Hali ya Sheikh Soroga Aliyemwagiwa Tindikali Bado ni Mbaya, MOI Kuchunguza Tindikali

Sheikh Fadhil Suleiman Soroga aliyemwagiwa tindikali akiwa hospitalini akipatiwa huduma ya kwanza Zanzibar

TAASISI ya Mifupa (MOI) katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam imeanza uchunguzi wa kubaini kemikali aliyomwagiwa Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Suleiman Soroga.

Tukio hilo lilitokea saa 12 asubuhi ya Novemba 6 mwaka huu, wakati katibu huyo akifanya mazoezi baada ya swala ya Alfajiri.Juzi Rais Jakaya Kikwete alikwenda kumjulia hali Sheikh Soroga akifuatiwa na Makamu wa Rais, Dk Gharib Bilal aliyefanya hivyo jana.

Kabla ya kufikishwa katika taasisi hiyo, kiongozi huyo wa kidini, alipatiwa huduma ya kwanza katika Hospitali ya Mnazi Mmoja huko Zanzibar. Akizungumza na waandishi wa habari jana, Ofisa Habari wa MOI, Jumaa Almasi alisema hali ya Sheikh Soraga haijawa ya kuridhisha na kwamba kwa sasa amepumzishwa katika chumba maalumu kwa ajili ya uchunguzi wa kina.

“Hali yake bado haijakuwa sawa na mpaka sasa yuko katika wodi ya MOI ili kurahisisha uchunguzi,” alisema Almasi. Almasi alisema kiongozi huyo anaendelea na matibabu kufuatia majeraha yaliyotokana na kemikali hiyo aliyomwagiwa.

“Uso wake kwa upande wa kulia ndiyo umeharibika, hali hiyo inatokana na kemikali aliyomwagiwa,” alisema Almasi.
Wakati huohuo, Makamu wa Rais, Dk Bilal jana alimtembelea Sheikh Soraga ili kumjulia hali.
Akizungumza na waandishi wa habari Dk Bilal amewataka wananchi kuendelea kuwa na moyo wa kuheshimiana, kuthaminiana na kuvumiliana na kuacha kuchukua sheria mkononi. Alisema Serikali haitakubali kuona matukio kama hayo yakiendelea kutokea.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz