Kamanda Barlow Aagwa Mwanza, Asafirishwa Kwenda Dar

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi akiuaga mwili wa Marehemu Liberatus Barlow

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo Marehemu Liberatus Barlow

Mwili wa marehemu Kamanda Barlow ukimwagiwa maji ya baraka na Paroko wa Kanisa la Nyakahoja, Padre, Raymond Manyanga (hayupo pichani) katika ibada ya kumuombea marehemu kabla ya kusafirishwa kuelekea Dar es Salaam.

Umati ukiwa katika viwanja vya Nyamagana kumuaga Kamanda Marehemu Liberatus Barlow

Familia ya marehemu Kamanda Barlow ikiwa katika majonzi (Picha zote na http://gsengo.blogspot.com/)

MWILI wa aliyekuwa Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, Marehemu Liberatus Barlow umeagwa katika Uwanja vya Michezo wa Nyamagana, ambapo viongozi wa kada mbalimbali na wananchi kutoka wilaya zote za mkoa wa Mwanza na mikoa jirani wametoa heshima za mwisho kwa marehemu Kamanda huyo wa Polisi.

Baada ya kuagwa na viongozi mbalimbali na wananchi, mwili wa marehemu Kamanda Barlow umepelekwa kwa msafara katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza, ambapo utasafirishwa kwenda jijini Dar es Salaam nyumbani kwake.

Taarifa zinafafanua baada ya kufikishwa Dar, maofisa wa Jeshi la Polisi Makao Makuu jijini Dar es Salaam, ndugu, jamaa, marafiki na wananchi watatoa heshima za mwisho kwa marehemu Kamanda Barlow, kisha mwili utasafirishwa kwenda mkoani Kilimanjaro, Marangu kwa mazishi.

Miongoni mwa viongozi mashughuli walioshiriki kuuaga mwili wa kamanda huyo leo mjini mwanza ni pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, Lawrance Masha ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa CCM, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Joseph Kasheku, Mbunge wa Rolya Lameck Airo na wabunge wengine. Pia wamehudhuria makamanda wa Jeshi la Wananchi na Maofisa mbalimbali wa Jeshi la Polisi, pamoja na wafanyabiashara anuai.