Napenda kutumia fursa hii kuwapa taarifa kuhusu tukio la mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Kamishina Msaidizi wa Polisi Liberatus Barlow yaliyofanywa na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi usiku wa kuamkia Oktoba 13, 2012 majira ya saa saba usiku Mkoani Mwanza.
Tukio hilo limetokea wakati kamanda huyo akitokea kwenye kikao cha harusi ya ndugu yake eneo la Frolida hotel Mwanza mjini, akiwa na ndugu yake waliyeongozana nae kutoka kwenye kikao hicho. Wakati akimshusha huyo ndugu yake eneo la Kitangiri Minazi Mitatu, walitokea watu wanaosadikika kuwa ni majambazi, na kumvamia na kuanza kumshambulia kwa risasi na kumuua papohapo.
Ndugu wananchi, kufuatia tukio hilo, tayari nimemtuma Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai DCI Robert Manumba kwenda mkoani Mwanza kwa lengo la kuimarisha ulinzi na upepelezi wa tukio hilo.
Najua tukio hili limetushitua na kutuhuzunisha wote. Hivyo, wakati tukiendelea na taratibu zingine kuhusiana na tukio hilo, niwaombe wananchi wote kuwa watulivu na kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi, utakaowezesha kuwabaini wahalifu hao. Tutaendelea kuwapa taarifa za tukio hilo, kadri tutakavyoendelea kuzipata.
Hata hivyo alisema kuwa kutokana na tukio hilo jeshi la polisi linataraji kuanza uchunguzi wake kuanzia leo na timu ya askari kutoka makao makuu ya polisi wataondoka mapema leo kwenda jijini Mwanza kuungana na askari wa mkoa huo kwa ajili ya uchunguzi zaidi na msako wa majambazi hayo.
Mwema amewataka wananchi wa Mwanza kutoa ushirikiano wao kwa jeshi la polisi ili kufanikisha zoezi hilo na kuwataka kutokuwa na hofu yoyote kutokana na tukio hilo.