Mchezo wa Ngumi Unavyopeteza Uasili Wake (Sehemu 15)

Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC), Onesmo Ngowi

Na Onesmo Ngowi

MASUMBWI au kwa majina mwengine ndondi au ngumi na kwa majina ya mitaani ndogwa, mawe n.k. ni mchezo unapoendwa sana na watu wengi. Aidha mchezo huu ni kati ya michezo inayoogopwa sana duniani. Mchezo wa ngumi uko hatarini kupoteza maana yake ya asili yaani kucheza kama burudani, kuwakilisha nchi na kujenga ushupavu wa mchezaji. Mamilioni ya watu wanaojazana kuutazama wasingependa kabisa kujiingiza kuucheza mchezo wa ngumi. Sasa endelea….!

MARVING HAGLER VS THOMAS HEARNS

Historia ya ngumi inatuonyesha jinsi mchezo huu ulivyopitia katika misukosuko mingi hadi kutambuliwa na kukubaliwa na jamii kama thana ya kutafuta kipato kwa wadau wake!

Hii inatokana na ukweli kwamba ngumi tangu zianze kwenye karne nyingi zilizopita zilipitia katika hatua mbalmbali ikiwa ni pamoja na kutumika kama kamari, ulingo wa kutoleana nishai, kujenga ushupavu na hata kupata wawakilishi wa nchi katika medani ya kimataifa. Yote haya yanadhihirisha jinsi mchezo huu ulivyopitia katika misukosko na mikiki mingi.

Wayunani (Wagiriki) na Wazumi (Waitaliano) walijenga misingi imara ya mchezo huu na hata kuufanya kuwa kati ya michezo iliyopendwa sana duniani. Katika karne ya ishirini hususan wakati dunia ikijiandaa kuingia kwenye karne ya ishirini na moja, ngumi zilishakuwa kivutio cha hali ya juu kwenye medani ya ndani ya nchi na kimataifa. Kukua kwa hatua endelevu za mchezo huu kunatokana na uhalali wa mchezo wenyewe.

Ngumi zikiwa ni kati ya michezo ya zamani sana duniani kama michezo ya Kung Fu, Karate na Mieleka zinatumika hadi leo kama kipimo cha kupima ushupavu wa mchezaji wake!

Katika makala zilitangulia tumeona jinsi mabondia maarufu duniani wakati huo kama kila Jack Jonson, Jack Dempsey, Sugar Ray Robinson na wengine wengi walivyoweza kuleta msisimko mkubwa katika mchezo wa ngumi na hata kujijengea umaarufu mkuwa katika jamii.

Mwishoni mwa karne ya ishirini ngumi hususan mapambano yaliyokuwa yana washirikisha mabondia wa uzito mwepesi hadi uzito wa kati (Ligtweight hadi Middleweight) yalileta msisimko mkubwa sana kutokana na kasi iliyokuwa inatumiwa na mabondia wengi katika kuyarusha pamoja na madaha ya uchezaji.

Mabondia wengi walikuwa wakipewa majina yanayoendana na ushupavu wao katika ulingo. Kama ilivyo kwenye michezo mingine kama vile mpira wa miguu wapiganaji wengi walipewa majina ya mabondai maarufu duniani.

Tunaona jinsi bondia kama Ray Charles Leonard alivyojipa jina la Sugar Ray kwa ajili ya kuvutiwa na bondia maarufu aliyemtangulia Sugar Ray Robinson. Sio hapa kwetu tu ambako wanamichezo wengi wanajiita majina ya wenzao wanaocheza michezo hiyo na waliokwisha kuwa au walio maarufu duniani.

Hapa kwetu wanamichezo wengi wanajiiita majina makubwa makubwa kwa ajili ya kujipatia umaarufu wa haraka haraka au kuwatisha wapinzani wao katika mchezo husika. Wako baadhi ya mabondia wanaojiita majina kama Marvin Hagler, Sugar Ray, Tyson, Thomas Hearns, Muhammad Ali na Smokin Joe!

Haya yote yanadhihirisha jinsi mabondia hao wa kigeni walivyoweza kuwavutia mabondia wa nchi mbalimbali kwa uchapaji wao wa makonde na kuweza kujibambikizia majina yao. Kama majina ya watu yangelikuwa na hati miliki basi kuna mabondia wengi ambao wangekuwa wanaishi tu kwa kulipwa fedha za matumiazi ya majina yao. Baadhi ya mabondia hao ni Marvelous Marvin Hagler na Thomas Hearns!

