Wabunge Waibana Serikali, Ni Kuhusu Kuzagaa kwa ARVs Feki

Dawa za kupunguza makali ya Ukimwi zinazodaiwa kuwa feki

Na Magreth Kinabo, Maelezo

KAMATI ya Bunge inayoshughulikia masuala ya Ukimwi imeishauri Serikali kutoa tamko la kuelezea ni hatua gani inaendelea kuchukua baada ya kusimamisha kazi baadhi ya viongozi wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD), kufuatia kuwepo kwa dawa bandia za kupunguza makali ya Ukimwi (ARV) katika kikao cha Bunge kitakachoanza mwishoni mwa mwezi huu.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Lediana Mng’ong’o wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam kuhusu kuwepo kwa dawa hizo.

“Sisi tungependa kuishauri Serikali kuendelea kufuatilia na hatua za kisheria pale itakapobaini katika uchunguzi huo ili tatizo hili lisiendelee kutokea,” alisema Lediana ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum Iringa.

Aliongeza kuwa wanaishauri Mamlaka cha Chakula na Dawa (TFDA) kuwa na wawakilishi katika kanda mbalimbali ili kuweza kudhibiti tatizo la kuwepo kwa dawa bandia.

Aidha kamati hiyo imelaani kampuni ambayo imeingiza dawa feki na imetaka hatua za kisheria zichukuliwe. Kamati hiyo imewataka watu wanaotumia dawa hizo kutoziacha, bali waendelee kuzitumia kwa kuwa dawa zote si feki na pia zipo za kutosha.