Usafiri wa Treni Dar es Salaam Wanza Rasmi Leo, Dk. Mwakyembe Azindua

Treni ya abiria iliyoanza kazi leo Dar es Salaam ikiwa kituo cha Ubungo Maziwa


Baadhi ya abiria wakipanda kwenye treni kituo cha Ubungo Maziwa kabla ya kuanza safari kuelekea katikati ya jiji.


Baadhi ya abiria wakikata tiketi za treni muda mfupi kabla ya kuondoka kuelekea katikati ya jiji la Dar es Salaam.


Baadhi ya wafanyakazi wa TRC wakiendelea kukatisha tiketi ndani ya treni kwa abiria wanaopandia njiani ama kutokuwa na tiketi wakati wa safari.


Hapa ni ndani ya behewa la treni kama linavyoonekana kwenye picha

Na Joachim Mushi

USAFIRI wa kutumia treni jijini Dar es Salaam kutokea eneo la Ubungo Maziwa kuelekea katikati ya Jiji la Dar es Salaam (Stesheni ya Treni) umeanza leo. Treni ya kwanza imeondoka Ubungo majira ya saa 12:00 asubuhi kuelekea katikati ya jiji, ambapo kwa mujibu wa maofisa wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) imetumia wastani wa dakika 30 kufika katikati ya jiji.

Treni ilioanza kazi leo iliyokuwa na injini mbili (vichwa vya traini) moja ikiwa imefungwa nyuma na nyingine mbele huku ikiwa na mabehewa sita, yaani matano ya abiria wa kawaida (watu wazima) na moja likiwa ni maalumu kwa ajili ya kubeba wanafunzi. Abiria mmoja ni sh. 400 kwa tripu huku wanafunzi wakitakiwa kulipa sh. 100 kwa kila mmoja.

Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe ndiye aliyezindua usafiri wa leo ambao ni wamajaribio, akiwa pamoja na viongozi waandamizi kutoka TRC, Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), TAZARA pamoja na Polisi Kitengo cha Reli. Treni hiyo pia imezinduliwa pamoja na treni ya TAZARA ambayo itafanya kazi kama ya Ubungo, lakini yenyewe ikianzia eneo la TAZARA kuelekea Mwakanga.

Kwa utulivu na usafiri wa starehe kama hivi kwanini usisome gazeti ukiwa safarini..! Abiria akijisomea gazeti ndani ya treni leo kama alivyonaswa na mpigapicha.


Akizungumza mara baada ya ufunguzi huo Waziri Mwakyembe alisema atahakikisha treni hiyo inaendelea kufanya kazi ili kuwasaidia kiusafiri wananchi wa Dar es Salaam ambao wamekuwa wakisumbuliwa na kero ya usafiri hasa kwa foleni, ambapo utumia muda mrefu njiani kuingia na kutoka jijini.

Alisema jumla ya mabehewa ya treni 14 pamoja na injini mbili zimekarabatiwa na mafundi wazalendo nchini, ambayo ndiyo yatakayokuwa yakifanya kazi ya kusafirisha abiria kuingia na kutoka jijini kila asubuhi na jioni. Alisema kwa sasa inafanya treni moja kwa majaribio lakini baada ya uzinduzi mkubwa zitafanya kazi treni mbili, na zitakuwa zikipishana njiani moja ikirudi na nyingine ikienda.

Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe (katikati anayepunga mkono dirishani) akiwa na baadhi ya viongozi walioshiriki katika uzinduzi wa treni leo.


Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe (aliyesimama) akizungumza kwenye hafka fupi ya uzinduzi mdogo wa treni ya abiria jijini Dar es Salaam leo. Wengine ni baadhi ya viongozi walioshiriki katika uzinduzi huo.


Akifafanua zaidi alisema kitendo cha mafundi wazalendo kufanya ukarabati kwa mabehewa na injini kimeokoa kiasi kikubwa cha fedha za umma kwani ukarabati wote umetumia sh. bilioni 2.1 tu, ilhali kama Serikali ingelazimika kukodi injini gharama ingekuwa kubwa zaidi kwani bei ya kukodi injini moja ya treni ni sh. milioni moja kwa siku.

Hata hivyoDk. Mwakyembe amewataka Watanzania hasa abiria kuwa wavumilivu kwa upungufu utakaojitokeza kwa safari za mwanzo kwani bado wanaendelea kufanya marekebisho kadhaa, lakini baada ya muda mambo yatakaa sawa. Mwandishi wa habari hizi alikuwa ni mmoja wa wasafiri walioizindua treni hiyo leo.

Awali akizungumza mmoja wa viongozi waandamizi wa TRC, alisema treni hiyo itafanya kazi kila siku isipokuwa kwa siku za jumapili na siku kuu na itaanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa sita mchana na kupumzika hadi saa 9:00 za jioni, itakapoendelea tena na safari zake hadi majira ya saa nne usiku.

Uchunguzi uliofanywa na muandishi wa habari hizi umebaini kuwa behewa moja la treni linauwezo wa kuchukua abiria 66 wakiwa wamekaa, lina milango minne, feni, taa, muziki/redio, pamoja na mikanda maalumu ya kujishikia kwa abiria ambao watakuwa wamesimama.

Aidha mabehewa yote yana madirisha ya kutosha kuingiza na kutoa hewa ya kutosha. Treni ilioanza kazi leo, ikitokea Ubungo ilikuwa ikisimama vituo vya eneo la Mwananchi (relini), Tabata Relini, Buguruni Miamani, Tazara, Kariakoo Gerezani (Kamata), na mwisho Kituo Kikuu cha Treni kilichopo jirani na Kituo cha Polisi Kati (Katikati ya Jiji).