Waislamu Washambulia Makanisa Dar, Wachoma na Kuharibu Magari

Pichani ni Kanisa la KKKT eneo la Mbagala lililoshambuliwa kwa kuharibiwa madirisha na milango

Pichani ni Kanisa la Sabato eneo la Mbagala lililoshambuliwa kwa kuharibiwa madirisha na milango

Moja ya gari lililochomwa moto na waandamanaji hao

Gari la Kituo cha Clauds FM ambalo nalo lilishambuliwa kwa mawe na waandamanaji hao.

Gari hili nalo lilishambuliwa kwa kuvunjwa vioo na waandamanaji hao

Na Mwandishi Wetu

BAADHI ya Waumini wa Kiislamu wameandamana huku wakifanya fujo za kushambulia baadhi ya makanisa maeneo na kuharibu mali wakipinga kitendo cha mtoto mdogo (mkristo) kudaiwa kukojolea kitabu cha dini ya Kiislamu alipokuwa akibishana na mwenzake (wa kiislamu).

Makanisa yalioshambuliwa ambayo yote ni ya maeneo ya Mbagala Kizuiani ni pamoja na Kanisa la Anglikana, Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Tanzania (KKKT-Mbagala) na Kanisa la Sabato ambayo yamevunjwa vioo pamoja na kuharibu mali kama magari yaliyokuwa yameegeshwa eneo la kanisa na mengine waliokutana nao waandamanaji hao.

Baadhi ya waandamanaji hao wakiokota mawe na kuyapanga barabarani. (Picha zote kwa hisani ya GPL Blogu)

Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema mtoto mmoja (mkristu jina tunalo) akiwa katika michezo na mwenzake wa Kiislamu walianza kubishana, kuwa endapo ukikojolea kitabu cha dini ya Kiislamu (msaafu) lazima ugeuke kuwa kichaa, hivyo Josephat alibisha na kumwambia mwenzake anaweza kufanya hivyo na kutodhurika.

Baada ya mabishano hayo Josephat aliamua kukikojolea kile kitabu ili aone kama angelidhurika kama alivyoelezwa na mwenzake, lakini haikuwa hivyo. Hata hivyo baadaye yule wa kiislamu alitoa taarifa kwa wazazi wake ndipo yalianza mazungumzo kati ya wazazi kwa wazazi.

Kova alisema mvutano huo ulifika katika kituo kidogo cha polisi na ndipo baadhi ya Waislamu walianza kujitokeza na kutaka wapewe maelezo na kadri ya walivyoongezeka eneo la kituo hali ilianza kuwa mbaya kwani baadhi yao walionekana kutaka kufanya fujo na kuomba wapewe yule mtoto ili wamuadhibu.

Baada ya hali kuwa tete Jeshi la Polisi lilileta askari wa kutuliza ghasia FFU kuwataka waliokuwa kituoni kuondoka kwa amani lakini baadhi yao walipinga hivyo kuanza kutumia nguvu kuwatawanya. “Baada ya wananchi hao kutawanyishwa baadhi walijikusanya na kuzunguka huku wakifanya fujo kwa kushambulia makanisa na mali za watu,” alisema Kova akizungumza na chombo kimoja cha habari.