Mchezo wa Ngumi Unavyopoteza Uasili Wake (Sehemu ya 11)

Ngumi

Na Onesmo Ngowi

MASUMBWI au kwa jina lingine ndondi au ngumi ni mchezo unapoendwa na watu wengi. Pamoja na hayo mchezo huu ni kati ya michezo inayoogopwa sana duniani. Mchezo wa ngumi uko hatarini kupoteza maana yake ya asili yaani kucheza kama burudani, kuwakilisha nchi na kujenga ushupavu wa mchezaji. Mamilioni ya watu wanaojazana kuutazama wasingependa kabisa kujiingiza kuucheza mchezo wa ngumi. Sasa endelea….!

Kuna ngazi mbalimbali katika mchezo ngumi zinazompa mdau yeyote nafasi ya kushiriki katika kuuendeleza mchezo wenyewe kwa jinsi anavyotaka. Ngazi hizi zimetejwa wazi wazi na sio lazima mtu awe tu kiongozi ndipo aweze kuchangia maendeleo kwenye mchezo wa ngumi. Baadhi ya ngazi zilizotajwa ni urefarii, ujaji, utunza muda, mtamngazaji wa ulingo, mkuzaji, mdhamini, meneja, kocha, mpanga mabondia nk. Mdau yeyote anayetaka kuchangia maendeleo ya mchezo wa ngumi anaweza kuchukua moja ya nafasi kati ya zilizotajwa hapo juu.

Hakuwezi kuwa na maendeleo kwenye mchezo wa ngumi kama wahusika waliotajwa hapo juu hawapo. Ni lazima kuwe kwanza na bondia na timu yake ya meeneja, kocha n.k ndipo promoter aweze kuandaa mpambano na mpinzani aliye na safu ya watu kama hao. Katika nchi zilizoendelea hususan Marekani na nchi nyingi za Ulaya bondia anatakiwa awe na kiwango kizuri ili ajiunge na ngumi za kulipwa. Kwa kuwa mchezo wenyewe wapenzi hulipa fedha nyingi kuuagalia wanategemea kuona mchezo mzuri hivyo wahusika lazima wawe na viwango vizuri vya ngumi.

Katika miaka ya 50 hadi 60 mabondia wengi wa ngumi za ridhaa waliokuwa wanashiriki na kushinda medali kwenye michezo ya Olympic, Jumuiya ya Madola, michezo ya majeshi ya dunia na mashindano mengine ya kimataifa walikuwa wakipata mameneja na mapromota wazuri kuanza michezo ya ngumi za kulipwa.

Mfano mzuri ni bondia Robert Wangila Napungi wa Kenya aliyeshinda medali ya dhahabu kwenye mashindano ya Olympic yailiyofanyika Korea ya Kusini mwaka 1988. Aliporudi tu nyumbani kwake Kenya mameneja wengi maarufu wa mchezo huo duniani walipigania kumchukua kwenye Kampuni zao.

Madau mbalimbali ya fedha yalitolewa na mameneja/mapromota hao hatimaye Bob Arum mmoja wa mapromota wakubwa duniani mwenye makao yake jijini Las Vegas, Nevada, Marekani akashinda na kumchukua. Kwa kuanzia tu Bob Arum alitoa kitita kisichopungua dola za Kimarekani laki 2 na nusu ili kupata sahihi ya Wangila ambaye alikuwa hajui hata baba yake mzazi (kwani alituzwa na nyanya yake tu). Kwa muda mfupi tu aliweza kununua nyumba ghali na ya kifahari kwenye eneo la Muthaiga ambalo hujulikana kuwa ni la matajiri jijini Nairobi pamoja na magari ya kifahari kabla hata hajarusha ngumi moja ya kulipwa.

Viwango vizuri vya bondia anayeanza ngumi za kulipwa ndivyo vinavyoweza kumhakikishia bondia mwanzo mzuri kwenye ngumi za kulipwa. Lakini viwango hivyo sio kikwazo kwa bondia kujiunga na ngumi za kulipwa. Wapo mabondia wengi wa miaka ya karibuni waliong’ara kwenye medani ya kimataifa bila ya kushiriki au kuwa mabingwa wa mashindano ya Olympic au Jumuiya ya madola. Kundi hili linaongozwa na bondia anayejulikana sana kwa wengi kama kielelezo cha mchezo huu kwa miaka ya karibuni, bondia Mike Tyson wa Marekani.

