Na Mwandishi Maalumu, Tokyo – Japan
WAZIRI wa Fedha Dk. William Mgimwa amekutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi namba moja la Kanda ya Afrika anayewakilisha nchi za Afrika kwenye Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF), Moeketsi Majoro.
Hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete alimteua, Dk. William Mgimwa kuwa Waziri wa Fedha nchini Tanzania na hii ni mara ya kwanza Waziri wa Fedha na Gavana wa Benki ya Dunia kuhudhuria mikutano ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Ulimwenguni inayofanyika nchini Tokyo, Japan.
Katika mikutano hiyo, Mgimwa amefanikiwa kuonana na Moeketsi na kufanya mazungumzo naye mbalimbali mojawapo likiwa ni jinsi gani Tanzania inaweza kufaidika na IMF na kuinua uchumi wake kupitia shirika hilo.
“Nina mambo muhimu manne ambayo ukisaidia kufikisha ujumbe huu na kama tutafanikiwa kupata fedha hizo tutakuwa tumepiga hatua sana katika kuinua uchumi wa nchi yetu. Moja, ni kurekebisha barabara zetu na kuziweka katika viwango vinavyotakiwa, pili ni mfumuko wa bei, kwa kweli mfumuko wa bei umekuwa ukisababishwa na upandaji wa bei za bidhaa hasa vyakula kama vile mahindi lakini tumegundua kuwa mchele unapanda sana hata kuzidi mahindi, tatu ni hii hali ya Tanesco, kwa kweli umeme umekuwa ni tatizo kwetu pamoja na jitihada zote tunazozifanya na hasa za kutumia gesi.” alisema Mgimwa akizungumza na Moeketsi.
Aliendelea kusema kuwa tunahitaji kuimarisha masoko ya ndani na kuwa na dhamana za kutosha, pamoja na kuwa tumeandaa mipango kabambe ambayo itatusaidia katika kutekeleza haya lakini bado tunahitaji nguvu kutoka shirika la fedha la kimataifa”.
Naye Moeketsi alifurahishwa na uelewa wa Mgimwa na kumhaidi kufuatilia kwa karibu, kwani mambo yote aliyoyaeleza ni ya msingi na kwasababu yako kwenye mpango mzuri ya taweza kutekelezeka. Mazungumzoya Mgimwana Moeketsi yamefungua mianya mipya na mahusiano ya karibu kati ya shirika la Fedha la kimataifa na nchi ya Tanzania.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Benno Ndulu, Kamishna wa fedha za nje, Said Magonya, Bi. Mwanaidi Mtanda ambaye ni Mhasibu Mkuu wa Serikali, Beda Shallanda ambaye ni Kamishna wa sera, Bi. Monica Mwamunyanye ambaye ni Kamishna wa Bajeti, Ahmed Rutashobola ambaye ni mwakilishi wa Tanzania huko IMF na baadhi ya maofisa kutoka Benki Kuu na Wizara ya Fedha.
Aidha Mgimwa alimalizia kwa kueleza kuwa Tanzania imejitahidi sana kupunguza deni la Taifa na vilevile inafanya jitihada za kuimarisha usimamiaji wa deni hilo kwa kuhamishia jukumu hilo Wizara ya Fedha ili kuweka usimamizi na udhibiti wa karibu zaidi. Nchi za Afrika zimegawanywa katika makundi matatu na Moeketsi anaziwakilisha nchi ishirini na moja za Afrika ambazo ziko kwenye kundi la kwanza.