JK Atuma Salamu za Rambirambi kwa Jeshi la Polisi

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ameshtushwa na mauaji ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Liberatus Barlow yaliyotokea Mwanza.

Katika salamu za rambirambi alizompelekea Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Saidi Mwema, Oktoba 14, 2012, Rais Kikwete ameagiza jeshi hilo kuhakikisha linachukua hatua za lazima kuwakamata na kuwafikisha mbele ya sheria watu wote wanaotuhumiwa kupanga na kutekeleza mauaji hayo.

“Nimepokea kwa mshtuko mkubwa na huzuni nyingi taarifa za kifo cha ACP Liberatus Barlow kilichotokea usiku wa Ijumaa katika Jiji la Mwanza ambako watu wasiojulikana walimpiga risasi na kumwua ofisa huyo mwandamizi wa Jeshi letu la Polisi.”

“Historia ya ACP Barlow ni historia ya mfano katika Utumishi wa Umma na hususani katika Jeshi la Polisi. Kwa hakika, Jeshi la Polisi limempoteza kamanda hodari na wananchi waTanzania, hususani wale wa Mkoa wa Mwanza, wamempoteza mlinzi shupavu wa usalama wao na mali zao,” amesema Rais Kikwete katika salamu zake na kuongeza:

“Nakutumia wewe IGP salamu zangu za rambirambi kufuatia mauaji hayo. Kupitia kwako nalitumia Jeshi zima la Polisi pole zangu kwa kuondokewa na mwenzao katika mazingira yenye kutia uchungu sana. Aidha, kupitia kwako, naomba uniwasilishie salamu zangu za dhati kwa familia ya ACP Barlow ukiwajulisha kuwa niko nao katika wakati huu mgumu sana. Naungana nao katika kuomboleza kifo cha baba yako na mhimili wa familia yao na katika kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke pema peponi roho ya marehemu. Amen.”

Rais Kikwete pia ametumia nafasi hiyo kulitia moyo Jeshi la Polisi. “Kitendo hiki ni kazi ya watu waoga lakini nawasihi kitendo hicho kisiwakatishe tamaa katika kutekeleza wajibu wenu na kufanya kazi nzuri ambayo mnaendelea kuifanya katika nchi yetu ya kulinda usalama wetu na mali zetu,”
Ameongeza: “Badala yake kitendo hiki cha woga kiwahamasishe kuongeza kasi ya kudumisha usalama wa nchi yetu. Na kwa kuanzia, tuhakikishe kuwa wote walioshiriki katika kupanga na kutekeleza mauaji hayo wanakamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.”