Bondia huyu sio tu kama alikuwa bondia wa kwanza wa umri mdogo kuwahi kuwa bingwa wa ndondi wa uzito wa juu duniani, bali alikuwa pia bondia wa kwanza kuweza kupata kitita kikubwa cha fedha toka kwenye ngumi. Wakati Tyson alipokuwa bingwa wa uzito wa juu duniani alikuwa na umri wa miaka 20 na aliweza kukusanya zaidi ya dola za Kimarekani milioni 300 kiasi ambacho hakijawahi kufikiwa na bondia mwingine yeyote duniani. Pamoja na kwamba fedha nyingi kati ya hizo zilitumika vibaya kwa ajili ya ushauri mbovu ni dhahiri kuwa kwa fedha hizi Mike Tyson alikuwa mmoja wa matajiri waliotukuka duniani.

Kwa hapa Afrika tunao mabondia walioweza kujikusanyia fedha na sifa nyingi katika medani ya mchezo huu wa ngumi. Baadhi yao wakiongozwa na Dick Tiger wa Nigeria, John Kotey wa Ghana, Azumah Nelson wa Ghana, Lottie Mwale wa Zambia, Ayubu Kalule, Bonza Edward na John Mugabi wote wa Uganda pamoja na utitiri wa mabondia wa Africa ya Kusini wakiongozwa na Dingan Thobela (Rose of Soweto) Baby Jacky Matlala, Francis Botha na wengine wengi. Nchini Tanzania tumebahatika kuwa na baadhi ya mabondia mabingwa wa Dunia wa vyama vya ngumi kama WBU, IBU, UBO mabondia hawa ni Rashid Matumla, Magoma Shaban, Mbwana Matumla, Francis Cheka na Karama Nyilawila.

Kama nilivyokwisha eleza hapo juu viwango na misingi mizuri ndiyo njia pekee ya mafanikio mazuri kwenye ngumi. Wengi wa mabingwa wa ngumi toka Afrika wanapata nafasi ya kuwa mabingwa wa dunia kwa kuongozwa na mameneja au mapromota toka nje ya bara hili. Hii imetokana na uelewa pamoja na uwezo wa kifedha wa mameneja na mapromota hao toka nje ya Afrika.

Ili kumpata bondia mzuri atakayeweza kushinda vizuri meneja au promota wa bondia hana budi kuwekeza kwa bondia husika. Kwa maana nyingine bondia ni kama mtambo wa meneja au promota wa kuzalisha fedha. Ili mtambo wenyewe uweze kuzalisha fedha hauna budi kuandaliwa na kutunzwa vizuri. Hatua mbalimbali zinatakiwa zifuatwe ili bondia aweze kuwa mwenye nafasi nzuri ya kutengeneza fedha.

Hatua hizi ni kama ifuatavyo; Meneja anapaswa kumtafutia bondia wake kocha aliye na uwezo wa kumwandaa ili awe na hali mzuri kimchezo wakati wowote. Meneja anatakiwa awajue wapanga mabondia (Matchmakers) mbalimbali ambao hutumiwa na mapromota kuwapanga mabondia katika mapambano wanayoandaa. Meneja anatakiwa ampate daktari atakaye mhudumia bondia wake wakati wowote ule.

Meneja anatakiwa kuhakikisha kuwa anavyo vifaa muhimu vya kumwandaa bondia wake pamoja na lishe bora. Meneja anatakiwa kumtetea bondia wake katika mikataba mbalimbali ili wote wanufaike. Meneja anatakiwa amlinde bondia wake asipigane mara nyingi kuliko anavyotakiwa ili kuzuia asije akachuja kimchezo. Yote haya yanahitaji fedha kwa hiyo meneja anatakiwa awekeze kwa bondia muda mrefu ili fedha zake ziweze kurudi na hatimaye atengeneza faida.

Mabondia wengi hapa Afrika hususan Tanzania hawana mameneja wenye uwezo wa kuwa meneji. Ama watu wenyewe wanaojiita mameneja hawajui maana halisi ya kumeneji mabondia au ni watu wanaotaka tu kumtumia bondia kwa manufaa yao wenyewe. Mabondia nao hawajui taratibu husika za kuwa na meneja mzuri.

Wenzetu wa Ulaya na Marekani hata Asia na Amerika ya Kusini na baadhi ya nchi za Africa wamepiga hatua kubwa kwenye jambo hili. Hii inatokana na ukweli kwamba mchezo wa ngumi unahesabika kama ajira na kuheshimiwa na serikali za nchi zao.

