Kikwete Amtumia Salamu za Rambirambi Sheikh Twakali Karago

Jakaya Mrisho Kikwete

Na Mwandishi Wetu

MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Mrisho Kikwete ametumia salamu za rambirambi Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Kigoma, Ndugu Amani Kabourou, kuomboleza kifo cha aliyekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Mkoa huo, Sheikh Twakali Ali Karago ambaye aliaga dunia usiku wa kuamkia Novemba 9, 2012.

Katika salamu zake, Rais Kikwete amesema: “Nimefadhaishwa na kusikitishwa na taarifa za kifo cha Mzee Twakali Ali Karago ambacho nimejulishwa kimetokea usiku wa kuamkia Novemba 9, 2012.” Ameongeza Rais Kikwete: “Mzee Karago alikuwa kiongozi makini na mtumishi hodari wa wananchi. Ametuacha lakini ametuachia urithi wa kutukuka kabisa wa utumishi wenye uadilifu na wenye kujali watu na maslahi yao. Alionyesha uongozi imara wakati wote wa maisha yake na tutaendelea kumuenzi kwa mchango wake katika maendeleo ya nchi yetu.”

“Nakutumia wewe Ndugu Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa, Ndugu Amani Kabourou, salamu zangu za rambirambi kufuatia kifo cha mzee wetu huyu. Kupitia kwako nawatumia pole zangu nyingi viongozi na wanachama wote wa CCM mkoani Kigoma kwa kuondokewa na kiongozi na mwanachama mwenzao,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Aidha, nakuomba kupitia kwako unifikishie salamu zangu za pole nyingi kwa wanafamilia wa Mzee Karago kwa kupotelewa na mhilimi wa familia.”