Na Mwandishi Maalumu, Tokyo, Japan
MAWAZIRI wa Fedha wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola wamekutana Oktoba 10, 2012 jijini Tokyo, kwa madhumuni ya kupitia kazi za jumuiya hiyo.
“Katika mkutano wetu tulikuwa na agenda kuu nne. Agenda ya kwanza ilikuwa ni juu ya ukosefu wa ajira kwa vijana; pili, tulizungumzia masuala yote ambayo yalitokana na mikutano iliyopita ambapo suala la ajira lilikuwepo; tatu, tulizungumzia jinsi ya kuhudumia madeni yetu kama nchi wanachama wa Jumuiya ya madola, kwani Jumuiyaya Madola inatoa tahadhari kuhusu madeni ambayo yanaweza yakaiathiri nchi mojawapo kwani kwa kuathirika kwa nchi moja kunaweza kuleta matatizo hata kama nchi nyingine ni tajiri; suala la nne lililozungumziwa katika mkutano huo lilikuwa ni juu ya kuimarisha uhusiano kati ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola na nchi zile za kundi la ishirini yaani ( G20),” alieleza Waziri wa Fedha wa Tanzania, William Mgimwa ambaye pia anahudhuria mkutano huo.
Waziri Mgimwa aliendelea kusema kuwa, Mkutano huo wa Mawaziri wa Fedha wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola ulifuatia mkutano wa Maofisa wa juu wa Serikali uliofanyika Oktoba 9, kwa kuwashirikisha Magavana wa Benki kuu. “Madhumuni ya msingi ya mkutano huu ni kujadili njia muafaka ambazo zinaweza kutatua matatizo yanayoukabili uchumi wa nchi zetu,” alisema Waziri Mgimwa.
Aidha katika mkutano na waandishi wa habari, Dk. Denzili. Douglas ambaye ndiye aliyeongoza mkutano huo alisema kuwa, pamoja na mambo yote manne ambayo wameyajadili, wanajitahidi sana kuhakikisha kuwa wanatilia mkazo juu ya kupambana na mtikisiko wa uchumi na kuweka vigezo ambavyo vitasaidia kuzuia kutetereka kwa uchumi wa nchi ambao ni wanachama wa Jumuiya hiyo na kuzuia matatizo ambayo yanaweza kuleta athari kiuchumi.
Mawaziri hao kwa pamoja pia walizungumzia suala la sekta Binafsi kwani kwa kufanya hivyo kutawawezesha kufikia malengo waliyojiwekea yaani malengo ya maendeleo ya Milenia ya 2015. Aidha Magavana wa Benki kuu walijadili pia changamoto zilizopo za kutokuwa na akiba za kutosha na dhamana katika Benki. Katibu Mkuu wa sekretarieti ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola, Kamalesh Sharma akitoa hitimisho kwa waandishi wa habari alisisitiza juu ya uimarishaji wa ushirikiano wa jumuiya hiyo na nchi za kundi la ishirini, G20.
“Nategemea nyie kama wanasiasa na mkiwa kama Mawaziri wa Fedha wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola, mtakuwa mawakili wazuri wa kuwaelimisha wanasiasa wenzenu na kuendeleza mjadala huu wa kuimarisha uhusiano wetu na nchi za kundi la ishirini (G20), bila hata kukaa kwenye meza na nchi hizo,” alisisitiza Sharma.
“Mkutano huo ulikuwa na mafanikio na wote kwa pamoja walikubaliana kuyatekeleza yote yaliyoazimiwa”. Alisema Mgimwa.
Mikutano hii ya jumuiya ya Madola inaenda sanjari na Mikutano ya mwaka ya Shirika la Fedha la kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia (World Bank), ambayo badoinaendelea hapa jijini Tokyo, hadi Oktoba 14.