RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, Oktoba 31, 2012 ameungana na mamia ya waombolezaji kumuaga na kumzika Bi. Lucy Adam Samillah ambaye alikuwa mtumishi wa Ikulu kwa miaka mingi akiwa ni Msimamizi (House Keeper) wa Ikulu Ndogo ya Arusha.
Rais Kikwete amewasili nyumbani kwa marehemu Bi. Lucy mjini Arusha kiasi cha saa sita mchana kuungana na mamia ya waombolezaji akiwamo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo K. Pinda na viongozi wengine wa Serikali.
Baada ya shughuli za kuaga mwili, Rais Kikwete aliungana tena na waombolezaji kwenye makaburi ya Njiro ambako mwili wa marehemu Bi. Lucy uliteremshwa kaburini kiasi cha saa saba na dakika 45 mchana.
Mara baada ya mwili kuwekwa kaburini, Rais Kikwete amekuwa wa kwanza kuweka udogo kwenye kaburi akifuatiwa na Pinda. Marehemu Lucy Adam Samillah alifariki dunia usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita akiwa na umri wa miaka 62 baada ya kupigana kwa miezi mingi na ugonjwa wa kansa.
Marehemu Bi. Lucy alizaliwa mwaka 1950 katika kijiji cha Wota kilichoko Wilaya ya Mpwapwa, Mkoa wa Dodoma. Alijiunga na Chuo cha Ualimu cha Ndala, Tabora mwaka 1965 baada ya kumaliza masomo ya darasa la nane. Alihitimu mwaka 1967 akiwa na Cheti cha Ualimu Daraja la Tatu.
Alianza kufundisha mwaka 1968 huku akiendelea kujiendeleza hadi kufikia Ualimu Daraja la tatu A na aliajiriwa Ikulu mwaka 1979 akiwa ni Msimamizi Msaidizi (Assistant House Keeper) na katika miaka yake Ikulu, Bi. Lucy aliweza kuwatumikia marais wote wanne wa Tanzania mpaka sasa.
Bi. Lucy alikuwa mwajiriwa wa Ikulu kwa miaka 33 na mpaka mauti yanamfika alikuwa Msimamizi wa Ikulu Ndogo ya Arusha. Marehemu ameacha watoto watatu.