LEO ni siku muhimu kwa Wamarekani kwani wapiga kura wa Marekani wanatarajia kuhitimisha zoezi la upigaji kura katika majimbo yote ili kumpata mshindi katika uchaguzi wa urais ulio na ushindani mkubwa.
Rais wa Marekani Barack Obama na mpinzani wake Mitt Romney siku ya jumatatu walifanya kampeni za dakika za mwisho kwa wapiga kura katika majimbo muhimu ikiwa imebakia siku moja kabla ya uchaguzi katika juhudi za mwisho kuvunja ushindani. Katika majimbo ya wisconsin , rais Obama alimshutumu bwana Romney kwa kujaribu kurejesha mawazo mabaya aliyoyatoa kabla na kusema taifa haliwezi kufanikiwa bila kuwa na daraja la kati lenye nguvu.
Kwenye mkutano wa jana asubuhi katika jimbo la kusini la Florida bwana Romney aliwaambia wafuasi wake kwamba kiongozi huyo aliyoko madarakani Mdemocrat ameshindwa kutekeleza ahadi zake wakati aliposhinda kiti cha urais mwaka 2008.
Wananchi wapiga kura nchini Marekani leo wanaelekea kwenye vituo vya kupigia kura katika uchaguzi huo wa Rais huku wagombea, Rais Obama wa chama cha Democrat na Mitt Romney kutoka chama cha Republican wakichuana vikali katika majimbo yanayojulikana kwa Pendulum (Swing States) ambayo ndiyo yanayotarajia kutegua kitendawili cha mchuano huo.
Rais Obama mwenye umri wa miaka 51 na mpinzani wake Romney mwenye umri wa 65 wanazidiana kidogo kwa mujibu wa maoni yanayochapichwa na vyombo vya habari. Katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2000, mgombea wa Democrat alimshinda Bush wa Republican kwa karibu kura 500, lakini Bush alikuwa rais kutokana na kupata kura 271 za Electoral College ikilinganishwa na 266 za mgombea wa Democrat.
Ili kushinda katika uchaguzi huu mgombea analazimika kujikusanyia kura za electoral Collage zisizopungua 270 na tayari Obama amejikusanyia kura 237 wakati mpinzani wake Romney akifikisha kura 206. Kitendawili kimesalia katika majimbo ambayo wapiga kura wake bado hawajashawishika yanayoshikilia kura 95.
VOA