Rais Kikwete Afungua Mradi wa Maji Singida

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia wananchi akiwa ziarani. Picha na Ikulu

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete Novemba 4, 2012, ameweka jiwe la msingi kwenye mradi mkubwa wa maji unaolenga kumaliza tatizo la maji mjini Singida. Rais Kikwete ameweka jiwe la msingi katika sherehe ya kufana iliyofanyika katika eneo la Mradi la Mwankoko, nje ya mji wa Singida, mara baada ya kuwasili Mkoani Singida kuanza ziara ya siku mbili kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo akitokea Mkoani Manyara ambako alifanya shughuli hizo hizo kwa siku mbili pia.

Mradi huo ulioanza kujengwa Novemba 2, mwaka 2009, umekamilika kwa kiasi cha asilimia 80 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 31, mwaka huu wa 2012. Kwa mujibu wa maelezo ya wasimamizi wa Mradi wa SUWASA, Mradi huo unagharimu dola za Marekani milioni 19.7 sawa na Sh.bilioni 31.126. Kati ya fedha hizo, Serikali ya Tanzania imetoa dola za Marekani milioni 10.42 sawa na Sh. 16, 463,600,000, Benki ya Maendeleo ya Nchi za Kiarabu (BADEA) imetoa dola za Marekani milioni 4.57 sawa na Sh. 7,220,600,000 na Mfuko wa OPEC kwa Maendeleo ya Kimataifa wa OFID umetoa dola za Marekani milioni 4.7 sawa na Sh. 7,426,000,000.

Mradi huo unaotekelezwa na Kampuni ya Spencon Services Limited unatarajiwa kutoa lita 17,208,000 kwa siku kutokana na visiwa viwili vilivyoko Mwankoko vyenye uwezo wa kuzalisha lita 292,000 kwa saa na visima viwili vilivyoko eneo la Irao vyenye uwezo wa kuzalisha tani 425,000. Mradi huo unatarajiwa kutoa huduma kwa jumla ya wateja 3,500 kati yao 2,500 katika awamu ya kwanza na wengine 1,000 katika awamu ya pili.

Mradi huo utaongeza upatikanaji wa maji kwa karibu kiasi cha asilimia 100 kwa wakazi wa mji wa Singida na utaongeza muda wa kupatikana maji kutoka saa tano za sasa kwa siku hadi saa 24 kwa siku.