Moja ya mapambano ya ngumi yaliyowahi kuwavutia watu wengi katika karne ya ishirni na hasa miaka ya 70 na 80 ni kati ya mabondia Marvelous Marvin Hagler na Thomas Hearns”

MARVING HAGLER ambaye baada ya kucheza ngumi kwa mua mrefu akiwacharanga mabondia wenzake bila ya kupewa heshima aliyostahiki alitokea katika mji wa Brockton kwenye jimbo la Massachusetts nchini Marekani. Baada ya kuwadhihirishia wadau wengi wa ngumi kwamba yeye kweli alikuwa ni moto wa kuotea mbali alipewa jina la Marvelous kuashiria umaridadi wake wa kuwachapa wapinzani wake bila ya huruma!

Hagler alikuwa bondia wa uzito wa kati yaani Middle kwa miaka mingi na aliweza kuitawala namba moja katika uzito huo kwa miaka mingi. Mabondia wengi wapinzani na mabingwa katika uzito huo walikuwa wanamuogopa. Kama ilivyo kawaida kwenye ngumi mameneja wengi waliokuwa na mabondia mabingwa katika uzito wa kati waliwakinga mabondia wao dhidi ya kupambana na Hagler!

Ikumbuwe kwamba ngumi ni kati ya michezo inayomuingizia bondia aliye na jina kubwa hususan bingwa wa uzito fulani fedha nyingi sana. Ni katika karne ya ishirini pekee ambapo mabondia wengi ambao hawakuwa mabingwa waliweza kujizolea vitita vya fedha lukuki. Bondia Marvin Hagler alikuwa mmoja wa mabondia hao!

Kutokana na ushupavu na ukali wa Hagler alilazimika mara nyingi kusafiri umbali mkubwa kutoka katika mji wake wa Brockton kwa ajili ya kukutana na mabondia waliodhaniwa kuwa wakali.

Hii yote ilikuwa katika jitihada zake za kupanda chati na kuweza kujipatia fedha za maisha. Hagler aliichukulia hali hii kama majaribio katika maisha yake na aliifurahia kwa jinsi alivyoweza kuzidi kuwadhihirishia watu wengi kwamba yeye kweli alikuwa moto wa kuotea mbali kwa kuendeleza kibano chake kwa wapinzani wake!

Moja ya mapambano ambayo Hagler alikumbana nayo mwanzoni mwa harakati zake za kuusaka umaarufu yalikuwa kati yake na mabondia maarufu wa jimbo la Philadelphia. Hata hivyo aliwahi kupewa kibano na mabondia Willie Monroe and Bobby ‘Boogaloo’ Watts. Hii ilimyima nafasi ya kupambana na mabondia waliouwa kwenye chati kama Carlos Monzon na Hugo Corro.

Wanazuoni wengi wa masuala ya masumbwi wanakiri kwamba mapambano haya pamoja na ukweli kwamba Hagler alinyimwa haki ya msingi ya kupambana na mabondia waliokuwa kwenye chati wakati huo yalimfanya ajenge tabia ya kuwa bondia aliyekuwa mkali ulingoni na asiyekuwa na masihara. Tabia hii ilimfanya Hagler awe jambia la uzito wa kati kwa jinsi alivyokuwa anawafyeka wapinzani wake!

Hagler alidhihirisha hali hii wakati aliporudisha vibano vya uhakika kwa mabondia waliowahi kumwadhiri Monroe na Watts. Aliweza kabisa kuwadhihirishia mashabiki wake kwamba yeye alikuwa Simba wa Yuda na kuwatahadharisha mabondia wengine katika uzito wa kati kuwa wakae chonjo kwani kweli wakati wa masihara ulikuwa umekwisha!

Aliendeleza kibano kwa kumnyuka vilivyo bondia Bennie Briscoe katika mpambano uliofanyika kwenye jimbo la Philadelphia na kijizolea sifa kemkem kwenye majimbo haya mawili ya Philadelphia na Massachussetts! Umaarufu huu ulimjengea sifa nyingi na hivyo moja wa mapromota maarufu wa ngumi duniani Bob Arum aliingia mkataba naye!

Mkataba wake na Bob Arum ulimpa nafasi ya kukutana na bingawa wa dunia katika uzito wa kati mwako 1979 bondia Vito Antuofermo. Mpambano huo ulizidi kuongeza wasiwasi wa Hagler wa kukubalika kama kinara wa uzito wa kati baada ya kutoka sare na Antuofermo! Japokuwa wengi wa wadau wa mchezo huo wanakiri huo kweli ulikuwa mpambano wa kukata na shoka lakini ulizidi kuongeza wasiwasi kwa Hagler!

