MKURUGENZI wa Shirika la Upelelezi la Marekani CIA, David Patreaus amejiuzulu kutokana na kuwa na mahusiano ya nje ya ndoa ambayo yamezua hali isiyofaa kwake kuendelea na kazi hiyo. Petreus, ambaye alichukua wadhifa huo miezi 14 iliyopita baada ya kustaafu katika jeshi la Marekani akiwa Jenerali mwenye nyota nne amefafanua kuhusu uamuzi wake huo katika barua yaliyoiandika kwa maafisa wa shirika hilo Novemba 09, 2012.
Katika barua hiyo Petraeus ameandika kuwa; “baada ya kuishi katika maisha ya ndoa kwa miaka 37, nimeonesha udhaifu kwa kujihusisha na mahusiano mengine nje ya ndoa hiyo. Tabia hiyo haikubaliki kote, kama mume na pia kama kiongozi wa taasisi kama hii yetu. Tayari Rais Obama amekubali ombi langu la kujiuzulu.”
Hata hivyo hakukuwa na taarifa rasmi juu ya lini mahusiano hayo yalifanyika na nani alihusika. Mwandishi wa mtandao wa Slate.com Fred Kaplan, ambaye amewahi kuandika kuhusu Patraeus na ushawishi alionao katika mipango ya Jeshi la Marekani amekiambia kituo cha televisheni cha CNN kuwa kiongozi huyo alikuwa na mahusiano na mwandishi Paula Broadwell.
Broadwell alitumia mwaka mmoja kumfuata Petraeus nchini Afghanistan kabla ya kuandika wasifu wake 2012 uliopewa jina la “All in: The education of General Petraeus.” Picha yake katika mtandao wa Amazon.com inamuonesha akiwa amekaa karibu na mahali alipokaa Patreaus huku ujumbe wake wa mwisho katika mtandao wa Twitter siku ya Jumatatu unahusu uongozi wa falsafa ya Maxim wa Jenerali huyo.
Amesema kuwa sababu za kujiuzulu kwake ni za binafsi zaidi na hazihusiki na uchunguzi unaoendelea kuhusu uvamizi wa ubalozi mdogo wa Marekani mjini Benghazi, Libya, ambako Balozi wa Marekani na maafisa wengine waliuawa. CNN inaripoti kuwa Shirika la Ujasusi la Marekani, FBI, linachunguza iwapo uamuzi huo ulitokana na hatari za kiusalama ikiwa ni pamoja na kujua kama Petraeus inawezekana kuwa alitishwa kutokana na mahusiano yake hayo.
Mahusiano ya nje ya ndoa ni suala nyeti katika tasnia ya usalama. Mahusiano hayo yanaweza kuwa kitisho kwa taaluma hasa kwa maafisa wanaoshikilia nafasi za juu kwenye majeshi na taasisi za usalama.
Aliyekuwa Mkuu wa CIA Jenerali David Petraeus Aliyekuwa Mkuu wa CIA Jenerali David Petraeus
Mbinu za jenerali huyo aliyepata sifa tele zimesaidia kuharakisha kuondolewa kwa jeshi la Marekani nchini Iraq. Alikuwa kamanda wa vita vya Afghanistan kabla ya kushika wadhifa huo wa mkuu wa CIA.
Petraeus mwenye umri wa miaka 60 alistaafu jeshi akiwa Jenerali mwenye nyota tano na muda mfupi baadae alipewa wadhifa huo wa kuiongoza CIA. Ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha kijeshi cha Marekani katika eneo la West Point mjini New York pamoja na Chuo Kikuu cha Princeton.
-BBC