Serengeti Boys Kuvunja Kambi

Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura

Na Mwandishi Wetu

TIMU ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) ambayo imepata tiketi ya kucheza raundi ya tatu ya michuano ya Afrika baada ya Misri kujitoa itavunja kambi yake kwa mechi ya kirafiki dhidi ya kikosi cha Yanga cha U20.

Mechi hiyo itachezwa Oktoba 6 mwaka huu Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam kuanzia saa 10.30 jioni. Kiingilio kwenye mechi hiyo kitakuwa sh. 2,000 tu.

Wakati huo huo; Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) imeongeza muda kwa wagombea kuchukua fomu kwa ajili ya uchaguzi wa chama hicho utakaofanyika katikati ya mwezi ujao.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TAFCA, Ramadhan Mambosasa, jana ndiyo ilikuwa mwisho wa kuchukua fomu lakini mwitikio wa wagombea umekuwa mdogo ambapo ni watano tu waliojitokeza.

Hivyo, amesema wameongeza muda wa kuchukua na kurudisha fomu ambapo mwisho itakuwa ni Oktoba 9 mwaka huu saa 10 kamili alasiri. Fomu zinapatikana ofisi za TAFCA ambazo ziko Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.

Nafasi zinazogombewa ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Katibu Msaidizi, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF, Mhazini na wajumbe watatu wa Kamati ya Utendaji.