M23 Yabadilisha Jina la Jeshi Lake

Kundi la waasi la M23 katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, linaloshutumiwa kuzusha vurugu mashariki mwa nchi hiyo, limesema limebadili jina la tawi lake la kijeshi na linajiandaa kuzima mashambulio mapya dhidi yake.

Kwa mujibu wa Kiongozi wa kundi hilo Jean-marie Runiga, sasa tawi la kijeshi la kundi hilo litajulikana kama Jeshi la Kimapinduzi la Kongo (ARC). Katika mahojiano na mwandishi wetu wa Goma, Runiga pia amesema kamanda wa jeshi hilo Kanali Makenga Sultani amepandishwa cheo kuwa Jenerali.

Jumuiya za haki za binaadamu zinalishutumu kundi la M23 kwa kuwabaka wanawake na wasichana pamoja na kufanya mauaji wakati likipigana na jeshi la serikali. M23 iliundwa mwezi Mei na wapiganaji wa zamani katika kundi la waasi wa Kitutsi ambao walijumuishwa katika jeshi la taifa, kutokana na mkataba wa amani wa 2008. Waasi hao wanadai matakwa yao hayakutekelezwa.

Hofu ya kuzuka kwa mapigano mapya
Machafuko mapya mashariki mwa Kongo yamewafanya raia wengi kuyahama makaazi yao Machafuko mapya mashariki mwa Kongo yamewafanya raia wengi kuyahama makaazi yao

Hatua hiyo ya waasi wa M23 hata hivyo imekuja siku moja baada ya Kiongozi wake Runiga kusema kwamba huenda mapigano yakaanza tena karibuni ikiwa serikali itakataa kuzungumza na kundi hilo.

Nchi jirani ya Rwanda imekuwa ikishutumiwa kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 , shutuma ambazo viongozi wa Rwanda wamezikanusha vikali.

Kwa upande mwingine baada ya ripoti ya tume ya wataalamu wa Umoja wa mataifa kumhusisha moja kwa moja waziri wa ulinzi wa Rwanda Jenerali James Kabarebe kuwa ndiye mwenye kuliamrisha kundi hilo , hivi karibuni ripoti nyingine ya Umoja huo ikaitaja pia Uganda.

Ripoti yake ilisema maafisa wa ngazi ya juu wa Uganda wameipa M23 wanajeshi na silaha pamoja na msaada wa kiufundi. Ripoti hiyo pia imeituhumu Uganda kutoa ushauri wa kisiasa kwa kundi hilo na kulirahisishia mahusiano ya kigeni.

Uganda imekanusha kuhusika na harakati za M23. Karibu watu laki tano wamelazimika kuyahama makaazi yao kwa sababu ya harakati za kijeshi za waasi hao, mashariki mwa Kongo.

Mwandishi: Mohammed Abdulrahman