Makamu wa Rais, Dk. Bilal Awavuta Wawekezaji

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein,akisalimiana na Balozi wa Spain nchini Tanzania, Luis Manuel Cuesta,alipofika Ikulu Mjini Zanzibar [Picha na Ramadhan Othman, Ikulu]

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewakaribisha wawekezaji kutoka Hispania kuja kuekeza Zanzibar hasa katika sekta ya utalii, kutokana na nchi hiyo kupata mafanikio makubwa katika sekta ya utalii na kuweza kutajika duniani. Dk. Shein aliyasema hayo wakati alipokuwa na mazungumzo na Balozi wa Hispania nchini Tanzania Mhe. Luis Manuel Cuesta, aliyefika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha.

Katika maelezo yake, Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar ina mengi ya kujifunza kutoka Hispania hasa katika sekta ya utalii ambapo nchi hiyo imeweza kupata mafanikio makubwa na kusisitiza haja ya kuja kuekeza katika ujenzi wa hoteli kubwa na za kisasa. Alisema kuwa licha ya kuimarishwa kwa sekta ya Utalii hapa Zanzibar lakini pia ipo haja kwa kuendelea kujenga hoteli kubwa zaidi na za kisasa ikiwa ni miongoni mwa vivutio vya utalii.

Kutokana na mafanikio hayo, Dk. Shein alieleza kuwa ipo haja kwa Shirika la ndege la IBERIA la nchi hiyo kufanya safari zake moja kwa moja hadi Zanzibar kama ilivyo kwa mashirika ya ndege ya nchini Italia hivi sasa. Alieleza kuwa hatua hiyo itawarahisishia watalii wengi wanaotoka nchini humo kuja Zanzibar kirahisi pamoja na kuimarisha sekta hiyo ya utalii hapa nchini.

Kwa upande wa nishati, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa ipo haja ya kuwepo kwa mashirikiano katika sekta ya nishati licha ya Mradi mkubwa wa umeme unaoendelea kutekelezwa hivi sasa chini ya ufadhili wa MCC, kwani bado Zanzibar inahitaji kuwa na chanzo chengine cha nishati.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alimuhakikishia Balozi huyo kuwa amani na utulivu iliyopo nchini itaendelea kuimarishwa kwa wageni wanaokuja kuitembelea Zanzibar pamoja na kwa wananchi wenyewe wanaoishi hapa nchini kwani hiyo ndio ajenda kuu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Katika suala zima la utamaduni na michezo Dk. Shein alimueleza Balozin Cuesta kuwa kuna uwiano mkubwa wa utamaduni kati ya Hispania na Zanzibar hasa katika mchezo maarufu wa ngombe ambao umekuwa ukichezwa hapa Zanzibar huko kisiwani Pemba na pia umekuwa ukichezwa nchini humo.

Kwa upande wa sekta ya Michezo, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa kutokana na nchi hiyo kupata mafanikio makubwa kimichezo hasa katika mpira wa miguu ameona haja ya kuwepo ushirikiano kwani Zanzibar ina mengi ya kujifunza kutoka Hispania.

Aidha, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa ni jambo la busara kama kutakuwa na ushirikiano zaidi katika mpira huo wa miguu ikiwa ni pamoja na kutazama uwezekano wa kupata kocha wa kufundisha timu ya Taifa ya Zanzibar kutoka nchini humo.

Alieleza kuwa kwa vile Zanzibar ina historia kubwa katika sekta ya michezo imefikia wakati kurejesha hadhi yake hiyo ili iweze kutajika tena katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kama ilivyokuwa hapo siku ya nyuma katika upande wa soka.

Nae Balozi wa Hispania nchini Tanzania, Mhe. Cuesta, alimueleza Dk. Shein kuwa nchi hiyo inathamini uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati yake na Zanzibar na kusisitiza kuwa iko tayari kutoa ushirikiano wake katika sekta ya utalii kwani Zanzibar imebarikiwa kuwa na vivutio vingi vya kitalii.

Balozi Cuesta alisema kuwa tayari kuna Makampuni kadhaa kutoka Hispania ambayo yana azma ya kuja kuekeza katika sekta za miundombinu na nishati hapa nchini, ambapo alisisitiza kuwa Hispania ina utaalamu mkubwa wa nishati itokanayo na bahari na upepo.

Pia, balozi huyo alimuhakikishia Dk. Shein kuwa juhudi za makusudi atazichukua juu ya ushirikiano katika usafiri wa anga kwa kuhakikisha kuna kuwepo usafiri wa moja kwa moja kati ya Hispania na Zanzibar kwa kupitia mashirika ya ndege ya nchi hiyo.

Balozi huyo alieleza kuwa licha ya Hispania kuwa na msuko suko wa kiuchumi lakini ana matumaini kuwa mafanio makubwa yatapatikana katika kipindi kifupi kijacho hatua ambayo pia, itatoa nafasi nzuri ya kuimarisha ushirikiano kati ya nchi mbili hizo. Wakati huo Dk. Shein alifanya mazungumzo na Mwakilishi mpya wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo ya Watoto Duniani (UNICEF), Dk. Jama Gulaid ambaye alifika Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha.

Katika mazungumzo yao, Mwakilishi huyo alimueleza Dk. Shein kuwa Shirika hilo litaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuhakikisha Watoto wanapata haki zao za msingi pamoja na maendeleo katika nyanja zao zote za kimsingi. Mwakilishi huo alisifu juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuendelea kusimamia maendeleo ya watoto hapa nchini.

Pia, Mwakilishi huyo alitoa pongezi kwa uongozi uliopo madarakani na kueleza kutokana na juhudi na mashirikiano yaliopo ni rahisi kwao kutekeleza majukumu yao ya kazi. Aligusia maeneo mbali mbali ambayo UNICEF imekuwa ikitekeleza katika kukuza ustawi wa watoto na wazazi kwa upande wa Zanzibar na Tanzania nzima kwa ujumla.

Kwa upande wa Dk. Shein, alimkaribisha Mwakilishi huyo mpya hapa nchini na kumueleza uzoefu wake alionao kwa shirika hilo kutokana na kuiunga mkono Zanzibar kwa muda mrefu.

Alieleza kuwa Shirika hilo siku nyingi limekuwa likiiunga mkono Zanzibar katika nyanja kadhaa zikiwemo utekelezaji wa sheria za watoto, kupambana na maradhi mbali mbali yakiwemo Malaria na Ukimwi pamoja na miradi ya maji safi na salama na mengineyo.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alitoa shukurani zake kwa Shirika hilo kwa jitihada zake za kuiunga mkono Serikali katika utekelezaji wake wa mipango mikubwa ukiwemo Dira ya 2020 na Mpango wa Kuondoa Umasikini Zanzibar (MKUZA).

Dk. Shein alimkaribisha Zanzibar Mwakilishi huyo wa UNICEF na kumueleza kuwa ujio wake wa kufanya kazi nchini Tanzania umekuwaja wakati muwafaka kwani Zanzibar inahitaji zaidi mashirikiano na Shirika hilo katika kuendeleza maendeleo ya watoto.