Mukama Aikamua CHADEMA

KATIBU Mkuu wa CCM, Wilson Mukama amesema Chadema hakiwezi kuwa chama chenye tija na hatma njema kwa taifa kutokana na kulazimika kuokoteza hata wagombea wake kutokana na wanaoshindwa kwenye michujo au chaguzi ndani ya CCM.

Alisema, Chadema na vyama vingine vya upinzania hapa nchini, vinazama katika hali hiyo, kutokana na kutokuwa na tanuru imara linalowawezesha kutoa viongozi waliopikika kimaadili, kama ilivyo ndani ya CCM.

Amesema, Chadema wanaposema, kwamba kwa CCM kutowafukuza au kuwanyima uongozi baadhi ya wana-CCM ni kuizika CCM, huko ni kulia kinyume kwamba kwa kutofanya hivyo CCM imewakosesha watu ambao wangehamia kwao hivyo chama chao kinakufa.

Mukama alisema hayo jana wakati wa sherehe ya kuwapongeza wana-CCM Kata ya Msasani kwa kukamilisha chaguzi zao ndani ya chama katika kata hiyo, iliyofanyika kweny6e ukumbi wa Maisha Club, Msasani jijini Dar es Salaam.

Mukama alisema, CCM ni taasisi iliyojengwa katika misingi imara na mshikamano wake ni kama ngumi inayoundwa na vidole vitano na kitaendelea kuwa imara kwa sababu viongozi wake wanatokana na tanuru lililowapika kimaadili wakapikika.

“CCM bwana ni tasisi yenye viongozi wenye chimbuko la maadili, siyo kama vyama vingine vinaongozwa na wenye vilabu vya usiku halafu eti navyo ni vyama vya kuweza kuongoza nchi”, alisema Mukama.

Alisema kutokana na CCM kuwa chama chenye chimbuko la maadili bora, ndiyo sababu kila kinapofanya uchaguzi wa kupata viongozi wake huwa ni wa kihistoria kwa kuwa anayepenya kuwa kiongozi huwa amepita kwenye tanuru la uchujwaji wa hali ya juu.

“Juzijuzi tulipokuwa tunateua majina ya wagombea, Kamati yetu ya maadili, haikuacha kuchunguza hatua kwa hatua na kwa makini kama kila aliyeomba uongozi anazo sifa bora na zinakidhi viwango vya kushinda anayetakiwa kuondolewa yeye abaki, hivi ndivyo chama chenye misingi ya uadilifu ya uongozi kinavyokuwa”, alisema Mukama na kuongeza:-

“Sasa hivi vyama vingine vinaweza kufanya mchujo wa aina hii? thubutu. Si mlisikia juzi juzi mbunge mmoja alijaribu kuonyesha nia ya kutaka uenyekiti wa Chama fulani, wee mliona alivyofurumushwa”.

Mukama alisema, wanaosema CCM inakufa ni wavivu kufanya tathmini au wanasema hivyo kudanganya watu na nafsi zao huku wenyewe wakiwa wanajua kwamba CCM ni imara tena kwa vigezo.

“Hivi jamani tujiulize na wao (wapinzani) wakitaka pia wajiulize chama chenye mwelekeo wa kufa kinaweza kupata wagombea ambao ni Wazee, Vijana kina baba na kina mama tena wengi wasomi kabisa waliobobea hadi ngazi za uprofesa, wanaokanyagana kwa wingi kama tulivyoona wakiomba uongozi katika nafasi mbalimbali? “, alihoji Mukama.

Alisema, tutokana na hali ya uchaguzi ndani ya Chama iliyojionyesha katika ngazi za mikoa, baada ya kumalizika ngazi ya taifa, CCM itakuwa itakuwa imara zaidi tayari kwa kutwaa dola tena baada ya uchaguzi mkuu wa 2015.

Katika hafla hiyo, wanachama wa Kata hiyo, waliuopongeza uongozi wa juu wa CCM kwa namna ulivyoweza kuweka taratibu zilizo wazi na za haki katika kuhakikisha uchaguzi ndani ya chama unazaa viongozi walio dhabiti.

Mapema, Mukama alikabidhi hati kwa vijanan na makamanda wa Umoja wa Vijana wa CCM, ambao wameshiriki katika shughuli mbali mbali za kuimarisha chama kwa namna moja au nyingine.