Wagombea 13 kati ya 15 waliojitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwenye Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) wamepitishwa baada ya usaili uliofanyika juzi.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TWFA, Ombeni Zavala, waliopitishwa kwenye nafasi ya uenyekiti ni Isabellah Huseein Kapera, Joan Ndaambuyo Minja na Lina Paul Kessy.
Makamu Mwenyekiti ni Rose Kisiwa wakati wanaowania nafasi ya Katibu Mkuu ni Amina Ali Karuma na Cecilia Oreste Makafu. Mgombea pekee wa nafasi ya Katibu Msaidizi, Macky Righton Mhango naye amepita kwenye usaili huo. Aliyepitishwa kwenye nafasi ya Mhazini ni Rose Stewart Msamila.
Furaha Francis na Zena Chande wamepitishwa kuwania nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wakati waliopita kuwania ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya TWFA ni Triphonia Ludovick Temba, Rahim Salum Maguza na Sophia James Charles.
Hivi mchakato wa uchaguzi wa TWFA uko katika kipindi cha kukata rufani ambapo ni kuanzia Oktoba 15-17 mwaka huu. Rufani zinatakiwa zifike kwa Katibu Mkuu wa TFF kabla ya saa 10 kamili jioni ya Oktoba 17 mwaka huu.
Wagombea wawili ambao hawakupitishwa kwa ajili ya uchaguzi huo
unaotarajiwa kufanyika Novemba 4 mwaka huu ni Julliet Mndeme na Jasmin Soud walioomba ujumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF. Wagombea hao ambao pia walikuwa wamewekewa pingamizi hawakufika kwenye usaili.
Na wakati huohuo Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika jana (Oktoba 14 mwaka huu).
Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa COREFA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia mchezo huo mkoani Pwani.
TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya COREFA chini ya uenyekiti wa Hassan Othman Hassan ambaye amechaguliwa tena kuongoza chama hicho.
Uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu mkoani Pwani kwa kuzingatia katiba ya COREFA pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yake.
Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya COREFA na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF.
Viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi huo ni Hassan Othman Hassan (Mwenyekiti), Riziki Majala (Katibu), Geofrey Irick Nyange (Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF), Juma Haruna Kisoma (Mwakilishi wa Klabu TFF) na Abubakar Allawi (Mhazini).
Waliochaguliwa kuwa Wajumbe wa Kamati ya Utendaji katika uchaguzi huo uliofanyika kisiwani Mafia ni Musa Bakari Athumani, Godfrey Magnus Haule na Gwamaka Oden Mlagila. Mwakilishi wa Wanawake ni Florence Ambonisye.