Uholanzi Kuhimarisha Uhusiano na Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akisalimiana na Balozi wa Uholanzi Nchini Tanzania Dk. Ad Koekkoek alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo kusalimiana na Rais. [Picha na Ramadhan Othman, Ikulu]

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

UHOLANZI imeeleza azma ya kuzidisha uhusiano na ushirikiano kati yake na Zanzibar katika kuimarisha sekta ya utalii na kusisitiza kuwa tayari mashirika ya ndege kutoka nchini humo likiwemo Shirika la ndege la KLM yameonesha nia ya kufanya safari zake moja kwa moja kutoka Uholanzi hadi Zanzibar.

Balozi wa Holland nchini Tanzania, Dk. Ad Koekkoek aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, Ikulu mjini Zanzibar. Katika maelezo yake Balozi Koekkoek alimueleza Dk. Shein kuwa nchi yake inathamini sana uhusiano na ushirikiano uliopo kati yake na Tanzania ikiwemo Zanzibar na kuahidi kuukuza na kuuendeleza hasa katika sekta mbali mbali za kimaendeleo ikiwemo utalii.

Balozi huo alieleza kuwa ili kuhakikisha ushirikiano huo wa pande mbili hizo unadumishwa alisisitiza haja hiyo ya kuwepo kwa usafiri wa moja kwa moja wa anga kutoka Holland mpaka Zanzibar hatua ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa kukuza sekta ya utalii na hata sekta ya biashara.

Aidha, Balozi huyo alieleza kufarajika kwake kwa kuwepo uhusiano na ushirikiano kati ya Zanzibar na Uholanzi ambao unazidi kuimarika siku hadi siku. Katika mazungumzo hayo Balozi Koekkoek alimueleza Dk. Shein kuwa amefurahishwa sana na juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuendeleza sekta hiyo ya utalii nchini.

Alisema kuwa Zanzibar imebarikiwa kuwa na vivutio vingi vya kitalii hatua ambayo imepelekea kuongezeka kwa idadi ya watalii kutoka kila pande ya dunia ikiwemo nchi ya Uholanzi. Kutokana na hatua hiyo Balozi Koekkoek ameeleza kuwa ipo haja ya kuzidisha uhusiano katika sekta ya utalii hasa ikizingatiwa kuwa na ushindani mkubwa katika sekta ya utalii katika nchi za visiwa vidogo vidogo.

Kwa upande wa sekta ya biashara Balozi huyo alimueleza Dk. Shein kuwa wafanya biashara kutoka Uholanzi wamevutiwa na fursa kadhaa za kuekeza zilizopo Zanzibar ambazo zitawarahisishia kuwekeza. Balozi Koekkoek alieleza kuwa juhudi na azma ya Serikali yaMapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya ikiwa ni pamoja na kuipandhisha daraja hospitali ya Mnazi Mmoja kuwa hospitali ya rufaa hi za kupongezwa.

Hivyo ameahidi kuwa nchi yake itaendelea kuunga mkono juhudi hizo kwa hatua mbali mbali ambapo hivi sasa teyari mikakati kadhaa imeshawekwa ya kuhakikisha ufanikishaji wa suala hilo. Balozi huyo alieleza kuwa Zanzibar imekuwa na utajiri mkubwa wa rasilimali za bahari hivyo kuna umuhimu wa kulindwa na kuhifadhiwa huku akiipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa hatua mbali mbali inayochukua katika kuhifadhi rasilimali hizo na kueleza haja ya kukuza na kuimarisha ushirikiano katika sekta hiyo muhimu.

Kwa mara nyengine tena Balozi huyo alitoa mkono wa pole kwa ajali ya kuzama kwa meli ya MV.Skagit iliyotokezea Julai mwaka huu na kusababisha maafa makubwa yaliyopelekea kwa vifo kwa raia wengi wa Tanzania na wageni kutoka nje ya Tanzania. Balozi huyo alitoa shukurani zake kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano alioupata katika kuhakikisha raia wa Uholanzi ambao waliokuwemo katika ajali hiyo katika upatikanaji wa taarifa na kuwashughulikia vyema.

Naye Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alitoa shukurani zake kwa nchi ya Holland kutokana na kuimarisha uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya nchi hiyo na Zanzibar ambao ni wa muda mrefu na umeweza kuleta maendeleo kwa pande zote mbili.

Dk. Shein alielzea uzoefu wake alioupata wakati akiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi Uholanzi iilivyokuwa ikiunga mkono Tanzania katika nyanja mbali mbali za maendeleo hatua ambayo imesaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha sekta hizo za maendeleo endelevu kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa upande wa sekta ya utalii Dk. Shein alitoa pongezi kwa Balozi huyo binafsi na kwa nchi yake kwa azma alionayo katika kuimarisha mashirikiano katika sekta hiyo na kueleza furaha yake juu ya azma ya kuanzishwa kwa usafiri wa anga wa moja kwa moja kati ya Uholanzi na Zanzibar hatua ambayo itasaidia kuongeza idadi ya watalii nchi na kuinua pato la taifa nchini.

Dk. Shein aliipongeza azma ya Uholanzi ya kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya ikiwa ni pamoja na kuiimarisha hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja ambayo yote hayo ni miongoni mwa malengo ya Serikali ya Mapainduzi Zanzibar. Kuhusu suala la uhifadhi wa mazingira ya bahari Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar itaendeleza juhudi zake katika uhifadhi wa mazingira na kutoa shukurani kwa ushirikiano unaotolewa na Uholanzi kwa Zanzibar katika uhifadhi wa mazingira hayo.

Hata hivyo, Dk. Shein alieleza kuwa katika kuhakikisha usalama wa usafiri wa bahari unaimarishwa zaidi mashirikiano makubwa ya Mamlaka za bahari kati ya Zanzibar na Tanzania Bara zikiwemo SUMATRA na ZMA zinaimarishwa. Dk. Shein alieleza kuwa mbali ya juhudi hizo zinazochukuliwa na Serikali katika kuhakikisha usalama wa bahari unaimarika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imo katika mchakato wa ununuzi wa meli mpya ambayo itasaidia katika usafiri wa baharini hasa kwa wananchi wenye kipato cha chini.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kufarajika kusikia azma ya wawekezaji kutoka Uholanzi kuja kuwekeza Zanzibar na aliwaahidi kuwa Zanzibar itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji. Sambamba na hayo, Dk. Shein alimuhakikishia Balozi huyo kuwa amani na utulivu iliyopo nchini itaimarishwa.