Kiongozi wa Uamsho, Sheikh Farid Hadi Kufikishwa Mahakamani Leo

Kiongozi wa Kikundi cha Uamsho cha Mjini Zanzibar, Sheikh Farid Hadi Ahmed

Na Mwandishi Wetu

KIONGOZI wa Kikundi cha Uamsho cha Mjini Zanzibar, Sheikh Farid Hadi Ahmed anatarajiwa kufikishwa mahakamani leo mjini Zanzibar kujibu mashtaka mbalimbali yanayomkabili, ikiwa ni siku chache baada ya kupatikana huku akidai alikuwa ametekwa na watu wasiojulikana (yeye anahisi ni watu wa usalama).

Kwa mujibu wa taarifa ambazo mtandao huu umezipata kutoka ndani ya Jeshi la Polisi Zanzibar, Sheikh Farid Ahmed atafikishwa mahakamani na wenzake sita ambao walikamatwa na Polisi wakihusika kwa makosa mbalimbali yakiwemo ya vurugu zinazodaiwa kufanywa na kundi la Uamsho.

Tayari Jeshi la Polisi Zanzibar linawashikilia Sheikh Farid Ahmed pamoja na watuhumiwa kadhaa ambao wote huenda watafikishwa mahakamani. Hata hivyo Polisi haijaweka wazi makosa ambayo wahusika watahusika nayo moja kwa moja, japokuwa wachambuzi wa masuala ya jamii wanasema makosa ambayo huenda wanaoshikiliwa watatuhumiwa nayo ni pamoja na vurugu, zilizoibuka hivi karibuni mjini Zanzibar ambazo zilileta madhara makubwa, ikiwemo kifo cha askari mmoja (aliyeuwawa) siku moja baada ya vurugu hizo.

Taarifa zaidi zinasema Jeshi la Polisi zanzibar limejipanga kikamilifu kudhibiti vurugu zozote ambazo zinatarajia kujitokeza, endapo wafuasi wa uamsho watapinga kitendo cha Farid kushikiliwa na hatimaye kufikishwa mahakamani hii leo.

Wakati huo huo; taarifa kutoka Polisi jijini Dar es Salaam zinasema watu wanaoshikiliwa kwa makosa mbalimbali ikiwemo kufanya vurugu na kutaka kuandamana bila kibali wanatarajiwa kufikishwa mahakamani muda wowote baada ya uandaaji wa mashtaka yao kukamilika. Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inawashikilia watu kadhaa ambao walikamatwa Ijumaa ya wiki iliyopita wakitaka kuandamana kwa nguvu baada ya kuzuiwa kufanya hivyo.