RAIS wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania, Jakaya Kikwete amewaonya watu na makundi ya watu wanaotafuta visingizo vya kufanya fujo kupitia siasa na dini wasiilazimishe Serikali yake kutumia nguvu za dola kupambana na hali hiyo. Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali yake imedhamiria kumaliza tatizo la walimu nchini katika miaka mitatu ijayo kwa sababu ya jitihada kubwa zinazofanyika kufundisha walimu.
Rais Kikwete ameyasema Novemba 4, 2012, wakati alipozungumza na wananchi mjini Katesh, Wilaya ya Hanang, Mkoa wa Manyara kwenye siku ya pili na ya mwisho mkoani humo. Rais Kikwete amesimama mjini Katesh akiwa njiani kwenda Mkoa wa Singida kuendelea na ziara yake ya mikoa minne ya kukagua, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi ya maendeleo, ziara ambayo tayari imempitisha katika Mikoa ya Kilimanjaro na Arusha.
Katika hotuba yake ambako alizungumzia masuala mbalimbali ya maendeleo na jitihada za Serikali yake katika kuboresha sekta za elimu, maji, afya na miundombinu, Rais Kikwete ametoa onyo kali kwa watu wanatafuta visingizo vya dini na siasa kufanya fujo nchini.
Amewaambia mamia ya wananchi wa Katesh: “Nimesema na nataka kurudia kuwa Serikali haitaruhusu watu wachache kutuharibia amani na utulivu kwa tamaa zao za siasa ama kwa tamaa zao za dini.”
Ameongeza: “Kama ni lazima Serikali itatumia nguvu za dola kulinda amani na ulituvu uliopo nchini. Lakini nawaomba watu hawa wasitufikishe huko kwenye virungu. Lakini wasiposikia na wakaendelea kukaidi, tutalazimika kufanya hivyo.” Amesema kuwa njia pekee ya kuendelea kuishi kwa amani ni kwa Watanzania kuendelea kuvumiliana katika tofauti zao za kidini, kikabila, kisiasa, rangi za miili na maeneo watokako kwa sababu haitawezekana kundi moja likalazimisha mabadiliko kwa manufaa ya kundi hilo tu. Kuhusu tatizo la ukosefu wa walimu linaloendelea kuzikabili shule karibu zote nchini, Rais Kikwete amesema kuwa katika miaka mitatu, Serikali yake itaweza kumaliza tatizo hilo.
“Tulipoingia madarakani, walikuwa wanapatikana wahitimu wa ualimu 500 kwa mwaka kutoka vyuo vyetu vyote nchini, sasa idadi hiyo kwa mwaka ni walimu 12,000 kwa sababu tumepanua sana nafasi za elimu ya ualimu ama tumefungua vyuo vipya kikiwamo Chuo Kikuu cha Dodoma.”
Kabla ya kuzungumza na wananchi, Rais Kikwete amekagua uzalishaji wa vifaa vya ngozi kwenye Mradi wa Ngozi wa Katesh ambako ameahidi kuwatafutia mitambo ya kisasa kutoka Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO) ili kuongeza kasi na urahisi wa uzalisha wa bidhaa za ngozi nchini.
Aidha, Rais Kikwete amewaahidi wananchi wa Katesh kuwa Serikali yake itawatafutia haraka iwezekanavyo kiasi cha Sh. milioni 395.18 kinachokwamisha kumalizika kwa mradi mkubwa wa maji katika eneo hilo kwa ajili ya kukabiliana na tatizo kubwa la maji mjini hapo.
“Hatuwezi kuwaacha wananchi wanahangaika kwa sababu ya Sh. milioni 300 hasa baada ya wao kufanya jitihada kubwa kukabiliana na tatizo hili la maji. Nikirudi Dar Es Salaam, nitatafuta fedha,” amesema Rais Kikwete.