KATIKA kipindi cha ziadi ya wiki tatu nchi imekuwa katika matatizo makubwa ya upungufu wa bidhaa za mafuta ya petroli na dizeli hali yenye athari kwa uchumi wa nchi na usumbufu na gharama za ziada kwa wananchi.
Katika kipindi hicho viongozi na watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini wakiwemo Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na taasisi zilizochini ya Wizara hiyo hususan Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) wamekuwa wakitoa taarifa zenye mkanganyiko kuhusu matatizo yanayoendelea.
Hivyo, nasisitiza Waziri Mkuu kwa madaraka yake ya ibara ya 51 ya katiba ya udhibiti, usimamiaji na utekelezaji wa shughuli za siku hata siku wa kazi za Serikali na kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni badala ya kutoa tu kauli bungeni aagize Waziri wa Nishati na Madini awasilishe hoja ya taarifa ya Serikali juu ya utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu mafuta na hatua ambazo zimechukuliwa na Serikali juu ya matatizo ya mafuta yanayoendelea.
Uamuzi huu utaliwezesha bunge kutumia vizuri mamlaka na madaraka yake kwa mujibu wa katiba ibara ya 63 ya kuishauri na kuisimamia Serikali katika kipindi hiki ambacho hatma ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini haijulikani hata baada ya Spika kukabidhiwa ripoti ya “Kamati ya Ngwilizi”.
Iwapo Serikali itawasilisha tu kauli bungeni kwa mujibu wa kanuni ya 49 Bunge litafungwa na kanuni kwa kuwa kauli hizo za mawaziri hazipaswi kujadiliwa wakati kuna masuala muhimu ambayo yanapaswa kujadiliwa hata baada ya hatua zilizochukuliwa tarehe 02 Novemba, 2012 na Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo alipokutana na makampuni yanayohusika na biashara ya mafuta na yenye maghala ya kuhifadhia mafuta nchini.
Serikali ieleze hatua zilizochukuliwa za kuwawajibisha watendaji wa wizara, taasisi zake na makumpuni yaliyohusika kusababisha hali hii kutokana na uzembe, udhaifu na uhujumu wenye athari kwa uchumi wa nchi na maisha ya wananchi na bunge lipitishe maazimio ya hatua za ziada za kuchukua iwapo matatizo haya yatajirudia tena katika taifa letu.
Bunge lijadili hatua iliyochukuliwa ya kuagiza asilimia hamsini (50%) ya mafuta yaliyokuwa yanakwenda nje ya nchi (Transit fuel) yauzwe ndani ya nchi iwapo ilitekelezwa kwa ufanisi na kwa kuzingatia maslahi ya nchi kitaifa na kimataifa.
Bunge lipewe taarifa ya kina iwapo meli za Miss Marelina iliyokuwa ikishusha mafuta (ikiwa na MT 22,039 za diseli na MT 14,925 za Petroli) na Meli ya Eskden inayoendelea kushusha mafuta (yenye MT 32,000 za dizeli) kuhakikisha mafuta yake yanasambazwa kwa uwiano na kwa wakati mikoani kutokana na upungufu uliopo hususan katika maeneo ya vijijini.
Serikali kupitia kwa Wizara ya Uchukuzi na Mamlaka ya Bandari (TPA) kueleza sababu za kuchelewa kujengwa kwa Boya kubwa la kupakulia mafuta (SBM) toka mwaka 2011 na kueleza hatua zinazochukuliwa kuhakikisha kwamba boya hilo linaanza kazi katika kipindi kisichozidi wiki moja kuanzia sasa kama jambo la dharura.
Sababu za Serikali kutochukua hatua dhidi ya Bodi ya Wakurugenzi wa Mfumo wa Uagizaji Mafuta wa Pamoja (Petroleum Importation Cordinator-PIC) iliyokuwepo toka mwanzoni mwa mwaka ilipolalamikiwa na wadau na hatua zinazochukuliwa kwa haraka kufanya marekebisho ya kanuni kukidhi mahitaji ya Mfumo wa Uagizaji wa Pamoja ikiwemo mfumo mpya wa uundaji wa bodi.
Serikali itoe maelezo ya hatua iliyofikiwa katika uanzishwaji wa Mpango wa Hifadhi ya Akiba ya Mafuta ya Taifa (Strategic Petroleum Reserve – SPR) ambao ungekuwa kinga ya nchi pale panapojitokeza upungufu katika uingizaji wa mafuta au hujuma za mafuta kufichwa katika maeneo mbalimbali na wafanyabiashara wasio waaminifu.
Serikali kupitia Bunge iombe radhi kwa wananchi kutokana na athari zilizojitokeza kwenye uchumi wa nchi na maisha ya wananchi kutokana na matatizo ya mafuta kujirudia tena.
Wakati huo huo, natoa mwito kwa EWURA pamoja na kutangaza bei mpya elekezi ieleze hatua ambazo mamlaka hiyo imechukua mpaka sasa katika kuwafutia Leseni wafanyabiashara wote ambao wana leseni za kuagiza mafuta lakini hawafanyi kazi hiyo na kutaja orodha ya makampuni hayo kwa umma.
Pia EWURA ieleze sababu za Serikali kuzidiwa nguvu na wafanyabiashara ambapo Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (EWURA) inapotoa bei elekezi za kushuka huficha mafuta kwa kisingizio cha kulalamikia kanuni ya kupanga bei safari hii wakitarajia kupanda kwa bei jumatano ya kwanza ya mwezi tarehe 7 Novemba 2012.
Kutokana na hujuma hizo tatizo la upungufu wa mafuta nchini limeongezeka kutokana na udhaifu kwa kuzingatia kuwa taarifa za ndani ya maghala makubwa ya kuhifadhia mafuta zinadhihirisha kwamba pamoja za uzembe wa uchelewaji uliotokea nchi isingekuwa katika matatizo makubwa ya mafuta ikiwa hali hiyo ingedhibitiwa kwa Serikali kusimamia utawala wa sheria kulinda maslahi ya nchi na maisha ya wananchi.
Izingatiwe kwamba EWURA ilitoa taarifa katika vyombo mbalimbali vya habari tarehe 5 Novemba 2012 kukanusha kuhusu mkanganyiko uliopo Waziri Mkuu Mizengo Pinda amekiri bungeni kuwepo kwa kutofautiana kwa kauli baada ya kutakiwa kutoa majibu na Spika kufuatia muongozo nilliomba wa kutaka Serikali itoe kauli bungeni.
Nilieleza kwamba pamoja na kauli ya Naibu Waziri Simbachawene tarehe 2 Novemba 2012 bungeni kuwa matatizo yamemalizika hali bado ni tete hususan mikoani hatua ambayo ilimfanya Spika amtake Waziri Mkuu atoe majibu ambaye aliahidi kwamba Serikali itatoa kauli kabla ya kuisha kwa shughuli za Bunge katika mkutano unaoendelea. Hivyo, nitaendelea kuisimamia Serikali kuchukua hatua zinazostahili kwa kadiri matatizo haya yatakavyoendelea.
Imetolewa tarehe 6 Novemba 2012 na:
John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini