujenzi na ukarabati wa miundombinu kuwa kubwa mno ikilinganishwa na uwezo wetu. Tunaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuzikabili changamoto hizo hatua kwa hatua na tunazipunguza.
Elimu
Ndugu wajumbe;
Tumefanikiwa kupanua sana fursa za kuwapatia elimu vijana wetu katika ngazi zote. Kuna watoto wengi katika elimu ya awali, na kwa elimu ya msingi asilimia 97 ya watoto wenye umri wa kwenda shule wamejiandikisha. Kwa kiwango hicho, tuko mahali pazuri kufikia asilimia 100 ifikapo mwaka 2015 kama ilvyoagiwa katika Malengo ya Milenia ya Umoja wa Mataifa. Kuhusu elimu ya Sekondari, wananchi na wadau wengine wameitikia wito wa Serikali wa kila Kata kuwa na shule ya sekondari. Kwa sababu hiyo idadi ya shule 3,165 zimejengwa kati ya 2005 na hivi sasa na idadi ya wanafunzi katika shule za sekondari imeongezeka kutoka 524,325 mwaka 2005 hadi 1,884,272 mwaka huu.
Tumepanua sana mafunzo ya ufundi na elimu ya juu. Hivi sasa nchi yetu ina vyuo vikuu 27 na wanafunzi waliopo vyuoni humo ni zaidi ya 166,484 ikilinganishwa na 40,719 wa mwaka 2005. Ili kutoa fursa sawa kwa wanafunzi wote tumeongeza sana uwezo wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ili iwape wanafunzi wengi mikopo ya elimu. Bajeti ya Bodi hiyo imeongezeka kutoka shilingi bilioni 56.1 mwaka 2005 hadi shilingi bilioni 306.0 mwaka huu. Wanafunzi wanaopata mikopo wapo 93,176 ukilinganisha na 16,345 mwaka 2005. Tutaendelea kuongeza fedha ili tuwafikie wanafunzi wengi kadri inavyowezekana.
Ndugu Wajumbe;
Upanuzi mkubwa wa elimu katika ngazi zote nchini umezua changamoto mbalimbali kuhusu ubora wa elimu. Tunazitambua changamoto hizo kuwa ni pamoja na zile za upungufu wa walimu, hususan wa sayansi; upungufu wa vifaa vya maabara, vitabu na nyumba za walimu hasa kwenye maeneo ya vijijini. Tumejipanga vyema kuzitafutia ufumbuzi na tumeanza kufanya hivyo. Tumeongeza vyuo vinavyotoa mafunzo ya ualimu ili kuongeza idadi ya waalimu. Bajeti ya elimu ni kubwa kuliko zote ili kusaidia kutatua tatizo la upungufu wa vitabu, maabara, vifaa vya kufundishia na nyumba za walimu na mahitaji mengineyo. Hivi karibuni nilipokuwa Mkoani Singida nimewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote nchini kuhakikisha kuwa shule zote za sekondari katika maeneo yao zinakuwa na maabara ya sayansi katika miaka miwili ijayo.
Afya
Ndugu wajumbe;
Suala la afya ya Watanzania tunalipa umuhimu mkubwa sana. Tumeongeza bajeti ya afya kutoka shilingi bilioni 271 mwaka 2005 hadi shilingi trilioni 1.5 mwaka huu. Nyongeza hii ndiyo iliyotuwezesha kutekeleza Sera mpya ya Afya (2007) na Mpango wa Miaka Kumi wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) wa kuitekeleza vyema Sera hiyo. Lengo kuu la sera na MMAM ni kuwapatia Watanzania huduma ya afya iliyo bora katika umbali usiozidi kilometa tano. Vile vile, ni kuimarisha huduma zinazotolewa katika hospitali za Wilaya, Mikoa, Kanda na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Katika mpango huu pia tumeazimia kukabili tatizo la upungufu wa madaktari, wauguzi na wataalamu wengi. Tunaendelea kupanua mafunzo ya wataalamu hao katika vyuo vyetu hapa nchini na hata nje ya nchi. Tumejenga na tutaendelea kujenga vyuo vipya, wakati huo huo tukipanua vilivyopo. Tumeendelea kujenga uwezo wa kupambana na maradhi makubwa yanayoua watu wengi. Tumeelekeza nguvu zetu kwenye maradhi yanayoambukiza kama vile malaria, UKIMWI na kifua kikuu na yale yasiyoambukiza kama vile saratani, moyo, shinikizo la damu na vifo vya kina mama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano.
Ndugu Wajumbe;
Kwa maradhi yote mafanikio ya dhahiri yanaendelea kupatikana. Maambukizi ya virusi vya UKIMWI yanapungua kutoka asilimia 8 hadi asilimia 5.7, vifo kutokana na malaria vimepungua kwa asilimia 40 kwa Tanzania Bara na kwa Zanzibar tunakaribia kutangaza kufutika kwa maradhi hayo. Tumepanua uwezo wa kutibu maradhi ya moyo ikiwa ni pamoja na kufanya upasuaji wa moyo. Tumepanua uwezo wa kuchunguza na kutibu maradhi ya kansa. Tunaendelea kujenga uwezo wa ndani kwa maradhi tunayopeleka wagonjwa wengi nje na mafanikio yanaaza kuonekana. Safari ni hatua, naamini tutafika kwani mwelekeo wetu ni mzuri.
Umeme na Maji
Ndugu wajumbe;
Tunaendelea kupanua uwezo wetu wa kuzalisha na kusambaza umeme nchini. Tumeanza safari ya uhakika ya kupunguza kutegemea mno umeme wa nguvu ya maji. Tunapanua umeme utokanao na vyanzo vingine hasa gesi asilia na makaa ya mawe. Mipango ya kutumia upepo na mionzi ya jua nayo iko mbioni. Pamoja na hayo tunayo mikakati ya kupunguza umeme unaozalishwa kwa kutumia mafuta kwa kubadili mitambo hiyo iweze kutumia gesi asilia.
Hivi majuzi tu nilizindua ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam. Litakapokamilika nchi yetu itakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 3,000 na kuung’oa mzizi wa fitina wa mgao na upungufu wa umeme nchini. Tumeendelea kuwekeza katika usambazaji wa umeme nchini jambo ambalo limetuwezesha kuwapatia umeme kwa asilimia 18.4 Watanzania kutoka asilimia 10 mwaka 2005. Kwa kasi hii naamini tutafikia lengo la asilimia 30 ifikapo 2015.
Kwa upande wa maji, jitihada za kuwapatia wananchi maji safi na salama zinaendelea vizuri. Eneo hili lina changamoto kuu mbili. Kwanza ni ule ukweli kwamba kuna baadhi ya maeneo ya nchi yetu hayana vyanzo vya maji karibu au hayapati mvua za kutosha au yana ukame. Katika maeneo ya aina hii upatikanaji wa maji huwa wa shida sana na hivyo kutulazimisha kujenga miradi ya maji ya bomba kutoka masafa marefu. Changamoto yetu ya pili ni ule uwezo mdogo wa kifedha kwa miradi mingi inayohitaji pesa nyingi. Mwaka 2006 tulianzisha Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji. Kufuatia utekelezaji ulio makini wa programu ya sekta ya maji, asilimia 60 ya watu wa vijijini na asilimia 86 ya watu wa mijini wanaopata maji safi na salama. Ni matumaini yangu kuwa tutafikia lengo letu la asilimia 65 la upatikanaji maji kwa vijijini na asilimia 90 kwa mijini ifikapo 2015. Bahati nzuri tunayo miradi ya maji inayoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini na itapokamilika tutafikia lengo letu au hata kulivuka.
Pongezi kwa Kuchaguliwa
Ndugu Wajumbe;
Katika Mkutano huu, Ndugu Amani Abeid Karume, Makamu Mwenyekiti wa Zanzibar na Ndugu Pius Msekwa, Makamu wa Mwenyekiti wa CCM kwa upande wa Tanzania Bara watastaafu. Ndiyo maana NEC imeamua kuwapendekeza kwenu Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Ndugu Philip Mangula kuchukua nafasi zao. Napenda kuchukua nafasi hii kwashukuru kwa dhati Rais Amani Abeid Karume na Mzee Msekwa kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya kunisaidia kuongoza Chama chetu. Wamekifanyia Chama chetu mambo mengi mazuri ambayo hatuna budi kuwapongeza na kuwashukuru. Waliendelea kuwa walimu wangu na washauri wangu kwa mambo mengi ya Chama na nchi. Nawashukuru sana. Sote tuwatakie afya njema na maisha marefu. Na tumuombe Mzee Msekwa asichoke kuandika vitabu ili hazina yake kubwa ya uzoefu na maarifa iwanufaishe wengi kwa miaka mingi ijayo.
Kwa viongozi wa Mikoa, Wilaya na Jumuiya pamoja na Wajumbe, nirudie kuwapongeza nyote kwa kuchaguliwa kwenu. Poleni kwa magumu ya uchaguzi mliyokumbana nayo. Sasa uchaguzi umeisha, fanyeni kazi ya kujenga Chama. Tibuni majeraha ya uchaguzi na hasa fanyeni kila muwezalo kuziba nyufa za uchaguzi na migawanyiko miongoni mwa wanachama na viongozi. Kumbukeni wosia wa Baba wa Taifa “Umoja ni Nguvu” Kumbukeni kaulimbiu ya Mkutano wetu huu ya Umoja ni Ushindi! Umoja na Ushindi! Kajengeni umoja katika maeneo yenu ya uongozi kwa maslahi ya Chama chetu na nchi yetu.
Hitimisho
Ndugu Wana-CCM;
Kwa kuhitimisha naomba nirudie kusema kuwa tumepata mafanikio ya kutia moyo katika ujenzi wa Chama na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 – 2015. Bado kazi kubwa iko mbele yetu kwa mambo yote hayo mawili. Tunaitambua na tunayo mipango thabiti ya kutekeleza majukumu yetu. Nina imani tutafanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kufikia malengo yetu. Tukiendelea kushirikiana tutafika. Umoja ni Ushindi! Umoja na Ushindi!
Baada ya hotuba yangu naomba sasa nitamke kuwa Mkutano Mkuu wa Nane wa CCM umefunguliwa rasmi.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Kidumu Chama cha Mapinduzi
Asanteni sana kwa Kunisikiliza