SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa ya Ruvuma (FARU) na Njombe (NJOREFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika Novemba 4 mwaka huu.
Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza vyama hivyo unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa FARU na ule wa NJOREFA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia mchezo huo katika mikoa yao.
TFF inaahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa kamati za utendaji za NJOREFA na FARU zilizochaguliwa chini ya uenyekiti wa Stanley Lugenge (NJOREFA) na Golden Sanga (FARU).
Uongozi huo mpya wa vyama hivyo una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu kwa kuzingatia katiba za vyama vyao pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yao.
Pia tunatoa pongezi kwa kamati za uchaguzi za FARU na NJOREFA na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi unaendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Viongozi waliochaguliwa kuongoza FARU ni Golden Sanga (Mwenyekiti), Dk. Kiyo (Makamu Mwenyekiti), Ahmed Chale (Katibu), Aljaba Chitete (Katibu Msaidizi), Humphrey Milanzi (Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF), James Mhagama (Mwakilishi wa Klabu TFF) wakati wajumbe ni Kevin Haule na Emmanuel Kamba.