PROMOTA maarufu wa ngumi za kulipwa kutoka nchini Misri, Richard Nwoba kutoka kampuni ya “Louaa Boxing Promotions” ametembelea ofisi za IBF zilizoko jijini Dar-es-Salaam ili kuangalia uwezekano wa kupromoti mapambano ya ngumi katika Ukanda wa Mashariki na Kati.
Nwoba akiwa nchini Tanzania alikutana na Rais wa IBF Afrika, Mashariki na Kati, Ghuba ya Uarabu na Uajemi , Onesmo Alfred McBride Ngowi na kufikia makubaliano ya kushirikiana na makampuni matatu ya Tanzania kuendeleza kazi hiyo ya kupromoti mapambano nanne ya ubingwa wa IBF Mwezi wa Novemba, 2012.
Alisema katika makubaliano hayo mabondia kadhaa wa Tanzania, Kenya na Misri watapambana kuwania mataji manne ya IBF Afrika, Mashariki ya Kati, Ghuba za Uarabu na Uajemi.
Aidha makubaliano hayo yalizaa matunda ya kupromoti mpambano wa ngumi katika Ghuba ya Uarabu ambapo bondia Francis Cheka wa Tanzania atachuana na mbabe wa Oman Amin Saad Mabrook Bait-Saleem katika mpambano wao wa mwezi wa Novemba!
Richard Nwoba ni bondia wa zamani wa ngumi za kulipwa wa uzito wa juu na sasa makao yake makuu yako katika jiji la Cairo, Misri ambako anaendesha biashara ya ulinzi wa makampuni pamoja na kupromoti ngumi za kulipwa akiendesha kampuni ya “Louaa Boxing Promotions”.