Silaha za Wapiganaji wa Al Shabaab Zanaswa Puntland

Wapiganaji wa kundi la Al-Shabaab

SHEHENA kubwa ya silaha ambazo zilikuwa zinapelekwa nchini Somalia, zimekamatwa katika Jimbo la Puntland. Kwa mujibu wa Gavana mmoja wa jimbo hilo, Abdisamad Gallan alisema boti iliyokuwa inatoka nchini Yemen ilinaswa ikiwa imebeba mabomu ya kutega ardhini na zana zingine za kivita.

Taarifa zaidi kutoka Somalia Abdisamad Gallan zinasema kuwa hii ni mojawapo ya shehena kubwa kuwahi kunaswa ikiwa na silaha zilizokuwa zinapelekewa wapiganaji wa Al Shabaab. Silaha hizo zilinaswa baada ya polisi kupashwa habari na wenyeji wa mji wa Pwani wa Qandala, katika jimbo la Puntland.

Al-Shabab inasema kuwa inataka kukuza mizizi yake katika jimbo hilo la Puntland. Kundi hilo lenye uhusiano na al-Qaeda, wakati mmoja lilikuwa limekita mizizi Kusini mwa Somalia na katika maeneo ya kati, lakini sasa wameondolewa kutoka miji hiyo. Hata hivyo kundi hilo bado linadhibiti sehemu kadhaa za vijijini, Somalia.

Bwana Gallan, alisema kuwa wanaamini silaha hizo zilitoka Yemen. Watu waliokuwa kwenye boti walitoroka kabla ya kuhojiwa na polisi lakini wenyeji wa Qandala walisema kuwa walikuwa wenye asili ya kigeni. Mapema wiki hii Mtandao mmoja wa Al-Shabab, Amiirnuur, ulitangaza kuwa wapiganaji wake wanataka kueneza haratakati zao katika jimbo la Puntland na kwamba wanataka kuonesha watu wa jimbo hilo ukweli wa dini ya Kiisilamu.
-BBC