EAC Yaimarisha Kitengo cha Tahadhari Kukabiliana na Usalama

Nembo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki

Na Isaac Mwangi, EANA-Arusha

KATIKA juhudi za kuimarisha mfumo wa ulinzi na usalama kikanda, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imeamua kukiimarisha kitengo chake cha utoaji taadhari na uwezo usuluhishi wa migogoro, Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) limeripoti.

Naibu Katibu Mkuu wa EAC anayeshughulikia Shirikisho la Kisiasa, Dk Julius Rotich, alisema hatua hiyo inatokana na kuwepo umuhimu mkubwa katika kufuatilia masuala yanayohusiana na matunda yaliyopatikana kutokana na kuimarishwa kwa demokrasia, utawala bora, utawala wa sheria na utetezi wa haki za binadamu na haki ya msingi ya uhuru.

Aliyasema hayo alipokuwa anafungua mkutano wa kitaalam wa siku tatu wa robo mwaka kati ya Umoja wa Afrika(AU) na Jumuiya za Kiuchumi za Kikanda uliofanyika hivi karibuni jijini Arusha. Mkutano huo ulijadili uendeshaji wa mfumo wa utoaji taadhari katika Afrika.

“Mkutano wenu unafanyika katika mazingira ya kuwepo ukuaji wa changamoto mpya katika ulinzi na usalama katika kanda ya EAC. Ugaidi, usafirishaji haramu wa binadamu na madawa ya kulevya, ukabila na vurugu katika jamii, migogoro ya kidini, uharamia na utakatishaji fedha vinaongezeka katika kiwango cha kutisha,” Dk Rotich aliwaambia washiriki wa mkutano huo.

Aliongeza, “Madhara ya mabadiliko ya hali ya hewa na matokeo hasi katika usalama wa chakula na uhaba wa rasilimali vinamchango wake katika picha hii mbaya. Kazi yenu kwa pamoja na wadau wengine inategemewa kusaidia kuzuia madhara yanayotokana na changamoto hizo.”

Changamoto hizo, alisema, zimeongzeka kutokana na kuwepo kwa Umoja wa Forodha na utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja kuhakikisha kwamba kunakuwapo na mwingiliano huru wa watu, kazi, huduma na mitaji na usalama wa uwekezaji katika mipaka.

Hata hivyo, changamoto za kiusalama hazipo katika Afrika Mashariki pekee. “Bara hili katika miaka miwili iliyopita limejionea baadhi ya changamoto mbaya zaidi za ulinzi na usalama, na zaidi katika ile inayojulikana ‘’ghasia zilizoibuka katika nchi za Kiarabu,” Dk Rotich alisema. “Mgawanyiko na kusambaa kwa migogoro hii na kujumuisha na madhara ya hali mbaya ya uchumi kimataifa, ni hofu mpya za ulinzi na usalama zinazolikera bara la Afrika.”

Malengo ya juhudi hizi zote ni kusadia utoaji wa tahadhari,kuzuia migogoro ya ndani na baina ya nchi wananchama wa AU. Hii ni mara ya pili EAC kuwa mwenyeji wa mkutano kama huo ambapo kwa mara ya kwanza ulifanyika Aprili 2009.