ECAPBA Yatoa Kibali cha Pambano la Ngumi Kati ya Mashali na Sebayala

Bondia kutoka nchini Tanzania, Thomas Mashali

Na Mwandishi Wetu

CHAMA cha Ngumi za Kulipwa cha Afrika Mashariki na Kati (ECAPBA) kimetoa kibali kwa promota Selemani Seminyo cha kuandaa pambano la kugombea Ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati katika uzito wa kati (middleweight), baina ya bondia Thomas Mashali wa Tanzania na Sebayala Med wa Uganda.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa pambano hilo litafanyika katika Ukumbi wa Friends Corner, Manzese, jijini Dar es Salaam, Oktoba 14, 2012. ECAPBA inajivunia kuwawezesha mabondia wengi kutoka katika nchi wanachama kuendeleza vipaji vyao kwa kugombea mikanda ya ubingwa wake.

Tanzania ina bahati ya kufanya mapambano mengi ya ubingwa wa ECAPBA na tunao mabondia wengi ambao ni mabingwa ikilinganishwa na nchi nyingine. Nchi wanachana wa ECAPBA ni pamoja na Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Malawi, Ethiopia, Sundan ya Kusini, DRC Congo na Zambia.

ECAPBA ilipendekezwa kuundwa mwaka 2004 baada ya kikao cha kwanza nchini Kampala Uganda katika hoteli ya Ghana kikiwashirikisha viongozi toka Tanzania, Kenya, Uganda, Zambia na Malawi na kufuatiwa na kikao cha uanzilishi mwaka 2004 katika hoteli ya Kilimanjaro Crane mjini Moshi, Tanzania.

ECAPBA inawaalika mapromota wengi kuandaa mapambano ya ubingwa kwa mabondia wengi kwani hii ji njia mojawapo ya kuinua viwango vya mabondai wetu.

Aidha, ECAPBA inawaomba wadau wa ngumi ikiwa ni pamoja na watu binafsi, makampuni, taasisi za serikali na binafsi zijitokeze kwa wingi kudhamini mapambano yake ya ubingwa kama njia mojawapo ya kuinua biashara zao na kuendeleza vipaji vya mabondia nchini. Shirikisho la Ngumi la Afrika ya Mashariki na Kati limesajiliwa nchini Tanzania ambako ndipo palipo na makao yake makuu kwa sasa.