KAMATI ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imefanya mabadiliko madogo ya ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom ili kupitisha mechi ya kirafiki ya kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kati ya Taifa Stars na Kenya (Harambe Stars) itakayochezwa Novemba 14 mwaka huu jijini Mwanza.
Mechi tano za ligi hiyo zilizokuwa zichezwe Novemba 11 mwaka huu, zimerejeshwa nyuma kwa siku moja ambapo sasa zitafanyika Novemba 10 mwaka huu. Mechi hizo ni Simba vs Toto Africans (Uwanja wa Taifa), Kagera Sugar vs Polisi Morogoro (Uwanja wa Kaitaba) na Oljoro JKT vs Ruvu Shooting (Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid).
Nyingine ni Tanzania Prisons vs JKT Ruvu (Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine) na African Lyon vs Mtibwa Sugar (Azam Complex). Mechi ya Mgambo Shooting vs Azam (Azam Complex) yenyewe itachezwa Novemba 10 mwaka huu kama ilivyokuwa imepangwa.
Nayo mechi ya Coastal Union vs Yanga (Uwanja wa Mkwakwani) itabaki Novemba 11 mwaka huu kwa vile Novemba 10 mwaka huu uwanja huo utakuwa na mechi nyingine. TFF imepanga utaratibu wa kuwapata kwa wakati wachezaji wa Yanga walioitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars.
Mabadiliko mengine ni ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ambapo mechi ya Villa Squad vs Transit Camp iliyokuwa ichezwe Novemba 8 mwaka huu sasa inachezwa Novemba 9 mwaka huu, na ile ya Novemba 7 mwaka huu kati ya Burkina Faso na Small Kids inachezwa Novemba 9 mwaka huu. Viwanja ni vilevile.
Kamati ya Ligi imelazimika kufanya mabadiliko hayo kutokana na viwanja husika kuwa na mechi nyingine, na vilevile Small Kids kupata matatizo ya usafiri kutoka mkoani Rukwa kwenda Morogoro.