Bondia wa kulipwa na baadhi ya mabondia wa ngumi za ridhaa wanalipa kodi kutokana na mapato anayopata. Hali hii inawaweka katika nafasi nzuri ya kuwa na mtiririko mzima wa uongozi katika mchezo wenyewe. Serikali za wenzetu zinathamini michango inayotolewa na michezo ya ngumi sio tu kwa kuwaletea mikanda ya ubingwa bali kwa kuchangia kwenye pato la taifa. Pambano moja tu ambalo bondia Mike Tyson alilocheza na Lenox Lewis liliingiza zaidi ya dola za kimarekani milioni 780.

Fedha hizi zinatokana na ulipaji wa matangazo mengi ya kibiashara wakati wa matayarisho ya mpambano na siku yenyewe ya mpambano. Kituo kimoja tu cha television kinaweza kumlipa promota wa mpambano kiasi cha mamilioni ya dola za kimarekani ili kurusha pambano lenyewe. Kituo hiki baadaye kinaviuzia mpambano huu vituo vingine vya television vya nchi mbalimbali na hivyo kutengeneza fedha lukuki. Hii ndio sababu bondia mmoja anaweza kulipwa kiasi cha dola za kimarekani milioni 20 na kuendelea.

Utaratibu huo wa kupromoti na kutangaza biashara hapa kwetu Afrika hususan Tanzania bado haujaanza kueleweka. Ni nchi chache sana Afrika ambapo vituo vya television vinaweza kulipa promota wa pambano fedha ili walirushe kwa watazamaji wake. Nchini Afrika ya Kusini na Namibia kuna utaribu wa television kuwalipa mapromota angalau fedha kiasi kwa ajili ya kurusha mapambano ya ngumi. Utaratibu huo hapa kwetu Tanzania bado haujaanza.

Kiasi cha fedha nyingi ambazo bondia hulipwa hutokana na fedha zinazotoka kwenye matangazo ya biashara. Nyingi ya fedha hizi zinaweza tu kupatikana kama vituo vya television vinarusha mapambano husika. Namna nyingine ya kupata fedha kwenye promosheni ya mpambano wa ngumi ni kwa kampuni mbalimbali zinazotaka kutangaza bidhaa zao. Kampuni hizi ama hutumia mpambano husika au bondia mmoja mmoja kwa kuingia naye mkataba wa kuitangazia biashara zake. Japokuwa utaratibu huu umeshaanza kutumika hapa Tanzania lakini kiwango chake ni kidogo sana.

Maajenti mbalimbali wa matangazo ya biashara ndio husimama kati ya kampuni hizi na wanamichezo. Sio rahisi bondia kujipeleka mwenyewe kwenye kampuni husika kwa minajili ya kutafuta mikataba. Mameneja wa mabondia wanatakiwa wawatafutie mikataba mbalimbali yenye manufaa kwa wote wawili. Makampuni nayo yanatakiwa yaelewe dhana nzima ya kuwatumia mabondia kupromoti bidhaa zao. Juhudi hizi za kuelimishana zinatakiwa zifanywe na taasisi za michezo zikishirikiana na vyombo husika vya dola.

Kwa kuwa michezo hususani ngumi ni ajira inatakiwa ipewe kipaumbele na serikali ili iweze kuchangia pato la taifa. Serikali ikiweza kushirikiana vyema na vyama au taasisi husika mchango wa mchezo wenyewe unaweza kuchangia kupunguza tatizo la ajira.

Ikumbukwe kwamba bondia mmoja tu anaweza kuwapa watu wafuatao kazi: Meneja, Kocha, Daktari, Cutman, Mechi Meka, Promota, Refarii, Jaji pamoja na watu wengi wanaouza bidhaa na huduma kadhaa wa kadha. Tukiwa na mabondia wengi walio kwenye viwango vizuri ni wazi kwamba namba ya watu waliotajwa hapo juu ingeongezeka kwa kiasi kikubwa. Mchango wao katika pato la taifa ni mkubwa sana kwani kila mmoja wao atalipa kodi na kutunza vyema familia yake. Iaendelea…!

Mwandishi wa makala haya ni; Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC), Shirkisho la Ngumi za Kulipwa Afrika Mashariki na Kati (ECAPBF), Shirikisho la Ngumi la Kimataifa bara la Afrika, Masharilki ya Kati, Ghuba ya Uarabu na Uajemi (IBF/AFRICA) na Mkurugenzi wa Baraza la Ngumi la Jumuiya ya Madola (CBC) E-mail: ibfafrica@yahoo.com