Tanzania Kujitangaza Kiutalii Kwa Kutumia Vyakula vya Asili

Mkurugenzi Mwendeshaji wa Bodi ya Utalii Nchini Dk. Aloyce Nzuki (kushoto) akimkaribisha mpishi maarufu Duniani kutoka nchini India, Sanjeev Kapoor ili azungumze na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam. Mtaalamu huyo alizungumzia umuhimu wa vyakula vya asili katika sekta ya utalii wa utamaduni. Kulia ni Naibu Meneja Mkuu wa Hoteli ya Serena, Daniel Sambai ambayo imegharamia gharama za chakula na maladhi kwa mpishi huyo kwa kipindi chote akiwa nchini. Picha na Anna Nkinda – Maelezo

Na Magreth Kinabo, Maelezo

BODI ya Utalii Tanzania, imeandaa mpango maalumu wa kutangaza utalii wa kiutamaduni, kwa kutumia filamu itakayoonesha vyakula vya kiasili vya Kitanzania kwa kushirikiana na mpishi maarufu duniani kutoka nchini India, Sanjeev Kapoor.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Alyce Nzuki wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Hoteli ya Serena iliyopo jijini Dar es Salaam.

“Bodi ya utalii Tanzania imeona ni fursa kutangaza utalii wa kiutamaduni kwa kumtumia mpishi huyu maarufu ambaye atatengeneza filamu ya kuonesha utalii wa kiutamaduni kwa kutumia vyakula vya Kitanzania. Filamu hii itaorushwa katika runinga yake ya ‘Food Food Channel,” alisema Nzuki.

Nzuki aliongeza kuwa filamu hiyo itaoneshwa nchini India na duniani kote hususan Asia hivyo itasaidia kukuza utalii na kukuongeza idadi ya watalii nchini.

Naye mpishi huyo, Kapoor alisema ni mara yake ya kwanza kutembelea Tanzania, hivyo atatumia nafasi hiyo ili kuweza kuutangaza utamaduni huo ipasavyo kwa kuangalia vivutio mbalimbali kupitia filamu hiyo kwa kutumia kipindi cha ‘Out of The World’.

Alisema kipindi chake huwa kinatazamwa na watu wapatao milioni 40 kutoka nchi mbalimbali. Mpishi huyo anatarajiwa kuhudhuria hafla ya kuchangaisha fedha kwa ajili ya watoto wenye matatizo ya moyo jioni itakyofanyika kwenye hoteli hiyo.