KAMATI ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ilikutana Oktoba 5 mwaka huu kupitia na kufanya uamuzi katika masuala mbalimbali na kupanga Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ianze kutimua vumbi Oktoba 20 mwaka huu.
Timu zimepangwa katika makundi matatu ya timu nane nane ambapo zitacheza ligi hiyo kwa mtindo wa nyumbani na ugenini. Mshindi wa kila kundi ndiye atakayepata tiketi ya kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao wakati timu ya mwisho kila kundi itashuka daraja kurudi Ligi ya Mkoa.
Kundi A lina timu za Burkina Moro ya Morogoro, Kurugenzi Mufindi ya Iringa, Majimaji ya Songea, Mbeya City ya Mbeya, Mlale JKT ya Ruvuma, Mkamba Rangers ya Morogoro, Polisi Iringa na Small Kids ya Rukwa.
Ndanda FC ya Mtwara, Ashanti United, Green Warriors, Moro United, Polisi, Tessema, Transit Camp na Villa Squad zote za Dar es Salaam ndizo zinazounda kundi B wakati kundi C ni Kanembwa JKT ya Kigoma, Morani ya Manyara, Mwadui ya Shinyanga, Pamba ya Mwanza Polisi Dodoma, Polisi Mara, Polisi Tabora na Rhino Rangers ya Tabora.
Ada ya ushiriki wa ligi ni sh. 200,000 zinazotakiwa kulipwa kabla ya Oktoba 13 mwaka huu. Pia Oktoba 13 mwaka huu kutakuwa na kikao kati ya wenyeviti wa klabu zote zinazoshiriki ligi hiyo na Kamati ya Ligi ambapo pia itafanyika draw (ratiba).
MECHI YA KAGERA SUGAR, YANGA YASOGEZWA
Kamati ya Ligi imesogeza mbele kwa siku moja mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Kagera Sugar na Yanga iliyokuwa ichezwe Oktoba 7 mwaka huu mjini Bukoba kutokana na Uwanja wa Kaitaba kuwa na shughuli nyingine za kijamii.
Sasa mechi hiyo itachezwa Oktoba 8 mwaka huu kwenye uwanja huo huo. Mabadiliko hayo pia yameathiri mechi kati ya Toto Africans na Yanga iliyokuwa ichezwe Oktoba 10 mwaka huu Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza. Mechi hiyo sasa itachezwa Oktoba 11 mwaka huu.
WAAMUZI WATATU WAONDOLEWA, SIMBA YAPIGWA FAINI
Kamati ya Ligi imewaondoa waamuzi watatu wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kwa kushindwa kumudu michezo waliyopangiwa. Waamuzi hao ni Mathew Akrama wa Mwanza aliyechezesha mechi namba 80 ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Yanga na Simba iliyochezwa Oktoba 3 mwaka huu.
Wengine ni Paul Soleji wa Mwanza aliyechezesha mechi kati ya Simba na Tanzania Prisons, na mwamuzi msaidizi namba mbili kwenye mechi hiyo Mwarabu Mumbi wa Morogoro. Pia mwamuzi msaidizi namba mbili wa mechi ya Yanga na Simba, Ephrony Ndissa wa Dar es Salaam amepewa onyo.
Kamishna wa mechi namba 28 kati ya Yanga na African Lyon, Pius Mashera ameondolewa kwenye orodha ya makamishna wa ligi hiyo kwa kuchelewa kufika kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (Pre match meeting) na uwanjani.
Vilevile Mashera kwenye ripoti yake aliwasilisha malalamiko dhidi ya msimamizi wa kituo cha Dar es Salaam, na kwa vile suala hilo ni la kinidhamu ametakiwa alipeleke kwenye Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya TFF.
Nayo Simba imepigwa faini ya jumla ya sh. 600,000 kwa kuchelewa kufika kwenye pre match meeting ya mchezo wao dhidi Tanzania Prisons (sh. 100,000) na kwa washabiki wake kuwatupia chupa za maji waamuzi wa mechi hiyo (500,000).
Pia Kamati ya Ligi imeagiza kuwa kwa vile suala la kipa Shabani Kado wa Mtibwa Sugar kudaiwa kumpiga kiongozi mmoja wa Ruvu Shooting mara baada ya mechi kati ya timu hizo iliyochezwa Uwanja wa Azam Complex ni la kinidhamu lipelekwe kwenye Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya TFF.
YANGA, AFRICAN LYON KUTOVAA BEJI YA MDHAMINI
Kwa vile msimu huu mdhamini mwenyewe ndiye anayegawa vifaa kwa timu, Kamati ya Ligi imeagiza Vodacom iandikiwe barua na nakala kwa klabu zote ili kujua timu ambazo tayari zimekabidhiwa vifaa hivyo zikiwemo logo na siku ambapo timu husika zilipokea. Baada ya majibu ya Vodacom ndipo Kanuni za Ligi Kuu zitakapotumika kutoka adhabu kwa timu ambazo zitabainika kuwa zilipokea vifaa lakini hazikuvitumia.