Kashfa Yaibuka NHC, Bilioni 25 Zatumika Nje ya Utaratibu

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyumba Tanzania, Nehemiah Mchechu

Na Magreth Kinabo- MAELEZO

KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), imelionya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuacha mtindo wa kutumia fedha pasipo kufuata Sheria ya Manunuzi ya Umma (PPRA) katika utekelezaji wa shughuli zake. Kamati hiyo ya Bunge inayosimamia hesabu za mashirika ya Umma imelazimika kulionya shirika hilo baada ya kutumia kiasi cha sh. bilioni 25 nje ya utaratibu wa PPRA.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti wa POAC, Kabwe Zitto wakati kamati yake ilipokutana na baadhi ya viongozi wa NHC kuzungumzia utendaji wa shirika hilo kwenye ukumbi wa Ofisi Ndogo ya Bunge jijini Dar es Salaam.

Katika taarifa yake POAC ilibainisha kuwa NHC kwa mwaka wa fedha 2010/2011 mbali na kupanga kutumia sh. bilioni 31 katika shughuli zake, sh. bilioni 25 zimebainika kutumika nje ya taratibu za PPRA kitendo ambacho ni kinyume cha utaratibu kwa mashirika ya umma.

Akijitetea kufuatia tuhuma hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyumba Tanzania, Nehemiah Mchechu alisema suala hilo limetokana na kuwepo kwa miradi ya dharura iliyoangalia masuala ya kibiashara zaidi. Hata hivyo amekiri kuwa eneo hilo ni moja ya changamoto wanayokabiliana nayo, hivyo wameshaanza kuifanyia kazi wakishirikiana na PPRA.

Kamati hiyo pia imelitaka shirika hilo, kuwakilisha matumizi ya fedha ya mwaka huu unaoishia Juni, 2012 kwa kuonesha mchanganuo sahihi kabla kikao kijacho na kubadilisha mfumo wa utaratibu wa malipo ya fedha taslimu, badala yake watumie benki ili kulinda mapato ya shirika.

Licha ya kuwepo kwa kasoro hizo, Mwenyekiti wa Kamati POAC, Zotto alilipongeza shirika hilo kwa kujiendesha kifaida kutoka sh. bilioni tatu hadi kufikia sh. bilioni sita na thamani ya mali za shirika hilo kwa sasa imefikia sh. trilioni 1.75.

Zitto aliongeza kuwa shirika hilo linatakiwa kuendelea mchakato wa kujiendesha kama kampuni ili liweze kupata mtaji wa kutosha. Kamati hiyo ilitaka shirika hilo, kuzingatia mpango wa kujenga nyumba zenye gharama nafuu kwa watu wenye kipato cha chini hususan maeneo ya vijijini.