Na Mandishi Wetu, Dodoma
WABUNGE wameanza kuijadili hoja binafsi ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto aliyewasilisha leo akilitaka Bunge liunde Kamati ya Uchunguzi kuchunguza na baadaye kuweka hadharani majina ya Watanzania walioficha mabilioni ya fedha haramu nje ya nchi yaani nchini Uswiss. Lengo kubwa la Hoja binafsi hiyo ni kuitaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwasiliana na Taasisi ya Benki ya Dunia kupitia kitengo cha ‘Assets Recovery’ kurejesha fedha haramu zilizofichwa na Raia wa Tanzania katika mabenki huko nchini Switzerland.
Baada ya Zitto kuwasilisha hoja hiyo bungeni, Wabunge wameanza kuchangia hoja huku wengine wakipinga bunge kuridhia kwa kile kuhoji kupata ushaidi zaidi juu ya hoja hiyo. Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mwibara, Kange Lugola, yeye amekuja juu zaidi akitaka bunge lilidhie hoja hiyo ili iundwe kamati ya uchunguzi kuchunguza jambo hilo.
Akichangia mbunge huyo alisema kitendo cha baadhi ya watu ambao wamekuwa wakificha fedha haramu nje ya nchi kinalinyima mapato taifa na kuendeleza rushwa kwenye uchaguzi jambo ambalo ni hatari. Alisema ipo haja ya wabunge wote kuugana na kuweka itikadi zao pembeni na kuunga mkono hoja hiyo ili kuundwa kwa kamati ya uchunguzi.
Aliongeza kuwa hatua hiyo itaokoa fedha nyingi za umma ambazo baadhi ya mafisadi wanazificha nje huku huduma za kijamii za elimu, afya, maji na shughuli nyingine za maendeleo zikiendelea kudorora. Hata hivyo aliomba Waziri Membe ajitokeze na kusaidia kuwataja kwa majina viongozi wenye mabilioni nje ya nchi, kwani alishawahi kusema bungeni kuwa anawajua baadhi ya watu.