Na Mwandishi Maalum
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema hakuna mtu yoyote ama kikundi chochote cha watu kitakachoruhusiwa kuvuruga amani na utulivu wa Tanzania. Aidha, Rais Kikwete amewataka wananchi kuepukana na mtego wa kufanywa kaseti na gramafoni ya watu wengine katika mchakato wa sasa wa kutoa maoni kwa ajili ya Katiba Mpya ya Tanzania.
Rais Kikwete ameyasema hayo Novemba Mosi, mwaka 2012, wakati alipozungumza na wananchi wa Wilaya ya Arumeru, Mkoa wa Arusha, baada ya kuwa amefungua rasmi hospitali ya Serikali ya Olturumet nje kidogo ya mji wa Arusha. Rais Kikwete amewaambia wananchi hao kuwa mambo ya fujo ambayo yamejitokeza nchini katika wiki za karibuni ni mambo ya aibu na ya kuchukiza.
“Yaliyotokea na yanayoendelea kuonyesha dalili za kujitokeza ambako watu wanafanya fujo ni mambo ya aibu na ya kuchukiza. Wapo watu wanaotumiwa ili kuvuruga amani ya nchi yetu kwa sababu siyo kila mtu anafurahia utulivu ulioko hapa nchini.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Lakini wananchi msiwe na wasiwasi, sisi tutashughulika na hawa watu na kwa kweli hakuna mtu yoyote ama kikundi cha watu kitakachoruhusiwa kuvuruga amani na utulivu wa Tanzania.”
Hivi karibuni hasa katika Jiji la Dar es Salaam na Zanzibar, zimejitokeza fujo zilizopelekea watu kadhaa kutiwa mbaroni na polisi na kufikishwa mahakamani.
Kuhusu mchakato wa Katiba Mpya, Rais Kikwete amewataka wananchi kuwa huru kutoa maoni yake mbele ya wajumbe wa Tume ya Katiba. Amewaambia wananchi: “Toeni maoni yenu kwa uhuru kabisa, msitishwe na mtu yoyote. Jambo moja tu nataka kulisema – msigeuke kuwa kaseti ama gramafoni za kutangaza na kunadi maoni ya mtu mwingine. Hii ndiyo njia itakayotuwezesha sote kupata Katiba nzuri na itayoitumikia nchi yetu kwa miaka mingi ijayo.”
Wakati huo huo; RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete jana, Novemba Mosi, 2012, amezindua rasmi mradi mkubwa wa kuboresha na kuendeleza miji ya Tanzania unaojulikana kama Mradi wa Uboreshaji Miji ya Tanzania (Tanzania Strategic Cities project – TSCP) utakaogharimu mabilioni ya fedha.
Aidha, Rais Kikwete amezidua rasmi Jiji la Arusha katika sherehe ya kufana iliyofanyika kwenye Mnara wa Azimio la Arusha katikati ya jiji hilo. Mradi wa TSCP unalenga kuboresha huduma za msingi katika miji saba na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) kwa kujenga upya, kukarabati na kupanua miundombinu pamoja na kuijengea uwezo wa kukusanya na kusimamia mapato ya miji husika.
Mradi ni moja ya miradi mitatu inayogharimiwa na Benki ya Dunia kwa nia ya kuboresha miji ya Tanzania. Mbali na TSCP, miradi mingine ni Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (Dar es Salaam Metropolitan Development Project – DMDP) na Urban Local Government Strengthening Programme (ULGSP). Mpaka sasa Benki hiyo imekwisha kutoa Sh. bilioni 8.76 kati ya Sh. bilioni 34.7 za TSCP.
Chini ya TSCP ambao unagharimu kiasi cha Sh. bilioni 191.3 miji itakayonufaika ni Tanga, Arusha, Mwanza, Kigoma, Dodoma, Mbeya, Mtwara na CDA ambayo ndiyo itakayopata pesa kubwa zaidi kuliko mjini mingine.
Aidha, chini ya TSCP, miji hiyo itajengewa miundombinu ya barabara zenye jumla ya kilomita 141.2, ujenzi wa madampo matano, ununuzi wa vifaa vya kusimamia taka ngumu, vituo vya mabasi sita, vituo viwili vya kuegesha malori na kilomita 15.9 za mitaro ya maji ya mvua.
Katika mji wa Arusha, kiasi cha barabara za lami zenye urefu wa kilomita 7.23 zitajengwa, mtaro mkubwa wa maji ya mvua wa mita 800 utajengwa, zitafungwa taa za kuongoza magari kwenye makutano ya barabara tatu ambazo ni Sokoine na Viwandani, Sokoine na Esso na Kanali Middleton na Makongoro. Katika awamu ya pili, kiasi cha barabara zenye urefu wa kilomita 7.8 zitajengwa katika Jiji la Arusha.
Miji itakayonufaika na ULGSP ambako Benki ya Dunia inatoa mkopo wa dola za Marekani milioni 255 na unatarajiwa kuanza katika mwaka ujao wa fedha ni Morogoro, Tabora, Moshi, Sumbawanga, Shinyanga, Songea, Singida, Musoma, Iringa, Bukoba, Lindi, Njombe, babati, Kibaha, Mpanda, Geita, Korogwe na Bariadi.
DMDP kwa ajili ya Jiji la Dar Es Salaam, itahusika wilaya zote tatu za Kinondoni, Ilala na Temeke na utagharimu kiasi cha dola za Marekani milioni 75.
Baada ya kuzindua mradi huo wa TSCP, Rais Kikwete amezindua Jiji la Arusha ambalo linapanda hadhi kutoka Manispaa. Katika uzinduzi huo, Rais amezindua nembo ya Jiji pamoja na kukabidhi cheti cha kulipandisha hadhi Jiji hilo.
Rais Kikwete amezindua miradi hiyo ikiwa ni shughuli zake katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku mbili kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Arusha. Rais amewasili Arusha mchana wa jana kutoka Dodoma.