Na Anna Nkinda, Maelezo
SERIKALI imewataka wananchi kuendelea kutunza rasilimali za misitu, wanyamapori na uvuvi ili ziweze kuwa na manufaa katika maeneo yao kwa kuinua kipato na kupunguza umasikini katika jamii.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi Dk. Yohana Budeba wakati akifungua mkutano wa mwaka wa wadau wa sekta ya maliasli uliofanyika katika chuo cha Taifa cha Utalii kilichopo jijini Dar es Salaam.
Dkt. Budeba alisema kuwa katika miaka ya nyuma jukumu la kutunza misitu, wanyamapori na uvuvi lilikuwa linafanywa na Serikali kuu lakini hivi sasa jukumu hilo limepelekwa katika ngazi ya vijiji na wilaya ambapo wananchi wanashiriki moja kwa moja katika utunzaji wa rasilimali husika.
“Serikali kuu inachokifanya ni kusimamia sera na miongozo ya maliasili ikiwa ni pamoja na kulipa fidia pale ambapo wanyama watakapovamia makazi ya watu na kuleta uhalibifu”, alisema Dk. Budeba.
Alisema kuwa Serikali itandelea kujenga na kuimarisha miundombinu ili kuwezesha wadau wa maliasili kufanya kazi katika mazingira mazuri.
Aidha Dk. Budeba aliviomba vyombo vya habari kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili iweze kuona umuhimu wa kuhifadhi mazingira kwani Serikali peke yake haiwezi ni lazima kushirikiana na wananchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka wizara ya Maliasili na Utalii Pingu Korongo alisema kuwa sera ya kuwashirikisha wananchi pamoja na wadau mbalimbali wa maliasili itasaidia katika utunzaji wa mazingira.
Alisema kuwa sera ya hiyo ilikuja ili kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi ambayo yalikuwa yanakwenda moja kwa moja Serikalini jambo wanalolifanya hivi sasa ni kuangalia njia bora zaidi ya kusimamia na kuona kuwa wadau pamoja na jamii wanafanya kazi vizuri.
Naye Mwenyekiti wa Ulinzi Shirikishi wa Maeneo ya Fukwe na Bahari kutoka wilaya ya Temeke Khatibu Abdala alisema kuwa hatua zaidi zinatakiwa kuchukuliwa katika utunzaji wa mazingira. Abdala alisema kuwa tangu wameanza kushiriki katika zoezi la utunzaji wa mazingira hizi sasa fukwe za bahari ni safi na wanafanya kazi hiyo kwa kusimamiwa na Serikali ya mtaa wa Kizito Kimbiji.
Kuhusiana na watu wanaoharibu mazingira alisema kuwa wakiwamakata wanawapeleka katika uongozi wa Serikali ya mtaa ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa. Mkutano huo wa siku mbili unahudhuriwa na wadau mbalimbali wa maendeleo na sekta ya mazingira kutoka taasisi za Serikali na binafsi.