Na Mwandishi Wetu
KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Charles Kenyela anatarajia kuwa mgeni rasmi katika pambano la kuwania Ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati baina ya Thomas Mashali wa Tanzania na Medi Sebyala wa Uganda litakalofanyika Oktoba 14, Siku ya kumbukumbu ya Baba wa Taifa (Mwalimu J.K. Nyerere) kwenye ukumbi wa Friends Corner Manzese jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, Mratibu wa pambano hilo linalosimamiwa na Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO), Regina Gwae, alisema mbali na Kamanda Kenyela, kutakuwa na wageni wengine maalumu akiwemo Mbunge wa Kinondoni, Iddi Azan.
Alisema wanashukuru kwa ushirikiano wa viongozi hao katika maandalizi na hatimaye wamethibitisha ushiriki wao katika pambano hilo ambalo linavuta hisia za watu wengi na wapenzi wa ngumi jijini Dar es Salaam.
Alitaja mapambano manne ya utangulizi ya siku hiyo ambapo Abdul Awilo atazichapa na Shedrack Juma, Selemani Shaaban atavaana na Hamisi Mohamed huku Jonas Segu akinyukana na Ibrahim Class wakati Charles Mashali atatwangana na Teacher Aaron.
“Tumeamua kuchukua mabondia kutoka katika klabu zenye mashabiki wengi, tumechukua kwa Mzazi tumechukua klabu ya manzese anakotoka Mashali na Super D Boxing Club,’ alisema Regina.
Regina alisema, bondia Medi Sebyala na Kocha wake wanatarajiwa kuwasili nchini Oktoba 11 na tayari maandalizi ya safari yao yamekamilika, ikiwemo kuwatumia tiketi na wameshazipokea.
Mratibu huyo, aliishukuru kampuni ya Promasidor wasambazaji wa Sossi Poa, Gazeti la Jambo Leo, City Sports Lounge na Times FM kwa kuwa bega kwa bega kuhakikisha pambano hilo linafanikiwa na kuwa, milango bado iko wazi kwa wadau kujitokeza kufanikisha mchezo huo ambao ni chanzo cha ajira kwa vijana.