Chama Cha Wapangaji Waja Juu Watoa Karipio Kwa NHC

Baadhi ya viongozi na wajumbe wa juu wa Chama cha Wapangaji Tanzania wakizungumza na vyombo vya habari.


Baadhi ya viongozi wa Chama Cha Wapangaji nchini wakizungumza na waandishi wa habari.

Na Mwandishi Wetu

CHAMA cha Wapangaji nchini kimelitaka Shirika la Nyumba Taifa (NHC) kuacha utaratibu wa kuziuza nyumba za shirika hilo kwa kisingizio cha mpangaji kukaa muda mrefu kwenye nyumba, na badala yake kuweka utaratibu wa kikomo cha mtu kukaa katika nyumba hizo.

Wakizungumza na vyombo vya habari jana jijini Dar es Salaam jopo la viongozi wa Chama cha Wapangaji, wameitaka NHC kuweka utaratibu wa mpangaji kuwa na kikomo cha kupanga katika nyumba hizo za taifa ili uwepo mzunguko kwa Watanzania wengine wapangaji waweze kufaidika kwa zamu kiupangaji.

“Watanzania wengi wamekuwa wakiushangaa utaratibu wa NHC wa kuwa na wapangaji wale wale miaka yote huku wakilipa kodi ndogo na kuwaacha Watanzania wengine wakiendelea kuhangaika kwenye nyumba za watu binafsi wakilipa kodi kubwa tena kwa mwaka mzima. Tunalishauri shirika hilo kuwa na muda wa upangaji wa kikomo ili kuwapa nafasi Watanzania wengine kufaidi rasilimali hizi za taifa zima,” alisema mmoja wa viongozi wa chama hicho.

Aidha walisema suala la kuuza nyumba za NHC zilizo katikati ya jiji na hasa maeneo ya Upanga kwa watu wachache wenye fedha ambao hutumia fedha zao kwa shinikizo linapaswa kuachwa mara moja. Hata hivyo walisema kwa kuwa idadi ya wapangaji Tanzania ni kubwa suala la makazi salama na gharama nafuu halina budi kufanywa ni haki ya kila Mtanzania na pia kuingizwa kwenye mchakato wa Katiba Mpya.

Pamoja na hayo wameitaka serikali kuhakikisha inawatetea wapangaji wote nchini na kuacha kutetea wapangaji wa NHC ambao ni asilimia 0.4 tu ya idadi ya wapangaji Tanzania. Asilimia 99.6 ambao ndiyo hupanga kwenye nyumba binafsi hawana mtetezi na ndiyo ambao hulipishwa gharama kubwa huku wakitakiwa kutoa kodi kwa mwaka mzima, jambo ambalo huwaumiza wengi.

“Sisi tunadhani iwepo Sera ya Nyumba ya Taifa ili kusaidia kutoa mwongozo wa mwenendo wa masuala ya upangaji nchini na kuboresha hali ya upangaji. Sera hiyo itatoa tafsiri sahihi ya haki ya mpangaji na mwenye nyumba. Kuwepo kwa sera hiyo ndiyo kutakao ondoa manyanyaso anayopata mpangaji ikiwemo kulipa kodi ya mwaka…,” alisema mmoja wa wajumbe hao.