Yanga na Ruvu Shooting Kucheza Uwanya wa Taifa, Viingilio Vyatajwa

Uwanja wa Taifa wa Jijini Dar es Salaam


*Mtanzania Aombewa ITC Marekani

Na Mwandishi Wetu

MCHEZO wa Ligi Kuu ya Vodacom kuwania ubingwa wa Tanzania Bara kati ya Yanga na Ruvu Shooting uliopangwa kuchezwa Oktoba 20 mwaka huu Uwanja wa Chamazi sasa umehamishiwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10.15 jioni.

Mabadiliko hayo yamefanyika kutokana na maombi ya timu hizo mbili kutaka mechi ichezwe Uwanja wa Taifa kutokana na sababu mbalimbali ambazo zimeridhiwa na Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ikiwemo siku hiyo uwanja huo kutokuwa na mechi.

Viingilio katika mechi hiyo itakayokuwa chini ya mwamuzi Amon Paul kutoka Mara ni sh. 5,000 viti vya kijani na bluu, sh. 8,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 VIP B na C na sh. 20,000 kwa VIP A. Pia Kamati ya Ligi imekataa ombi la timu ya Azam kutaka mechi zake za nyumbani za ligi hiyo zichezwe dhidi ya Simba na Yanga zichezwe Uwanja wa Chamazi kutokana na sababu za kiusalama.

Nayo Coastal Union itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar katika mechi nyingine ya ligi hiyo itakayochezwa Oktoba 20 mwaka huu katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Mchezo huo namba 56 wa kukamilisha raundi ya nane utachezeshwa na mwamuzi Israel Nkongo atakayesaidiwa na Hamis Chang’walu na Omari Kambangwa, wote kutoka Dar es Salaam.

Ligi hiyo itaendelea tena Jumapili ya Oktoba 21 mwaka huu kwa mechi tatu. JKT Ruvu itaoneshana kazi na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Chamazi, Mgambo Shooting itaikaribisha Simba kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga wakati Tanzania Prisons na Toto Africans zitapimana ubavu kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

Vile vile; Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) chini ya Mwenyekiti wake Ombeni Zavala imewataka wanachama wa TWFA ambao ni mikoa ya Tanzania Bara kuwasilisha orodha ya wajumbe wao wa mkutano wa uchaguzi. Wajumbe wenye sifa ya kuhudhuria Mkutano wa TWFA ni kutoka vyama vya mikoa ambavyo tayari vimefanya uchaguzi. Wajumbe hao ni Mwenyekiti, Katibu na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TWFA.

Mikoa ambayo imeshafanya uchaguzi mpaka sasa ni Iringa, Kigoma, Mwanza, Pwani na Tanga. Mikoa ambayo bado inahimizwa kufanya uchaguzi, na mwisho wa kutuma majina ya wajumbe kwa Mwenyekiti Zavala ni Oktoba 25 mwaka huu. Mkoa ambao utakuwa haujafanya uchaguzi utakuwa umenyimwa haki ya kushiriki uchaguzi wa TWFA utakaofanyika Novemba 4 mwaka huu.

Wakati huo huo; Mchezaji Millan Mbise kutoka Tanzania ameombewa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) itakayomwezesha kucheza mpira wa miguu nchini Marekani.

Shirikisho la Mpira wa Miguu la Marekani (USSF) limemuombea hati hiyo Mbise kama mchezaji wa ridhaa ili ajiunge na timu ya Virginia Youth Soccer. Klabu ya zamani ya Mbise aliyezaliwa Agosti 18, 1994 imetajwa kuwa Super Sport FC, na mechi ya mwisho kwenye timu hiyo alicheza Novemba 15 mwaka juzi.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linafanya mawasiliano na pande husika kabla ya kutoa hati hiyo kwa mchezaji huyo kama ilivyoombwa na shirikisho hilo la Marekani.

Wakati huo huo; Chama cha Madaktari wa Tiba ya Michezo Tanzania (TASMA) Oktoba 19 mwaka huu kimetangaza kuanza mchakato wa uchaguzi wa chama hicho uliopangwa kufanyika Novemba 28 mwaka huu. Kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TASMA, Dk. Francis Mchomvu, fomu kwa wanamichezo wanaotaka kugombea uongozi wa chama hicho zitaanza kutolewa Oktoba 21 mwaka huu.

Mwisho wa kuchukua na kurejesha fomu hizo zinazopatikana ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ni saa 10.00 alasiri ya Oktoba 26 mwaka huu. Ada ya fomu kwa nafasi nne za juu ni sh. 200,000 wakati kwa nafasi nyingine zilizobaki ni sh. 100,000. Kati ya Oktoba 27-31 mwaka huu Kamati ya Uchaguzi ya TASMA itapitia fomu na kutangaza majina ya waliojitokeza kuomba uongozi.

Nafasi zitakazogombewa ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Katibu Msaidizi, Mhazini, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF na wajumbe wawili wa Kamati ya Utendaji. Kipindi cha pingamizi kwa waombaji ni kuanzia Novemba 1-6 mwaka huu, na pingamizi zinatakiwa kuwasilishwa kwa Katibu wa Kamati ya Uchaguzi ya TASMA kabla ya saa 10.00 alasiri ya Novemba 6 mwaka huu. Hakuna ada kwenye pingamizi.

Pingamizi zitajadiliwa na kufanyiwa uamuzi kati ya Novemba 7-9 mwaka huu. Usaili utafanyika kati ya Novemba 10-11 mwaka huu ambapo matokeo ya usaili huo vilevile yatatangazwa ili kutoa fursa kwa rufani ambazo zinatakiwa kukatwa kati ya Novemba 11-13 mwaka huu. Rufani ambazo zinaambatana na ada y ash. 500,000 zinatakiwa kufikishwa kwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kabla ya saa 10.00 alasiri ya Novemba 13 mwaka huu.