SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linapenda kuwataarifu kuwa Ofisa Habari wake, Boniface Wambura ameteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika (CAF) kuwa mmoja wa maofisa watakaoshughulikia masuala ya habari wakati wa fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake zitakazofanyika nchini Equatorial Guinea.
Uteuzi huo umefanywa na Rais wa CAF, Issa Hayatou kwa ajili ya kufanikisha uendeshaji wa fainali hizo za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake zilizopangwa kuanza Oktoba 28, 2012 na kumalizika Novemba 11, 2012.
Wambura atakuwa mmoja wa maofisa watatu watakaoshughulikia habari kwenye fainali hizo. Wengine ni ofisa kutoka makao makuu ya CAF, Mahmoud Garga na Arlindo Macedo kutoka Angola. Wambura atakuwa ni Mtanzania pekee kwenye Kamati ya Maandalizi ya fainali hizo, kitu ambacho TFF inajivunia kutoa mwakilishi kwenye moja ya mashindano makubwa ya mpira wa miguu Tanzania. Rais wa TFF, Leodegar Tenga ameelezea uteuzi huyo kuwa ni matokeo ya kazi nzuri ambayo Wambura amekuwa akiifanya tangu ajiunge na Shirikisho hilo Januari mwaka 2011.
“Taarifa zake mbalimbali zimeifanya Tanzania iwe inang’ara CAF na hata FIFA kwa kuwa kwa sasa wanajua kila kinachoendelea kwenye soka la Tanzania,” alisema Rais Tenga na kumtakia Wambura kila la kheri kwenye kazi hiyo atakayoifanya kwa takriban siku 14.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, akizungumza kwa niaba ya Sekretarieti, amemtakia Wambura kazi njema na kwamba awe kioo cha mabadiliko makubwa yanayoendelea kwenye soka la Tanzania. Wambura alijiunga na TFF Januari, 2011 akiwa mmoja wa waajiriwa watatu wapya kwenye Shirikisho baada ya watendaji wengine wawili kumaliza muda wao wa mikataba.
Wambura ni mwandishi wa habari mwandamizi ambaye ameshafanya kazi kwenye vyombo mbalimbali kuanzia kazi ya uandishi hadi Mhariri Mtendaji wa gazeti la Jambo Leo ambalo alikuwa akifanya kazi kabla ya kujiunga na TFF.