Tanzania Kushiriki Maadhimisho ya Miaka 67 ya Umoja wa Mataifa

Pichani ni Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania Dk. Alberic Kacou akizungumza machache kuhusiana na umuhimu wa wiki ya Umoja wa Mataifa inayoanza leo, ambapo amesema mabadiliko ya hali ya hewa yanayotokea duniani ni ushahidi wa kutosha wa ongezeko la mafuriko na ukame kunakotokana na uharibifu wa mazingira mambo ambayo tunapaswa kuyachukulia kama changamoto kwa kuwa yanatukwaza katika kutimiza malengo ya Maendeleo ya Milenia.
Ameongeza kuwa Wiki ya Umoja wa Mataifa kwa mwaka 2012 inaadhimishwa kwa shughuli mbalimbali zinazolenga vijana, wanafunzi, wasomi, vyombo vya habari na jamii kwa ujumla.

Na Mwandishi Wetu

TANZANIA inaungana na nchi nyingine mbalimbali duniani kuadhimisha miaka 67 ya Umoja wa Mataifa ambapo kutakuwa na shughuli anuai zinazoanza leo Oktoba 17 hadi 24, 2012 ambayo ndio siku ya kilele cha shughuli hizo.

Kitaifa nchini Tanzania miaka 67 ya Umoja wa Mataifa itaadhimishwa kwa kauli mbiu ambazo zimekuwa zikitoka kila mwaka na kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Changing Peoples’ Lives: Greening The Environment For Sustainable Livelihoods’.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, John Haule amesema kauli mbiu hiyo imekuja wakati muafaka ili kutukumbusha mahusiano yetu ndani ya Jumuiya ya Umoja wa Mataifa lakini vilevile inatukumbusha changamoto ya jinsi uharibifu wa mazingira unavyofanyika hivi sasa.

Ameongeza kuwa wiki ya maadhimisho ya miaka 67 ya Umoja wa Mataifa itaadhimishwa na matukio mbalimbali ikiwemo uzinduzi wa leo, na Siku ya Familia itakayohusisha michezo mbalimbali itakayofanyika kwenye viwanja wa Leaders Club Oktoba 20, 2012.

Michezo hiyo itawahusisha wanadiplomasia waliopo nchini Tanzania, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje.