MAWAZIRI Wakuu wa zamani pamoja na wapinzani wa CCM wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete na Serikali yake kwa juhudi za kuleta maendeleo nchini na utekelezaji wake wa kiwango cha juu wa Ilani za Chama cha Mapinduzi (CCM) za Chaguzi Kuu za 2005 na 2010. Pongezi hizo zimetolewa na waliokuwa Mawaziri Wakuu Waheshimiwa Frederick Tluway Sumaye na Edward Lowassa wakati wa ziara ya Rais Kikwete katika mikoa ya Arusha na Manyara, ziara ambayo inamalizika Novemba 5, 2012.
Katika pongezi zake kwa Rais Kikwete, Mheshimiwa Lowassa amesema: “Mheshimiwa Rais naomba radhi kwa kushindwa kuhudhuria shughuli ya leo kwa sababu niko Ujerumani nikifanyiwa uchunguzi na uangalizi wa macho yangu na afya yangu kwa jumla. Lakini Mheshimiwa Rais tunakupongeza sana na kukushukuru kwa miradi uliotujengea katika Mkoa wa Arusha.”
Lowassa ameongeza kumwambia Rais Kikwete katika ujumbe wa simu (sms) ambayo amemtumia Mkuu wa Wilaya ya Monduli Mheshimiwa Njowika Kasugga na ambao aliusoma kwenye sherehe ya uwekaji jiwe la msingi kwenye ukarabati wa Barabara ya Minjingu-Arusha Novemba 3, 2012:
“Kwa hakika umetekeleza vizuri na kwa uaminifu Ilani za Chama cha Mapinduzi (CCM) za 2005 na 2010. Tunajivunia mafanikio yako haya. Tunajivunia uongozi wako. Wewe ni kiongozi mkuu ambaye umesimamia vizuri maendeleo ya nchi yetu na uongozi wa nchi yetu. Ndiyo maana tutakapokutana kwenye Mkutano Mkuu wa Chama chetu wiki ijayo kila mwana-CCM atakuwa anasimama kifua mbele.”
Naye Mheshimiwa Sumaye amemwambia Rais Kikwete: “Sisi wana-Katesh tunakushukuru sana kwa kutufikiria na kutuweka katika ratiba yako kwenye ziara yako hii. Aidha, Mheshimiwa Rais tuko pamoja na Serikali yako, tunakupongeza sana kwa mafanikio mengi ambayo yamepatikana katika kipindi cha uongozi wako. Tunaipongeza sana Serikali yako kwa kazi nzuri na tunaitambua kazi hiyo.”
Mheshimiwa Sumaye alikuwa anazungumza kwenye mkutano wa hadhara ambao ulihutubiwa na Rais Kikwete mjini Katesh wakati akiwa njiani kwenda Singida kwa ziara ya siku mbili kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo. Akizungumza kwenye mkutano huo huo, Mbunge wa Viti Maalum wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mheshimiwa Rose Kamili amemshukuru Rais Kikwete na Serikali yake kwa kutimiza ahadi zake.
Mheshimiwa Kamili amemwambia Rais Kikwete: “Tunakushukuru na kukupongeza kwa kutimiza ahadi zako na ahadi za Serikali yako kwa wananchi wakiwamo wananchi wa Hanang.” Pongezi hizo za Mheshimiwa Kamili zimekuja kufuatia pongezi za namna hiyo ambazo zimetolewa na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, Mbunge wa Rombo (CHADEMA), Joseph Selasini na Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema wakati wa ziara ya Rais Kikwete katika Mkoa wa Kilimanjaro.