Na Mwandishi Wetu
SHIRIKISHO la Ngumi la Kimataifa (IBF) Barani Afrika, Mashariki ya Kati, Ghuba ya Uarabu na Uajemi limewataka Watanzania kujitokeze kwa wingi kumshangilia bondia Francis Cheka katika mpambano wake na Benjamin Simon wa Ujerumani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Rais wa TPBC, Onesmo Ngowi mpambamo huo utafanyika Novemba 18, 2012 katika Ukumbi wa Universal jijini Berlin nchini Ujerumani utawakutanisha miamba miwili iliyosheheni kila aina ya ujuzi wa kupigana.
Aliwaomba Watanzania kuwa na tabia ya kuwaenzi wenzao wanapowakilisha taifa hili kama wenzetu wa nchi nyingine kama Kenya na Uganda wanavyofanya. Mbali na watanzania watakaokwenda wakifuatana na Francis Cheka tokea nyumbani, pia watanzania wanaoishi nchini Ujerumani na nchi nyingine za Ulaya kama Uingereza, nchi za Skandinavia, Ufaransa, Uholanzi, Hungary na nyingine wanaombwa kujitokeza kwa wingi ili waweze kumshangilia Mtanzania mwezao aweze kupeperusha bendera ya nchi yetu vizuri.
Tayari mtangazaji maarufu wa ITV na Radio One “Maulid Baraka wa Kitenge” pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Jambo Concept inayomiliki magazeti ya Jambo Leo, City Sports Lounge, Jambo Magazine Brand Tanzania, Juma Abbas Pinto ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) wameonesha nia ya kwenda nchini Ujerumani kulitangaza pambano hilo kwenye vyombo vyao vya habari pamoja na kumshangilia Francis Cheka.
Aidha aliishauri Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) inahamasishwa pia itumie nafasi hii kuitangaza nchi yetu huko Ulaya kama zinavyofanya bodi nyingine kama za Kenya, Botswana, Uganda, Oman na nyinginezo zinazotumia wanamichezo wake kutangaza vivutio vya kitalii nchini mwao. “Tunaishauri Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) izitumie nafasi ambazo watanzania wanawakilisha nchi ili kutangaza vivutio vyake vya katalii,” alisema Onesmo Ngowi.