Baada ya bondia Antuofermo kupoteza ubingwa wake kwa Mwiingereza Alan Minter, Hagler alipata tena nafasi nyingine ya kujaribu bahati yake ambapo aliazimika kusafiri hadi London ili kupambana na Minter kwenye ubingwa wa dunia!
Mbabe Thomas Hearns akimwadhibu Marvin Hagler katika koja ya mapambano yao

Mpambano huo ulifanyika katika ukumbi maarufu wa Wembley arena na ulichukua raundi tatu tu baada ya Hagler kumshushia kipigo kitakatifu Alan Minter na kuufanya umati wa mashabiki wengi wa kiingereza waliohudhuria kuanza kurusha chupa na kuleta ghasia kubwa. Juhudi kubwa za police wa kiingereza zilitumika kuwalinda Hagler na kocha wake mpaka wakaweza kuingia kwenye chumba cha kujitayarisha na hivyo kuepuka ghasia hizo!

Baada ya ushindi huo Hagler aliweza kuudhihirishia ulimwengu kwamba kweli yeye alikuwa ndiye kinara wa uzito huo baada ya kumshushia kipigo bondia aliyetegemewa Fulgencio Obelmejias na aliyekuwa bingwa wa zamani wa uzito huo Antuofermo kwa KO! Wote walishuhudia walipewa vibano hivyo katika ukumbi wa Boston Garden!

Bondia shupavu na aliyekuwa raia wa Siria Mustafa Hamsho aliendeleza vibano walivyopata mabondia wa uzito wa kati baada ya kunyukwa na Hagler kwenye raundi ya 11. Hamsho baadaye alikuja kumtandika bondia aliyekuja kuwa bingwa wa dunia Bobby Czyz. Mabondia kama Caveman Lee, Obelmejias, Tony Sibson na Wilford Scypion walijipanga na kuchukua vibano kwenye raundi za kwanza, tano, sita na nne.

Wakati huu Hagler alishajijengea umaarufu mkubwa katika medani ya ngumi na kuwa mgeni maarufu katika maonyesho mbalimbakli ya televisheni hususan televisheni ya kulipia inayojulikana kama Pay Per View (Lipa Uone). Ili uangalie chochote kwenye televisheni hii unalipia aidha kwa mwaka au kwa kila tukio unalotaka kuona.

Hizi ndizo nyenzo zinazoufanya mchezo wa ngumi kuwa na fedha nyingi sana katika nchi zilizoendelea. Mitandao mbalimbali ya televisheni hutoza fedha taslim watazamaji wake waotaka kuona mapambano mbalimbali kwenye televisheni hizo na hivyo kutengeneza fedha nyingi!

Baada ya ushindi mfulilizo kwa Hagler mpambano mkubwa na Roberto Duran uliandaliwa kuona ni nani kati yao aliyekuwa jogoo! Wakati huu Duran alishacheza mara mbili ya Sugar Ray Leonard katika mpambano wao wa No Mas ulioishia kwa Duran kulamba kipigo kitakatifu na kukataa kuendelea kwenye raundi ya nane akisema No Mas ( Sitaki tena )

Hagler alimchakaza Duran kwa poini kwenye mpambano wa raundi kumi na tano (15)! Hili pia lilikuwa pambano la kwanza kwa mpinzania wa Haler kumaliza pambano katika mapambano yake ya ubingwa wa dunia.

Ushindi wa mpambano huu ulizidisha sifa za Hagler na kupandishia dau alizokuwa anapata kwenye mapambano yake. Mapambano yake yalianza kuwa na bei kubwa kwenye HBO ambao ni mtandao mkubwa wa televisheni nchini Marekani unaoonyesha michezo!

Bondia Juan Roldan alikuwa bondia wa kwanza kumwangusha Hagler wakati walipokutana kwenye mpambano wao wa dunia. Roldan alimtwanga Halger konde zito kwenye raundi ya kwanza na kumpeleka chini bingwa huyo aliyejulikana kama tishio toka Massachusetts!

Lakini hiyo ilikuwa kama Roldan aliamsha mashetani ya Hagler kwani kilichofuata ni kipigo ambacho kilimfanya Roldan ashindwe kabisa kumudu mpambano wenyewe! Halger aliendelea kumwadhibu Roldan mpaka raundi ya kumi (10) ambapo mpambano ulisimamishwa kwa Hagler kushinda kwa KO!

Mustafa mwana wa Hamso mwarabu toka Siria alikutana na Hagler kwenye mpambano wa marudiano akijaribu kurudisha heshima ya waarabu waliyokuwa nayo kwenye ngumi. Mpambano huo uliishia kwenye raundi ya tatu (3) kwa Mustafa kupewa kipigo cha ajabu.inaendelea…!

Mwandishi wa makala haya ni; Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC), Shirkisho la Ngumi za Kulipwa Afrika Mashariki na Kati (ECAPBF), Shirikisho la Ngumi la Kimataifa bara la Afrika, Masharilki ya Kati, Ghuba ya Uarabu na Uajemi (IBF/AFRICA) na Mkurugenzi wa Baraza la Ngumi la Jumuiya ya Madola (CBC) E-mail: ibfafrica@yahoo.com